Wasafirishaji Ruvuma wadai mil. 375/-


na Stephano Chitete, Songea
WASAFIRISHAJI wa mizigo mkoani Ruvuma, wameitaka Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuona umuhimu wa kuwalipa deni lao la sh milioni 375 wanazozidai kwenye kitengo cha Taifa cha kuhifadhi mahindi kilichopo (SGR).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasafirishaji hao ambao wameomba majina yao yahifadhiwa, walisema kuwa walikopwa kuyasafirisha mahindi hayo kwa ahadi kuwa fedha zao wangelipwa mara baada ya kumaliza kazi lakini hadi sasa hawajalipwa.
Walisema kuwa wafanyabiashara wengine waliikodisha serikali magodauni ili wahifadhi mahindi hayo kwa sababu yale ya kituo cha hifadhi kilichopo mjini hapa hayakuwa na uwezo wa kumdu mahindi yote.
Walisema kuwa walijitahidi kwa uaminifu mkubwa kufanya kazi hiyo ya kubeba mahindi kutoka kwenye maeneo ambayo miundombinu yake ni mibovu pasipo kujali vipuri vya magari na mafuta kupanda bei.
“Tuna mikopo ya benki na tunalipa kodi mbalimbali zikiwamo za Mamlaka ya Mapato (TRA) na kuchangia michango mbalimbali ya maendeleo mkoani hapa lakini tunashangazwa na kitendo cha serikali kutowathamini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani hapa, Mays Mkwembe, alisema kuwa wafanyabiashara wengi ambao waliikopesha serikali wamekuwa wakihangaika sana katika shughuli zao kutokana na kuidai fedha nyingi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko, alikiri kuwa wafanyabiashara wanaidai serikali kutokana na huduma waliyoitoa hivyo wasubiri kidogo kwani wanaandaa utaratibu wa kuwalipa. 
Chanzo: Tanzania Daima

Kampuni kufundisha wakulima 100,000 shamba darasa


Mwandishi Wetu, Songea
KAMPUNI ya Lutukira Mixed Farm Project  yenye makao yake jijini  Dar es Salaam imepanga kutoa mafunzo ya shamba darasa kwa wakulima 100,000 watakaozunguka eneo la mradi wa  uwekezaji wa kilimo  cha karanga,ufuta  na alizeti  wilayani Songea.

Mradi huo tayari umepata eneo la ekari 20,000 za kulima mazao ya kibiashara na kujenga kiwanda cha kukamua mafuta ya mbegu. Wakulima watakaofundishwa watalima mazao mbalimbali na kuyauza kwenye kampuni hiyo ambayo itayakamua na kuyaunza nje ya nchi. 

Mwenyekiti ambaye pia ni  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni  hiyo, Alhaji Said Kilahama alisema hayo jana jijini hapa alipozungumzia mkakati ya kutekeleza mradi wa kilimo Lutukira Mixed Farm Project.
Alisema  mafunzo hayo yatatolewa katika kipindi cha miaka 10 ijayo  kwa njia ya vitendo.

Kilahama alisema kampuni yake itatekeleza mpango huo katika Kijiji cha Lutukira ambako  imepata ekari 50,000 za mradi wa kilimo cha kibiashara kwa  mazao ya karanga, ufuta  na alizeti na kwamba kwa sasa tayari ekari 300 zimelimwa.

“Ndugu waandishi, kampuni yangu kwa ushirikiano na Kampuni ya Montara Land Limited iliyoandikishwa Seychelles ilianza  mradi kwa kutenga Dola 3 milioni za Marekani  ili kupata eneo la kilimo cha kibiashara ikiwa ni kuitikia wito wa Serikali ya Tanzania kuboresha kilimo nchini’’ alisema.

Alisema mradi huo utaajiri  wafanyakazi  61 wa kudumu na wengine 100 watakuwa wakiajiriwa wakati wa kipindi maalumu cha kazi nyingi.

Mwenyekiti huyo alipongeza ushirikiano mzuri alioanza kuupata kutoka kwa wananchi  wa Lutukira ,viongozi wa Wilaya ya Songea na Mkoa wa Ruvuma  kwa ujumla katka kutekeleza mpango huo.

