Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani
amesema, serikali haitamvumilia na kumuonea huruma mkurugenzi wa
halmashauri, mji, manispaa na jiji ambaye atashindwa kasi ya utendaji wa
Serikali ya Awamu ya Tano.
Mbali na hilo, Naibu Waziri amewaagiza wakurugenzi wote hapa nchini
kutumia rasilimali za msitu zilizoko katika wilaya zao kumaliza tatizo
la madawati na kusema kwamba hakuna mwanafunzi yeyote atakayekaa chini
kwa kukosa dawati.
“Agizo hili ni la serikali ya awamu ya tano, sisi hatuangalii wapi ni
lazima uwajibike pale unapoona mambo hayaendi vizuri, hata mkurugenzi
wangu na wewe agizo hili linakuhusu, mkurugenzi tumia rasilimali za miti
zilizoko katika halmshauri yako kupunguza tatizo la madawati kama
lipo,” alisema Ngonyani.
Naibu Waziri ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, ametoa kauli
hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na madiwani na baadhi ya
watumishi wa halmashauri ya Namtumbo katika kikao cha Baraza la
Madiwani.
Alisema amepiga marufuku tabia ya madiwani kufanya biashara na
halmashauri kwa kuwa jambo hilo linaweza kuleta mtafaruku kwa
halmashauri na hivyo kushindwa kukamilika kwa miradi ya maendeleo.
Alisema hata yeye japokuwa ni mbunge wa jimbo hilo, hatoweza kufanya
biashara Na halmashauri kwani ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma
hivyo kila kiongozi kuanza kujitafakari nafasi aliyonayo kwa wananchi.
Aidha amewataka madiwani hao kuhakikisha kwamba wanashirikiana na
watumishi wa halmashauri kupunguza tatizo la uhaba wa matundu ya choo,
madawati na upungufu wa zahanati katika maeneo yao.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment