Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limekataa mkataba wa kununua umeme wa makaa ya mawe kwa gharama kubwa kutoka Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), kwa kuwa utavuruga mpango wao wa kupunguza gharama ya umeme kwa wananchi.
Akizungumza juzi mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Meneja Uzalishaji wa Tanesco Makao Makuu, Costa Rubagumya, alisema bei ya umeme wa NDC kwa Tanesco ni kubwa, tofauti na mapendekezo yao kwa shirika hilo la maendeleo.
Kwa mujibu wa Rubagumya, NDC wanataka kuiuzia Tanesco uniti moja ya umeme kwa dola za Marekani senti 9.5, wakati Tanesco walipendekeza iwe dola za Marekani senti saba, ili wafanikishe lengo la kuwauzia wananchi umeme kwa gharama ya chini.
“Kwanza hawa si wazalishaji umeme, bali ni madalali, kwa sababu wakishaingia mkataba na sisi Tanesco, watatafuta mtu mwingine wa kuzalisha umeme, wao ni wachimba madini,” alisema Rubagumya.
Msimamo huo wa Tanesco, ulitolewa wakati Maswi alipotembelea mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, unaoendeshwa na kampuni ya Tancoal kwa ubia na NDC.
Salamu mbaya
Katika hatua nyingine, msimamo huo wa Tanesco ni salamu mbaya kwa wafuaji umeme wa kutumia mafuta mazito na dizeli, ambao wamekuwa wakiiuzia Tanesco umeme kwa bei ghali maradufu, kuliko hiyo ya senti 9.5 ya NDC ambayo imekataliwa.
Maswi mwenyewe alikiri kuwa ni matarajio yake kwamba mgodi huo ukianzishwa, utasaidia kutatua tatizo la umeme unaozalishwa na kuendeshwa kwa gharama kubwa za mafuta.
Wafanyabiashara hao bei yao ni kati ya dola za Marekani senti 33 na 50, wakati Shirika hilo la Umeme linalazimika kuuza umeme kwa Watanzania kwa kati ya dola za Marekani senti 10 mpaka 19, hivyo kujikuta shirika likijiendesha kwa hasara.
Hali hiyo ilisababisha mwanzoni mwa mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kuchakata gesi Mtwara na Lindi, kuahidi kupambana na wafanyabiashara hao mara tu gesi itakapofika Dar es Salaam, ili washushe bei ya umeme wanaouza Tanesco mpaka angalau senti za Marekani nane kwa uniti moja.
Unyonyaji Tanesco
Kwa mujibu wa Pinda, kutokana na bei ya sasa ya wafanyabiashara hao wanaotoa karibu asilimia 80 ya umeme wote wa Gridi ya Taifa, shirika hilo limekuwa likinyonywa karibu Sh bilioni nne kila siku.
“Sisi tunaona kuwa suluhu ya kuondokana na gharama hizi ni gesi, lakini kuna watu wanajua watanyang’anywa tonge mdomoni, vita hii tunaijua; lakini sisi hatuwezi kurudi nyuma katika hili ni lazima tuendelee mbele,” alisema Pinda.
Alisema kuna watu kwa sasa wananufaika na kitendo cha Tanesco kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme. Alisisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuachana na umeme huo wa mafuta.
Alisema kama wafanyabiashara hao, watataka kuendelea na biashara ya kuuzia Tanesco umeme ni vyema wabadilishe mitambo yao iwe ya gesi na sio ya mafuta, kama ilivyo sasa hivi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema bei ya umeme iliyopo kwa sasa ni ya muda tu na itashuka baada ya ujenzi wa bomba la gesi kukamilika, ambapo mitambo ya kufua umeme inayotumia mafuta, itatumia gesi na mitambo mipya ya gesi italetwa.
“Serikali inataka umeme mwingi utokane na gesi, jua, upepo na joto ardhi, lakini wapo wanaokataa bomba lisije Dar es Salaam na hao hao wanalalamika umeme bei juu, mtu yeyote anayejua dunia inakwendaje, hawezi kupinga kujengwa bomba la gesi. “Miaka ijayo, chanzo kikubwa cha umeme nchini kitakuwa gesi asilia… nyie mtanitukana, mtanisema sana lakini mimi nitabaki kwenye utaalamu na wala siwezi kuyumba, tatizo la umeme wa Tanzania litatatuliwa na gesi, kila kitu kikikamilika Tanesco na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji), hawawezi kuendelea kuweka bei juu,” alisema Profesa Muhongo.
Katibu Mkuu ashangaa
Akizungumzia mvutano kati ya Tanesco na NDC ulioibuka katika ziara yake inayoendelea mikoani, Maswi alisema hata yeye anashangaa bei hiyo ya NDC, wakati ufuaji wa umeme wa makaa ya mawe ni nafuu kuliko hata huo wa gesi.
Aliagiza mashirika hayo, NDC na Tanesco, yapeleke taarifa zao za hesabu kuhusu bei hizo ili kupata suluhu ya mradi huo wenye uwezo wa kufua megawati 200 na kuacha kugeuka walalamikaji.
Alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa pande zote kuhusu uanzishwaji wa mtambo huo. Alisema anashangazwa namna mashirika hayo, ambayo yote ni ya umma, yanavyoshindwa kuelewana.
“Kitu kinachotuumiza nchi hii ni wote kugeuka kuwa walalamikaji, sasa Tanesco na NDC wote ni mashirika ya umma, inakuwaje mshindwe kuelewana na kukubaliana kuhusu jambo hili muhimu kwa Watanzania ambao wote mnawahudumia?” alihoji.
Chanzo;Habari Leo