Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Elimu ya ujasiriamali katika nchi yetu haina ‘umri’ mkubwa kama
zilivyo taaluma nyingine zikiwamo lugha, historia, siasa na sayansi. Hii
ni kutokana na historia ya nchi yetu hasa baada ya kupata uhuru, kwamba
tuliamua kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea kupitia Azimio la
Arusha.
Siasa ya ujamaa na kujitegemea haikushadidia
ujasiriamali kwa vile ulifananishwa na ubepari ambao ulichukuliwa kama
unyama. Wale wote waliokuwa wanajihusisha na shughuli za kijasiriamali
hasa biashara katika kipindi hicho walionekana kama ‘wanyama’ au watu
ambao walikuwa wamechepuka kutoka katika njia kuu ambayo ilikuwa
inaaminiwa na jamii kubwa wakati huo.
Wafanyakazi serikalini walikuwa hawaruhusiwi
kujihusisha na biashara na kwamba shughuli za ujasiriamali zilionekana
kufanywa na watu ambao hawakuwa na elimu ya kutosha kupata ajira, na
wageni hasa kutoka Bara la Asia kama vile Wahindi.
Hata hivyo, kutokana na hali halisi ya maisha
katika nchi yetu na duniani kwa jumla, kwenye miaka ya katikati ya 2000,
taifa lilianza utaratibu wa kuingiza elimu ya ujasiriamali katika elimu
ingawa haikuwekewa kipaumbele sana. Kwa sasa elimu ya ujasiriamali
imekuwa kama wimbo wa taifa, siyo shuleni na vyuoni bali hata katika
sekta ambazo si rasmi kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia matangazo
mbalimbali juu ya kuendesha elimu ya ujasirimali katika makundi
mbalimbali ya jamii yetu.
Kutokana na wanajamii na taifa kwa jumla kuanza
kuona elimu ya ujasiriamali kama mwarobaini wa matatizo yanayowakabili
kama vile ajira na umaskini, lengo la makala haya ni kuelezea umuhimu wa
elimu ya ujasiriamali katika shule na vyuo kama njia mojawapo yenye
kuonyesha jinsi elimu ya ujasiriamali inavyoweza kuisaidia jamii na
taifa katika kuleta maendeleo.
Ujasiriamali ni mchakato au hali waliyonayo baadhi
ya watu ya kutaka mafanikio yanayoshadadiwa na moyo wa ushindani,
kujiamini, uwezo binafsi wa kukabiliana na kutatua changamoto zilizopo
ikiwa ni pamoja na uthubutu wa kukabiliana na changamoto ambazo wakati
mwingine huweza kuathiri maisha yao katika kipindi cha mpito.
Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kama
ujasiriamali hufundishwa au mtu huzaliwa nao ingawa si lengo la makala
haya kujikita katika mjadala huu, kwa kuwa tunaelewa nguvu iliyonayo
elimu katika kuyatengeneza maisha ya mwanadamu.
Elimu ya ujasiriamali ni muhimu sana katika ngazi zote za elimu kwa ajili ya kuwatayarisha vijana juu ya maisha yao ya baadaye.
Tunaamini kuwa vijana wana maono na matamanio yao
katika maisha kama walivyo watu wazima ingawa watu hawa wawili wanaweza
kutofautiana hapa na pale kutokana na sababu za umri, mazingira, wakati
na uzoefu katika maisha.
Elimu ya ujasiriamali katika shule na vyuo hujenga
msingi mzuri wa kujiamini miongoni mwa vijana na hivyo kuwafanya
wayakabili maisha bila woga, jambo ambalo litawafanya kufanya kazi zao
wanazozipenda kwa umahiri, weledi na kujiamini zaidi.
Badala ya kuwafanya vijana wajiamini katika yale
wanayoyafanya na wanayoyapenda kulingana na uwezo na vipawa vyao,
tumekuwa tukiwatia hofu ya maisha kwa njia ya mitihani kiasi hata cha
kutoa mikopo ya elimu kwa kuzingatia madaraja ya ufaulu, jambo ambalo
linajenga taifa la watu wasiojiamini katika kazi ambazo si lazima ziwe
za kukaa ofisini.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment