Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU
wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, amekipongeza chuo kikuu cha sayansi
ya kompyuta cha Mtakatifu Joseph Tawi la Songea kwa jitihada zake za
kuendelea kupanua wigo wa kutoa huduma na kukuza elimu ya juu hapa
nchini.
Mwambungu, alitoa pongezi hizo juzi wakati wa mahafali ya tano ya
chuo hicho mjini Songea, yaliyohusisha wahitimu 119 wa shahada na
stashahada.
Alisema kuanzishwa kwa chuo hicho, kumesaidia kulipunguzia taifa
tatizo la ukosefu wa wataalamu wa sayansi hususani katika ukanda wa
kusini na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa kuanzishwa kwa chuo kikuu cha sayansi ya kilimo na
teknolojia katika sekta ya kilimo ni jambo jema kwa ustawi wa nchi huku
akiwataka wahitimu hao kuitumia elimu waliyoipata kwa ajili ya kuleta
mabadiliko katika jamii na taifa kwa ujumla kwa kufanya kazi kwa bidii
na ufanisi.
Alisema kuwa katika maisha ya hivi sasa, hakuna njia fupi ya kufikia
mafanikio katika maisha zaidi ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa na
kudai kwamba, changamoto zilizopo katika chuo hicho zigeuzwe kuwa fursa
pekee ya kujipanua na kutoa elimu bora huku akiwataka kuboresha
mawasiliano ili kukuza wigo wa utatuzi wa changamoto mbalimbali.
Aidha, amewaomba wanafunzi wa chuo hicho, kuombea amani hususani
katika kipindi hiki kigumu ambacho taifa linaingia kwenye mchakato wa
uundwaji wa katiba mpya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya chuo hicho, Askofu
John Ndimbo, alisema kuwa anajisikia fahari kuona chuo hicho kinazalisha
wataalamu wengi wa sayansi ukanda wa kusini huku akidai kuwa elimu ni
tunu kubwa ya maendeleo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment