Wafanyabiashara wilayani hapa, wametishia
kutomchagua Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo kwenye
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa kile walichodai ameshindwa kuwatetea
bungeni na badala yake ameunga mkono ongezeko la kodi la asilimia 100.
Wakizungumza wakati wa kikao cha wafanyabiashara
na maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mbinga, mmoja wa
wafanyabiashara hao, Benedict Lwena alisema wameumizwa na mbunge wao
kushindwa kuwatetea kuhusu suala hilo. “Hatukumtuma bungeni kwenda
kulala, bali kutuwakilisha, kutokana na kutugeuka nasi tumejipanga
kumwangusha kwani hatuwezi kuwa na mbunge asiyejali kero za wananchi
wake,” alisema Lwena.
Mfanyabiashara mwingine, Ally Mbunda alisema kwa
muda mrefu wamekuwa wakiomba kukutana na mbunge huyo ili waweze
kuzungumzia kero zinazowasumbua lakini amekuwa akisema amebanwa na
majukumu mengine.
Hata hivyo, akizungumza kwa simu jana, mbunge huyo
alikiri kusikia malalamiko hayo lakini akashangazwa na taarifa hizo
akisema, tangu kikao kilipomalizika hakuna viongozi wala wafanyabiashara
waliomfuata kumweleza hatua zilizofikiwa juu ya kikao hicho.
Alisema anashangaa kwa nini malalamiko hayo
yanatokea kipindi hiki cha kampeni, “Siyo wafanyabiashara peke yao
wanaopiga kura, kwanza sheria inapitishwa na wabunge wote na inatumika
nchi nzima hivyo sioni haja ya wao kuniadhibu.”
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment