Home » » DCI: BOMU LILILOJERUHI POLISI NI LA KIENYEJI

DCI: BOMU LILILOJERUHI POLISI NI LA KIENYEJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu, (pichani) amesema bomu waliorushiwa polisi wanne limetengenezwa kienyeji.
 
Hata hivyo, amesema bomu hilo limetengenezwa kitaalamu zaidi kuliko mabomu mengine yaliyotengenezwa kienyeji na kulipuliwa katika baadhi ya maeneo nchini, lakini akasema hadi sasa hakuna anayeshikiliwa kwa tuhuma hizo.
 
Alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya polisi Mkoa wa Ruvuma.
 
Mngulu alisema bomu hilo ni la aina yake,  ingawa kwa sasa hawezi kuelezea zaidi kwa sababu akifanya hivyo atatoa  nafasi kwa watu wengine kutengeneza mabomu hayo na kuendelea kuhatarisha amani nchini.
 
“Nimekagua matukio mengi hapa Tanzania yanayohusiana na milipuko ya mabomu. Lakini tukio la Songea, bomu hili ni la aina yake. Kwani lina ‘cover’ ya bati gumu, ambalo linaonyesha limetengenezwa kiufundi zaidi,” alisema Mngulu.
 
Alisema katika tukio hilo, askari watatu walijeruhiwa; wawili kati yao bado hali zao ni mbaya na wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa huo.
 
Aliwataja askari hao kuwa G7351 PC Ramadhan, WP 10399 PC Felista na H 3484 PC Respicus, ambaye ametibiwa na kuruhusiwa.
 
Alisema uchunguzi wa kuwabaini waliohusika na tukio hilo unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama.
 
Wakati huo huo, majeruhi wawili waliojeruhiwa katika tukio hilo, ambao wamelazwa katika hospitali hiyo walisema hali zao zinaendelea vizuri na tayari wameshafanyiwa upasuaji.
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa huo, Dk. Benedicto Ngaiza, alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa