Imeandikwa na Muhidini Amri, Songea
|
Dk Mashinji alifikishwa mahakamani hapo jana na wanachama wengine
watano wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Polisi wa Kituo Kikuu cha
Polisi Songea Mjini. Walisomewa mashitaka mawili ya kufanya mkusanyiko
usio halali na kufanya maandamano kinyume cha sheria, ambayo yanaweza
kuhatarisha usalama wa nchi.
Akisoma mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa
wa Ruvuma, Simon Kobelo, Wakili Mfawidhi wa Serikali kutoka Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Songea, Renatus Mkude alidai Julai
15, mwaka huu mjini Mbamba Bay wilayani Nyasa, washitakiwa walikamatwa
na Polisi wakiwa katika maandamano bila kuwa na kibali.
Aidha, Mkude alifafanua kuwa kosa lingine ni kufanya mkusanyiko
kinyume cha sheria, hivyo kuhatarisha usalama wa nchi. Katika kesi hiyo
ya jinai namba 113 ya mwaka 2017, mbali na Dk Mashinji, washitakiwa
wengine ni wabunge Zubeda Sakuro wa Viti Maalumu na Mwenyekiti wa
Chadema Kanda ya Kusini Masasi na mbunge wa Ndanda kupitia chama hicho,
Cecil Mwambe.
Wengine ni Katibu wa Ulinzi wa Taifa wa Chadema, Sanuda Madawa,
Katibu Mwenezi Kanda ya Kusini Masasi, Charles Makunguru na Katibu wa
Chadema Kanda ya Kusini Masasi, Filbert Ngatunga.
Washitakiwa baada ya kusomewa mashitaka yao, walikana kutenda makosa
hayo. Hata hivyo wakati wanasheria wa Chadema wakikamilisha taratibu ya
dhamana, Jeshi la Polisi liliwachukua washitakiwa na kuwapandisha kwenye
gari na kuwapeleka rumande hadi kesho, ambapo kesi hiyo itatajwa tena.
DK Mashinji na wanachama hao walikamatwa Julai 15, mwaka huu katika
mji mdogo wa Mbamba Bay wilayani Nyasa na Jeshi la Polisi Wilaya ya
Nyasa wakiwa katika maandamano na kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria,
licha ya serikali kuzuia mikutano yote vyama vya siasa.
Baada ya washitakiwa hao kushikiliwa na polisi wilayani Nyasa kwa saa
48, walipata dhamana kabla ya Jumanne na kupelekwa Ofisi ya Kamanda wa
Polisi Mkoa mjini Songea, kabla ya jana kufikishwa mahakamani kujibu
tuhuma hizo.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Edson Mbogoro ulilalamikia
kitendo cha wateja wao, kupelekwa mahabusu kwani hakimu tayari alishatoa
ruhusa ya dhamana kwa washitakiwa, jambo ambalo alisema ni kinyume cha
taratibu.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment