Home » » Wanakijiji wapigwa mabomu

Wanakijiji wapigwa mabomu

Vurugu kubwa zimetokea katika kijiji cha Ntunduwalo, wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma na Jeshi la Polisi kulazimika kufyatua mabomu ya machozi baada ya wakazi wa kijiji hicho kufunga barabara kuzuia magari yaliyobeba makaa ya mawe yasipite wakishinikiza hadi walipwe fidia.

Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi wakati magari hayo yaliyobeba makaa ya mawe kutoka mgodi wa Mngaka yalipofika katika kijiji hicho, wananchi walijipanga barabarani kuyazuia na kusababisha vurugu ambazo baadaye zilizimwa na polisi waliofika eneo la tukio.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deudedit Nsimike alisema kufuatia vurugu hizo, watu 20 wakiwamo Mwenyeviti wa serikali ya kijiji hicho na maofisa watendaji wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano zaidi.

Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Mwenyekiti wa serikali ya kijiji  cha  Ntunduwalo, John  Nyimbo  (36), Matrida Nchimbi (49) ambaye  ni Afisa Mtendaji wa kata ya Rwanda, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ntunduwalo, Joachim Ngaponda, Mwenyekiti wa kamati ya miradi ya kijiji hicho, Garusi Komba  (49 na John  Joachim Mahai  (45), mkazi wa kijiji cha Malindindo.

Kamanda Nsimike alisema wanakijiji hao waliyazuia magari hayo kwa lengo la kuishinikiza serikali iwalipe nyongeza ya fidia ambayo  wanadai kwa muda mrefu.

Alisema wananchi hao wanadai kuwa malipo waliyolipwa awali baada ya eneo lao kuchukuliwa na mwekezaji aliyenunua mgodi huo, walipunjwa wakati wanafanyiwa tathmini ya mali zao kutokana na serikali kutumia sheria ya zamani badala ya sasa.

 Aliongeza kuwa wananchi hao katika kufanikisha azma yao, waliwatanguliza wanawake na watoto mbele na kukaaa katikati ya barabara huku wakidai kuwa wamechoshwa na ahadi za serikali zisizotekelezeka.

Alisema kabla ya wananchi hao kutekeleza mkakati huo, Katibu Tawala Wilaya ya Mbinga, Idd Mponda, aliwasihi waondoe kizuizi ili magari yaendelee na kazi ya kusomba makaa ya mawe, lakini walikataa na kumweleza kuwa hawamuitaji kumuona yeye pamoja na watu wengine wala Mkuu wa wilaya hiyo bali wanachotaka walipwe fedha zao wanazodai na si vinginevyo.

Aidha, Kamanda Nsimeki alisema pamoja na polisi  kuwashikilia wanakijiji hao jana asubuhi vurugu  zilirejea tena na kwamba polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya  wanakijiji hao.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu, amesema kuwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngasa kukutana na wananchi hao wakati mgogoro huo ukitafutiwa ufumbuzi.

Wanakijiji hicho kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita wamekuwa wakiidai serikali sehemu ya fedha ya fidia ambayo hawakulipwa badala yake kampuni ya Tancol ilipewa kazi ya kuchimba madini hayo chini ya usimamizi wa NDC.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa