Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WADAU
wa zao la korosho wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma wameridhia kuuza
korosho kupitia mfumo wa Stakabadhi ya mazao ghalani kuanzia msimu huu
wa mwaka 2014/2015 zikiwa ni juhudi za kujiletea maendeleo tofauti na
sasa ambapo wakulima hao wamekuwa wakipata hasara na kuwanufaisha
wajanja wachache pindi wanapouza mazao yao kupitia mfumo wa soko holela.
Aidha wadau hao pia
wamewapiga marufuku viongozi wa Vyama vya Msingi vya Wakulima wilayani
humo kuendelea na utaratibu wa kwenda kukopa mikopo katika mabenki na
kwenda kuwalipa fedha hizo kama malipo yao ya awali na kwamba hali hiyo
pekee ndiyo itakayo saidia kuondoa manung'uniko kwa wakulima kulalamikia
kuibiwa fedha zao.
Wajumbe hao waliendelea
kubainisha kuwa fedha hizo za mikopo zimekuwa ni mzigo mkubwa kwa
wakulima kutokana na kutakiwa kulipiwa riba kubwa ambazo hutozwa na
mabenki hayo hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakulima kushindwa kulipwa
malipo yao ya pili na ya tatu baada ya fedha hizo kuishia kulipia riba
za mikopo hiyo katika mabenki ambayo hukopwa na viongozi hao wa vyama
vya ushirika, mambo ambayo yamekuwa yakileta ugumu kwa wakulima kuupenda
mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani.
Tamko hilo lilifikiwa
katika mkutano uliohusisha wadau wa korosho wa kujadili mfumo wa
kisheria wa kuuza mazao yao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ya mazao
ghalani.
Aidha katika
kuhakikisha kuwa mfumo wa ununuzi wa mazao hayo kwa wakulima
unafanikiwa, wakulima hao walikubali kutekeleza makubaliano ya kukusanya
mazao yao katika maghala yaliyopo katika maeneo yao na kusubiri
wanunuzi waende kununua hukohuko na kugawiwa fedha zao kulingana na
idadi ya kilo alizozikabidhi.
Awali akitoa mada ya
dhana ya bei dira na utekelezaji wake Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho
Tanzania, Bw.Mfaume Juma alisema kuwa mfumo huo ulianza kuhamasishwa
msimu wa mavuno na mauzo ya korosho mwaka 2013/2014 na kuanza kutumika
katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.
Alisema kuwa baadaye
wilayani Tunduru mkoani Ruvuma msimu wa mwaka 2007/2008 na kwamba kabla
ya hapo wanunuzi walikuwa wakinunua kupitia mfumo wa soko holela lakini
wakiwa wananunua kupitia bei dira ambayo ilikuwa ikipangwa na Bodi ya
Korosho Tanzania.
Bw.Juma aliendelea
kufafanua kuwa pamoja na bodi hiyo kujipanga kusimamia utaratibu huo kwa
uwazi kwa kuwashirikisha wawakilishi wa wakulima wakati wa kuuza
korosho zao pia wameandaa mkakati maalumu na mazingira ya kusimamia
uuzwaji wa korosho za Tunduru ikiwezekana hata kuhakikisha korosho hizo
zinauzwa kwa utaratibu wa malipwani.
Alisema kuwa kwa tani 1
huuzwa hadi kwa dola za Marekani 1400, sawa na sh.2,240,000 tani moja
sawa na kila kilo moja itauzwa kwa bei ya sh. 2,240 zikiwa ni juhudi za
kumuondoa mtu wa kati yani Madalali na viongozi wa vyama vya ushirika
mabavyo vimekuwa vikijinufaisha kupitia mgongo wa wakulima, Bw. Juma
Aliendelea kueleza kuwa Kupitia mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani
kazi za vyama vya msingi ni kukusanya mazao na kuyatunza katika maghala
ya chama,kupanga madaraja,kufungasha katika magunia yenye uzito sahihi,
kusafirisha korosho hadi sokoni, kusimamia mauzo wakati wa minada na
kuwagawia wakulima fedha zao.
Alisema kwamba mtindo
wa kukopa fedha katika mabenki haupo katika utekelezaji wa mfumo huo na
kwamba viongozi wabadhirifu katika vyama vyao wawatoe wakati wa uchaguzi
na kuwaweka madarakani viongozi waadilifu.
Akifafanua matumizi ya
mfumo huo Mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Tanzania,
Bw.Athuman Nkinde alisema kuwa pamoja na mkakati huo wa kuwadhibiti
walanguzi hao mfuko huo umetenga sh. bilioni 6 kwa ajili ya kujenga
viwanda vitatu katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Mtwara na Wilaya
ya Mkuranga mkoani Pwani.
Alisema katika mpango
huo kila kiwanda kimetengewa sh. bilioni 2 zikiwa ni juhudi za serikali
kukuza soko la ndani ili kuwainua wakulima na kuwawezesha kuuza mazao
yaliyosindikwa na kwamba, mkutano huo umelenga kuwajengea uwezo na
kufungua upeo kwa wakulima na kuwawezesha wakulima kupata faida na
kuiwezesha halmashauri kupata ushuru mkubwa na kuifanya halmashauri yao
kujitosheleza katika bajeti zake za matumizi ya ndani
Chanzo:MMjira
0 comments:
Post a Comment