MSAFARA wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, umepigwa mawe na wananchi waliojitokeza kuzungumzia kero ya daraja la Matarawe, ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya watatu mwezi Oktoba mwaka huu.
Tukio
hilo limetokea jana saa 10:00 jioni hadi saa 12:00, ambapo wananchi
hao wakiwa na hasira walifanya fujo wakimshinikiza Nchimbi ambaye ni
Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini awasaidie kupanua daraja hilo ambalo
kwa muda mrefu limesababisha kutokea kwa ajali za mara kwa mara katika
eneo hilo.
Wananchi
hao wa Kata ya Matarawe, Manispaa ya Songea, wakiwamo waendesha
pikikipiki maarufu kwa jina la ‘yeboyebo’ walifunga barabara kwa zaidi
ya saa mbili huku wakifanya fujo za kung’oa kingo za daraja, kuweka
magogo na mawe katikati ya daraja na kuchoma matairi moto ili kumzuia
kiongozi huyo asiweze kupita na atoe majibu ya kina juu ya daraja hilo.
Hatua
hiyo ilililazimu Jeshi la Polisi kuwatawanya wananchi hao kwa
kuwafyatulia mabomu ya machozi ili kukabiliana na uharibifu pamoja na
kuruhusu msafara huo uweze kupita.
Aidha, kufuatia vurugu hizo, Jeshi la Polisi liliweza kuwashikilia watu wanane.
Hata
hivyo Dk. Nchimbi alilazimika kusimama na kushuka kwenye gari lake
akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali akiwamo
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Joseph Mkirikiti, ambapo aliwapa pole
kwa ajali zinazotokea huku akiwataka kuwa na subira wakati ombi lao
linashughulikiwa.
“Natoa
pole sana kwa msiba na ajali ambazo zimetokea nimewasikia, na
ninaahidi nitawajengea daraja hili, kama nimeweza kujenga barabara hii
kwa kiwango cha lami bila maandamano wala kufungiwa barabara
nitashindwa daraja?” alihoji.
Nchimbi
alisema kuwa vitu hivyo vinavyozungumzika hakuna haja ya kufanya
maandamano na kuwataka wananchi hao kuhudhuria mkutano wake kwa kuwa
anajua ufinyu wa daraja hilo na ameahidi kulifanyia maboresho zaidi.
Naye
Diwani wa kata hiyo, James Makene, aliungana na kundi la wananchi hao
na kumueleza Nchimbi kuwa hiyo ni changamoto ambayo wakazi wake
wamekuwa wakilia kwa kipindi kirefu.
Aidha,
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Deusdedit Msimeki, alisema kuwa kufuatia
vurugu hizo tayari watu wanane wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa
zaidi ili kuwabaini vinara wengine waliosababisha fujo hizo.
TANZANIA DAIMA
TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment