Home » » MGOMO WENYE MADUKA WAZIDI KUSAMBAA

MGOMO WENYE MADUKA WAZIDI KUSAMBAA

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum.
Mgomo wa wafanyabiashara wa mduka umesambaa mikoa kadhaa nchini kupinga matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs).
 
Mgomo huo ulioanzia kwa wafanyabiashara wa maduka Kariakoo, jijini Dar es Salaam kuanzia juzi, kupinga Mwenyekiti wao Johnson Minja, kukamatwa na polisi, sasa umesambaa hadi miji ya Mwanza, Iringa, Songea na Dodoma.
 
APANDISHWA KIZIMBANI
Minja (34), jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa makosa mawili likiwamo la kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa kutumia EFDs na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Rebbeka Mbiru.
 
Wakili wa Serikali, Godfrey Wambari, alidai kuwa Septemba 6, mwaka 2014, katika ukumbi wa Chuo Cha Mipango Dodoma alitenda kosa la kushawishi wafanyabiashara kutenda kosa la jinai kwamba wasilipe kodi.
 
Katika shitaka la pili, siku na mahali pa tukio la kwanza mshtakiwa anadaiwa kuzuia ukusanyaji wa Kodi kwa kutumia mashine za EFD.
Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi la dhamana.
 
Mshtakiwa alikana mashitaka yake.
 
Hakimu Mbiru alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili akiwemo mtumishi wa serikali mmoja, watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni nne.
 
Wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga, alidai kuwa mshtakiwa ni mfanyabiashara maarufu nchini na kwamba anaaminika hawezi kutoroka mahakama ipunguze masharti ya dhamana.
 
Hata hivyo, mshtakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo itatajwa Februari 11, mwaka huu.
 
IRINGA
Katika hatua nyingine, wakazi wa mkoa wa Iringa jana walishindwa kupata huduma  muhimu kutokana na wafanyabiashara wenye maduka kuungana na wafanyabiashara wa mikoa mingine katika mgomo wa kufungua maduka baada ya Minja kukamatwa.
 
Mgomo huo umedumu kwa siku nzima na kusababisha wakazi wa manispaa ya hiyo kukosa huduma muhimu za kijamii.
 
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoa wa Iringa, Odilo Nambanga, alisema kwamba mgomo huo wameungana na wenzao nchi nzima kufunga biashara zao mpaka matatizo yao ya msingi yatakapotatuliwa.
 
Nambanga alisema kauli mbiu yao ni mwenyekiti kwanza na masuala mengine yatafuata ikiwa ni pamoja na kuungana kwa umoja wao na kutatua matatizo yao.
 
Naye mfanyabiashara Sylivester Mmasi, alisema hawawezi kufungua biashara hata zipite wiki mbili hadi watakapopata tamko la kukamatwa mwenyekiti wao.
 
Alisema umesababisha wanafunzi kukosa huduma za vifaa vya shule hasa wale wanaokwenda shule zilizopo nje ya Manispaa ya Iringa na kulazimika kuhudhuria masomo.
 
SONGEA
Wafanyabiashara wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamelazimika kufunga maduka yao kupinga kitendo cha kukamatwa kwa Minja na kwamba mgomo huo utadumu mpaka hapo watakapopata uhakika wa usalama wake na si vinginevyo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Tawi la Ruvuma, Isaya Mwilamba, alisema wamefunga maduka kusubiri hatma ya Minja.
 
Mwilamba alisema kuwa wafanyabiashara wote nchini wanasitisha shughuli zote hadi watakapojua hatma ya kiongozi na mtetezi wao.
 
 “Tunaitaka serikali kuzingatia nia njema ya kuundwa kwa kamati hiyo ya majadiliano na itoe taarifa stahiki kwa wafanyabiashara kwani tunapata wasiwasi kuwa kukamatwa kwake kiongozi wetu kunatokana na juhudi za wafanyabiashara kupinga ongezeko la kodi kwa asilimia 100 na matumizi ya mashine za EFD,” alisema Mwilamba.
 
Alisema serikali inapaswa kutumia njia za kidemokrasia kumaliza changamoto zake na siyo kutumia nguvu kuzima madai ya msingi ya wafanyabiashara hivyo ni vyema ikasikiliza kilio cha wafanyabiashara ambao kimsingi ndio wachangiaji wakubwa wa kodi za serikali.
 
MWANZA
 Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka jijini Mwanza wa mitaa ya Lumumba, Pamba na Rwegosore, wamefunga maduka kupinga kukamatwa kwa Minja.
 
Akizungumza na NIPASHE jana, Michael Massanja, mfanyabiashara wa jijini hapa, alisema wamesikitishwa kukamatwa kwa kiongozi wao na wameamua kuungana kwa kufunga maduka kama walivyofanya wenzao wa Dar es Salaam.
 
Massanja alisema kukamatwa kwa kiongozi wao sio suluhisho la kuwafanya wafanyabiashara kutumia mashine hizo badala yake serikali izungumze na wafanyabiashara  husika ili kutatua mgogoro huo.
 
”Hatutafungua maduka yetu hadi pale tutakapopata taarifa ya Mwenyekiti wetu mahali alipo ingawa tumesikia yupo Dodoma,  lakini hatuna uhakika na hilo,” alisema Massanja.
 
Naye Zuberi Issa, mfanyabiashara wa maduka mtaa wa Pamba, alisema kufuatia kukamatwa kwa Mwenyekiti wao Minja, kumesababisha kutofanyika biashara yoyote kwa siku nzima ya jana, huku akisisitiza maduka kutofunguliwa.
 
”Tukio hili limechangia tusifanye biashara toka asubuhi kwa kuwa tumesisitiziwa na wenzetu kuungana ili tujue hatma ya kiongozi wetu yupo wapi na atapatikana lini,” alisema Issa.
 
Hata hivyo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Christopher Wambura, hakupatikana kuzungumzia mgomo huo.
 
KARIAKOO BADO
Wafanyabiashara wa Soko Kuu Kariakoo Mtaa wa Kongo, jijini Dar es Salaam, wameendelea kugoma kufunga maduka yao kushinikiza kuachiwa kwa Minja.
 
Uchunguzi  uliofanywa na NIPASHE ulibaini kuwa karibu mitaa yote inayopatikana Karikoo, maduka mengi yalikuwa yamefungwa jana huku machache yakiwa yamefunguliwa.
 
Katika Mtaa wa Kongo, wafanyabiashara walikutwa wakiwa nje, hali iliyowawia vigumu wateja kupata mahitaji kama vile bidhaa kadhaa.
 
NIPASHE lilibaini baadhi ya maduka ya simu machache yaliyokuwa yamefunguliwa milango nusu hali iliyowafanya wateja kununua bidhaa za hizo kwa taabu.
 
Walipohojiwa wafanyabiashara hao kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema wataendelea kugoma kufungua maduka yao hadi watakapojua sababu ya kukamatwa kwa kiongozi wao.
 
“ Hatufungui maduka yetu mpaka tujue sababu ya kukamatwa kwa Minja, tutayafungua endapo tutaelezwa sababu za kukamatwa kwake,” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.
 
Minja alikamatwa juzi  na Jeshi la Polisi na kusafirishwa kupelekwa mjini Dodoma kujibu mashitaka ya kuhamasisha wafanyabiashara wa mkoa huo wagome kufungua maduka kupinga matumizi ya EFDs.
 
Imeandikwa na Daniel Mkate, Mwanza, Peter Mkwavila, Dodoma; Gideon Mwakanosya, Songea; George Tarimo, Iringa na Hussein Ndubikole, Dar.
 
CHANZO: NIPASHE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa