Mwenyekiti wa Halimashauri ya Musoma vijijini ambae ni Diwani wa Kata ya
Nyankanga Magina Magesa, akikagua ujenzi wa maabara katika shule ya
sekondari Bisumwa, juzi
Desemba 9 mwaka jana ndiyo ulikuwa mwisho wa utekelezaji wa
agizo la Rais Jakaya Kikwete kuhusu ujenzi wa maabara katika shule za
sekondari za Serikali nchi nzima.
Akiwa katika mikutano ya hadhara katika Wilaya za
Lushoto na Kilindi mkoani Tanga Julai, Rais Kikwete aliagiza ifikapo
Novemba 30 aone vyumba vya maabara vimekamilika. Kutoka Novemba 30 muda
ukaongezwa hadi Desemba 9.
Utekelezaji wa ujenzi
Tayari kuna mikoa iliyotekeleza ujenzi huo kwa asilimia zaidi ya 90, mingine asilimia 50 na hata 30 kwa baadhi ya mikoa.
Mikoa iliyotekeleza agizo hilo na asilimia katika
mabano ni Dar es Salaam (100), Mbeya (95.45), Njombe (95), Kigoma chini
ya asilimia 40, Morogoro (60) na Ruvuma zaidi ya asilimia 92.
Katika maeneo mengi utekelezaji wa ujenzi huu
umekumbwa na kadhia nyingi zikiwamo walimu kukatwa fedha kwa nguvu,
wananchi kutishwa na hata baadhi ya watendaji kuvuliwa nyadhifa zao na
wengine kukumbana na kipigo.
Mfano barua ya Septemba 15, mwaka 2014 kutoka
Halmashauri ya Kongwa mjini Dodoma kwenda kwa waratibu wa elimu wa kata,
iliwataka watendaji hao kuhakikisha wanakusanya fedha za michango
kutoka kwa walimu.
Barua hiyo ilibainisha viwango vilivyotakiwa
kutolewa ku ni Sh60,000 (waratibu elimu kata), Sh60,000 (walimu ngazi ya
mshahara TGTS F-G), Sh30,000 (ngazi ya mshahara TGTS D-E) na Sh20,000
(TGTS B-C).
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet),
Cathleen Sekwao, anasema huwezi kuwaeleza wananchi wachangie maabara
wakati wanaona fedha zipo ila wanafaidi wachache.
“Watu wanachota pesa wanakula halafu unapofika
wakati wa uboreshaji wa elimu wananchi wachangie, kweli hiyo Sh1.6
trilioni si ingetosha kujenga hizo maabara lakini je, waliokula
wamechukuliwa hatua gani,” anasema na kuongeza:
“Fedha zipo na wananchi, walimu wanalia
kuchangishwa, mifumo ya uongozi ni mibovu kwani ingekuwa imara
rasilimali tulizonazo zinazopotea kwa wajanja kujinufaisha wao ndiyo
inatufikisha hapa.’’
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba katika
mahojiano na gazeti hili Oktoba mwaka jana, alikaririwa akisema Serikali
imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh1.6 trilioni kwa mishahara hewa nchini
kila mwaka.
“Ukisoma taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), utagundua zaidi ya Sh1.6 trilioni zinapotea kutokana na
mishahara hewa, fedha inayotosha bajeti ya wizara,” alieleza Nchemba.
Kwa wadau wengi wa elimu, fedha anazotaja Mwigulu
na nyinginezo zingeweza kutumika katika vipaumbele ikiwamo ujenzi huo wa
maabara ambao sasa unaendeshwa kwa nguvu ya wananchi kupitia maagizo ya
viongozi wa Serikali.
Fedha nyingine zinazoweza kutumika katika shughuli
za maendeleo ni pamoja na zile zinazosamehewa katika misamaha ya kodi.
Kwa mfano Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/14, inaonyesha kwa mwaka huo
zaidi ya Sh1.6 trilioni zilipotea kupitia misamaha ya kodi.
Walimu wa Sayansi
Wakati hamasa ya sasa ikiwa ni ujenzi wa maabara,
baadhi ya watu wanauliza kuna mikakati gani ya kuwapata wataalamu wa
maabara hizo na hata vifaa husika?
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), Ezekiel Oluoch anasema katika masomo ya Fizikia, Kemia na
Baiolojia kuna upungufu wa asilimia 50 ya walimu.
Anasema jumla ya shule za sekondari za kata nchi
nzima ziko 3,500 na zote hazina maabara na kwa maabara za masomo ya
sayansi inahitaji wataalamu wa maabara mmoja, hivyo kwa zote
watahitajika watatu.
“Kwa idadi hiyo jumla ya wataalamu wa maabara
12,000 watahitajika…maabara zinatakiwa kuwa zimekamilika Novemba 30
mwaka huu je, walimu wa kuziendesha wanatoka wapi au tutakuwa na majengo
tu ya maabara?’’ anasema.
Anaongeza: “Nilichokuwa nakiona mimi wakati
Serikali inapanga kujenga maabara, ingepanga pia kuandaa walimu wa
kutosha na wataalamu wa maabara hizo lakini sasa tujiandae kuwa na
majengo ya maabara na si maabara kama wanavyodai.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Romanus
Dimoso anasema changamoto anayoitazama katika ujenzi wa maabara ni ndogo
kuliko ujenzi huo utakapokamilika.
“Sitoshangaa kama nikiona au kusikia majengo hayo
yamebadilishwa matumizi kwani gharama za ujenzi kama tunahangaika hivi
itakuaje gharamza za vifaa vya kufundishia na kujifunza ambavyo ni kubwa
kuliko ujenzi wenyewe?” anahoji.
“Walimu bado ni tatizo na hata waliopo hawakusoma
kwa vitendo na walijikita kinadharia zaidi sasa unapotaka watumike
katika maabara sijui itakuaje,” anaongeza kusema.
Chanzo:Mwananchi
Kauli ya Wizara
Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, (Tamisemi) anayeshughulikia elimu, Kassimu Majaliwa anasema
maabara zitakapokamilika watawasiliana na ofisi ya utumishi ili
kuhakikisha wataalamu wanaajiriwa.
“Mbali na walimu pia tutafanya juhudi za kuwaajiri
wataalamu wa maabara hizo ambao watakuwepo katika maabara hizo ili
kurahisisha zoezi zima la utoaji wa huduma kwa wanafunzi,” anasema.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment