Home » » JANUARY MAKAMBA: NCHI IKO NJIAPANDA

JANUARY MAKAMBA: NCHI IKO NJIAPANDA

Mbunge wa Bumbuli na pia ni Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba.
 
Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijiandaa kupanga ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wake ndani ya dola katika vikao vijavyo, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, ametahadharisha kwamba kama watapatikana viongozi ambao wamekuzwa na kuulea mfumo wa sasa uliopo, nchi isitegemee kupata mabadiliko yeyote ya maendeleo.
Makamba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, ni miongoni mwa makada wa CCM ambao walishatangaza nia yao ya kutaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Makamba akihojiwa jana katika radio moja alisema hivi sasa nchi  ipo njia panda na mwaka 2015 ndio utakaoamua kati ya njia moja nchi kupaa kwa kuendelea kiuchumi au kuporomoka.

Alisema dalili za nchi kuwa njia panda ambazo zinaonekana ni pamoja na tatizo la vijana wengi kukosa ajira, mitafaruku, ukali wa maisha kuzidi kuongezeka miongoni mwa jamii na watu kuanza kuongea lugha za utengano.

Alisema kati ya njia hizo kuna mambo ambayo yanaweza kufanyika kuipaisha nchi au kuiporomosha na kwamba aina ya uongozi utakaopatikanani mwaka huu ndio utaamua hatma ya nchi.

“Naamini kwamba kwa zama hizi tulizokuwa sasa ambako kunahitaji mabadiliko makubwa sana katika mfumo wa siasa, mfumo wa utawala ,mfumo wa uongozi na mfumo wa uchumi na lazima kupata viongozi ambao hawakuwa sehemu ya kuuweka mfumo uliopo sasa,” alisema.

Aliongeza kuwa kama watapatikana  viongozi ambao wamekuzwa na kuulea mfumo uliopo sasa tusitegemea tutapata mabadiliko yeyote.

“Tunaamini kuwa vijana wameandaliwa vizuri, tukipata viongozi wa zama hizi ambao wamelelewa kiuongozi na wanaelewa uongozi na thamani ya zama tulizonazo sasa na wakaaminiwa nchi yetu itapaa kimaendeleo,” alisema.

Makamba alisema malalamiko ya wananchi yaliyopo yapo chini ya uwezo wetu kutegemeana aina ya kiongozi ambaye atapatikana ambaye atajali maslahi ya wananchi badala ya maslahi yake binafsi.

Makamba alisema Watanzania  wanapaswa kuondoa dhana kwamba nafasi ya juu ya urais ni lazima mtu uwe na uzoefu, na kwamba hadi sasa wenye uzoefu na suala la urais ni Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na  Rais Jakaya Kikwete tu.

“Ukiacha hao marais wastaafu, hakuna mtu mwingine yeyote ambaye anaweza kusema kazi aliyoishika imemuandaa kuwa kiongozi mkubwa wa nchi kwa maana ya rais,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa