Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANAFUNZI wa darasa la awali shule ya Msingi Nakayaya wilayani hapa
mkoani Ruvuma, wanasomea chini ya mti kutokana na darasa hilo
kuendeshwa bila ya kuwa na chumba maalum.
Hali hiyo imebainika, baada ya mwandishi wa habari hizi kuitembelea
shule hiyo hivi karibuni na kuwakuta wanafunzi wakiendelea na masomo
hayo nje chini ya mti ulio na kivuli cha kuwahifadhi wakati wa jua
kali.
Akizungumza shuleni hapo, Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Christina
Mhowera, alisema watoto hao wamelazimika kusomea nje baada ya huduma ya
elimu hiyo kuanzishwa shuleni hapo bila ya kuwa na jengo maalum kwa
wanafunzi wa awali.
Alisema awali wanafunzi hao walikuwa wakisomea kwenye gofu (jengo
mbovu), lililokuwa jirani na shule, lakini walilazimika kuondolewa baada
ya jengo hilo kutwaliwa kwa matumizi mengine.
Aliongeza kuwa baada ya hapo walihamishiwa kwenye nyumba ya mwalimu
kabla ya kukamilika, lakini waliondolewa tena na kuanza kusomea nje
chini ya mti hadi sasa.
Alisema darasa hilo lenye wanafunzi 92, linaendeshwa bila ya kuwa na
chumba cha darasa maalum wala madawati kutokana na shule hiyo kukabiliwa
na uhaba wa vyumba vya madarasa hadi hapo watakapopata darasa maalum
kwa ajili ya wanafunzi hao.
Kwa upande wake mwalimu wa darasa hilo, Teckla Milanzi, alisema mbali
na darasa hilo kutokuwa na chumba, linakabiliwa na changamoto lukuki
ikiwemo ya uhaba wa vitendea kazi kama vitabu na vyenzo zingine za
kufundishia na hakuna bajeti yoyote inayotumwa kuliwezesha darasa hilo.
Aidha, uchunguzi uliofanywa katika shule nyingine tatu za Wilaya ya
Tunduru, yaani Shule ya Msingi Nanjoka, Majengo na Shule ya Msingi
Tunduru Mchanganyiko kuangalia mazingira ya utoaji elimu ya awali
katika shule hizo umebainisha kukabiliwa na changamoto nyingi hali
ambayo inahatarisha msingi wa elimu kwa wanafunzi.
Chanzo Tanzania Daima