Home » » WANAFUNZI TUNDURU WASOMEA CHINI YA MTI

WANAFUNZI TUNDURU WASOMEA CHINI YA MTI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WANAFUNZI wa darasa la awali shule ya Msingi Nakayaya wilayani hapa mkoani Ruvuma, wanasomea chini ya mti kutokana na darasa hilo kuendeshwa bila ya kuwa na chumba maalum.
Hali hiyo imebainika, baada ya mwandishi wa habari hizi kuitembelea shule hiyo hivi karibuni na kuwakuta wanafunzi wakiendelea na masomo hayo nje chini ya mti ulio na kivuli cha kuwahifadhi wakati wa jua kali.
Akizungumza shuleni hapo, Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Christina Mhowera, alisema watoto hao wamelazimika kusomea nje baada ya huduma ya elimu hiyo kuanzishwa shuleni hapo bila ya kuwa na jengo maalum kwa wanafunzi wa awali.
Alisema awali wanafunzi hao walikuwa wakisomea kwenye gofu (jengo mbovu), lililokuwa jirani na shule, lakini walilazimika kuondolewa baada ya jengo hilo kutwaliwa kwa matumizi mengine.
Aliongeza kuwa baada ya hapo walihamishiwa kwenye nyumba ya mwalimu kabla ya kukamilika, lakini waliondolewa tena na kuanza kusomea nje chini ya mti hadi sasa.
Alisema darasa hilo lenye wanafunzi 92, linaendeshwa bila ya kuwa na chumba cha darasa maalum wala madawati kutokana na shule hiyo kukabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa hadi hapo watakapopata darasa maalum kwa ajili ya wanafunzi hao.
Kwa upande wake mwalimu wa darasa hilo, Teckla Milanzi, alisema mbali na darasa hilo kutokuwa na chumba, linakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ya uhaba wa vitendea kazi kama vitabu na vyenzo zingine za kufundishia na hakuna bajeti yoyote inayotumwa kuliwezesha darasa hilo.
Aidha, uchunguzi uliofanywa katika shule nyingine tatu za Wilaya ya Tunduru, yaani Shule ya Msingi Nanjoka, Majengo na Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko kuangalia mazingira ya utoaji elimu ya awali katika shule hizo umebainisha kukabiliwa na changamoto nyingi hali ambayo inahatarisha msingi wa elimu kwa wanafunzi.
  Chanzo Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa