Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Mgomo huo ulioanzia kwa wafanyabiashara wa maduka Kariakoo, jijini
Dar es Salaam kuanzia juzi, kupinga Mwenyekiti wao Johnson Minja,
kukamatwa na polisi, sasa umesambaa hadi miji ya Mwanza, Iringa, Songea
na Dodoma.
APANDISHWA KIZIMBANI
Minja (34), jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa
Dodoma kwa makosa mawili likiwamo la kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa
kutumia EFDs na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Rebbeka
Mbiru.
Wakili wa Serikali, Godfrey Wambari, alidai kuwa Septemba 6, mwaka
2014, katika ukumbi wa Chuo Cha Mipango Dodoma alitenda kosa la
kushawishi wafanyabiashara kutenda kosa la jinai kwamba wasilipe kodi.
Katika shitaka la pili, siku na mahali pa tukio la kwanza mshtakiwa
anadaiwa kuzuia ukusanyaji wa Kodi kwa kutumia mashine za EFD.
Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi la dhamana.
Mshtakiwa alikana mashitaka yake.
Hakimu Mbiru alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na
wadhamini wawili akiwemo mtumishi wa serikali mmoja, watakaosaini hati
ya dhamana ya Sh. milioni nne.
Wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga, alidai kuwa mshtakiwa ni
mfanyabiashara maarufu nchini na kwamba anaaminika hawezi kutoroka
mahakama ipunguze masharti ya dhamana.
Hata hivyo, mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa Februari 11, mwaka huu.
IRINGA
Katika hatua nyingine, wakazi wa mkoa wa Iringa jana walishindwa
kupata huduma muhimu kutokana na wafanyabiashara wenye maduka kuungana
na wafanyabiashara wa mikoa mingine katika mgomo wa kufungua maduka
baada ya Minja kukamatwa.
Mgomo huo umedumu kwa siku nzima na kusababisha wakazi wa manispaa ya hiyo kukosa huduma muhimu za kijamii.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoa wa Iringa, Odilo Nambanga,
alisema kwamba mgomo huo wameungana na wenzao nchi nzima kufunga
biashara zao mpaka matatizo yao ya msingi yatakapotatuliwa.
Nambanga alisema kauli mbiu yao ni mwenyekiti kwanza na masuala
mengine yatafuata ikiwa ni pamoja na kuungana kwa umoja wao na kutatua
matatizo yao.
Naye mfanyabiashara Sylivester Mmasi, alisema hawawezi kufungua
biashara hata zipite wiki mbili hadi watakapopata tamko la kukamatwa
mwenyekiti wao.
Alisema umesababisha wanafunzi kukosa huduma za vifaa vya shule
hasa wale wanaokwenda shule zilizopo nje ya Manispaa ya Iringa na
kulazimika kuhudhuria masomo.
SONGEA
Wafanyabiashara wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamelazimika
kufunga maduka yao kupinga kitendo cha kukamatwa kwa Minja na kwamba
mgomo huo utadumu mpaka hapo watakapopata uhakika wa usalama wake na si
vinginevyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo
Tawi la Ruvuma, Isaya Mwilamba, alisema wamefunga maduka kusubiri hatma
ya Minja.
Mwilamba alisema kuwa wafanyabiashara wote nchini wanasitisha shughuli zote hadi watakapojua hatma ya kiongozi na mtetezi wao.
“Tunaitaka serikali kuzingatia nia njema ya kuundwa kwa kamati
hiyo ya majadiliano na itoe taarifa stahiki kwa wafanyabiashara kwani
tunapata wasiwasi kuwa kukamatwa kwake kiongozi wetu kunatokana na
juhudi za wafanyabiashara kupinga ongezeko la kodi kwa asilimia 100 na
matumizi ya mashine za EFD,” alisema Mwilamba.
Alisema serikali inapaswa kutumia njia za kidemokrasia kumaliza
changamoto zake na siyo kutumia nguvu kuzima madai ya msingi ya
wafanyabiashara hivyo ni vyema ikasikiliza kilio cha wafanyabiashara
ambao kimsingi ndio wachangiaji wakubwa wa kodi za serikali.
MWANZA
Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka jijini Mwanza wa mitaa ya
Lumumba, Pamba na Rwegosore, wamefunga maduka kupinga kukamatwa kwa
Minja.
Akizungumza na NIPASHE jana, Michael Massanja, mfanyabiashara wa
jijini hapa, alisema wamesikitishwa kukamatwa kwa kiongozi wao na
wameamua kuungana kwa kufunga maduka kama walivyofanya wenzao wa Dar es
Salaam.
Massanja alisema kukamatwa kwa kiongozi wao sio suluhisho la
kuwafanya wafanyabiashara kutumia mashine hizo badala yake serikali
izungumze na wafanyabiashara husika ili kutatua mgogoro huo.
”Hatutafungua maduka yetu hadi pale tutakapopata taarifa ya
Mwenyekiti wetu mahali alipo ingawa tumesikia yupo Dodoma, lakini
hatuna uhakika na hilo,” alisema Massanja.
Naye Zuberi Issa, mfanyabiashara wa maduka mtaa wa Pamba, alisema
kufuatia kukamatwa kwa Mwenyekiti wao Minja, kumesababisha kutofanyika
biashara yoyote kwa siku nzima ya jana, huku akisisitiza maduka
kutofunguliwa.
”Tukio hili limechangia tusifanye biashara toka asubuhi kwa kuwa
tumesisitiziwa na wenzetu kuungana ili tujue hatma ya kiongozi wetu yupo
wapi na atapatikana lini,” alisema Issa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Christopher Wambura, hakupatikana kuzungumzia mgomo huo.
KARIAKOO BADO
Wafanyabiashara wa Soko Kuu Kariakoo Mtaa wa Kongo, jijini Dar es
Salaam, wameendelea kugoma kufunga maduka yao kushinikiza kuachiwa kwa
Minja.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE ulibaini kuwa karibu mitaa yote
inayopatikana Karikoo, maduka mengi yalikuwa yamefungwa jana huku
machache yakiwa yamefunguliwa.
Katika Mtaa wa Kongo, wafanyabiashara walikutwa wakiwa nje, hali
iliyowawia vigumu wateja kupata mahitaji kama vile bidhaa kadhaa.
NIPASHE lilibaini baadhi ya maduka ya simu machache yaliyokuwa
yamefunguliwa milango nusu hali iliyowafanya wateja kununua bidhaa za
hizo kwa taabu.
Walipohojiwa wafanyabiashara hao kwa masharti ya kutotajwa majina
yao, walisema wataendelea kugoma kufungua maduka yao hadi watakapojua
sababu ya kukamatwa kwa kiongozi wao.
“ Hatufungui maduka yetu mpaka tujue sababu ya kukamatwa kwa Minja,
tutayafungua endapo tutaelezwa sababu za kukamatwa kwake,” alisema
mmoja wa wafanyabiashara hao.
Minja alikamatwa juzi na Jeshi la Polisi na kusafirishwa kupelekwa
mjini Dodoma kujibu mashitaka ya kuhamasisha wafanyabiashara wa mkoa
huo wagome kufungua maduka kupinga matumizi ya EFDs.
Imeandikwa na Daniel Mkate, Mwanza, Peter Mkwavila, Dodoma; Gideon
Mwakanosya, Songea; George Tarimo, Iringa na Hussein Ndubikole, Dar.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.