Kuhusu huduma za jamii, Kilahama alisema mradi huo utashirikiana kwa karibu na wananchi ambapo  sasa inawapatia trekta wananchi ili walitumie katika kilimo na kwamba pia itashirikiana na  Serikali katika kupunguza kero za jamii hususan masuala ya afya, elimu, maji  na kuondoa njaa nchini.

Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa kulima mazao ya alizeti na karanga ambayo yatakuwa na soko la uhakika katika kampuni yake.Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ,Said Mwambungu alinukuliwa akiwataka wakazi wa mkoa huo kushirikiana vizuri na wawekezaji.
Chanzo: Mwananchi

Mwandishi MCL ahukumiwa kwa rushwa


Mwandishi Wetu, Songea

MWANDISHI wa Gazeti la Mwananchi mkoani Ruvuma, Kwirunus Mapunda amehukumiwa kwenda jela miaka sita au kulipa faini ya Sh 1,000,000 baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa kutoka Shirika la Watawa Wabenediktine la Peramiho. 

Mapunda ametiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Songea wiki iliyopita chini ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Elizabeth Misana. Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Christa Kabekenga alidai kwamba Mapunda alitenda kosa hilo Desemba mwaka jana kwa kuomba rushwa ya Sh2 milioni ili asiandike habari mbaya za shirika hilo la Wabenediktine, lililo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Songea. 

Ilidaiwa kwamba baada ya kuomba kiasi hicho uongozi wa shirika hilo ulitoa taarifa Takukuru ambayo ilimwekea mtego na kumnasa. 

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Misana alisema baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, mahakama yake iliamua kutoa adhabu kali kwa kila kosa miaka mitatu ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo. Hata hivyo baada ya hukumu hiyo, Mapunda alilipa faini ya Sh1,000,000 na kunusurika kwenda jela.
Chanzo: Mwananchi

Mgogoro wa ardhi wamalizika


Na Amon Mtega, Songea
MGOGORO wa ardhi kati ya wananchi wa Kijiji cha Lutukila, Kata ya Mkongotema, Songea Vijijini na mwekezaji wa shamba la Kampuni ya Lutukila Mixed Farm umekwisha, baada ya mwekezaji huyo kukubali kukaa meza moja na wanakijiji hao kwa kukubaliana masuala ya msingi yaliyokuwa yakihitajika kabla ya kusaini mkataba wa umiliki wa shamba hilo.

Makubaliano hayo yalifanyika mjini hapa jana, wakati wa mkutano uliofanyika katika kijiji hicho, baada ya wananchi hao kumtaka mwekezaji huyo akubaliane na mahitaji waliyokuwa wakihitaji.

Akiwakilisha madai yao, Mwenyekiti wa Kamati ya Kufuatilia Makubaliano, Eligius Danda, alisema mambo wanayotaka wafanyiwe ni maji ya bomba, kuchangia utengenezaji wa barabara ziendazo mashambani, ukarabati wa madarasa ya shule za sekondari na msingi, trekta litakalosaidia kubadili kilimo cha mkono kwenda cha kisasa, ujenzi wa kituo cha afya na vitabu vya shule.

“Naomba ndugu zangu tusieleweke vibaya, wanakijiji wa Lutukila hatukusema hatumtaki mwekezaji, hapana, bali tunahitaji mwekezaji ambaye naye anashiriki mambo ya kijamii katika sehemu husika aliyowekeza, ikiwamo kutoa michango mbalimbali inayotakiwa,” alisema Danda.

Alisema kama wanakubaliana hayo, basi mgogoro haupo, kwa kuwa wana uelewa mkubwa kuwa uchumi katika kijiji hicho utapanda kwa baadhi ya vijana wao kupata ajira na wengine kulima kilimo chenye tija kutokana na elimu watakayoipata kutoka kwa mwekezaji huyo. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Said Kilahama, alisema yeye ni mmoja wa familia ya wanakijiji cha Lutukila, kwa kuwa ana dhamira ya wazi kuwekeza katika kijiji hicho.

Alisema kwa upande wa maji, trekta, vitabu vya ziada na kiada, vitaanza mara moja iwezekanavyo pindi mkataba utakaposainiwa na vitu vingine vinahitaji viende taratibu, kama ujenzi wa kituo cha polisi na nyumba zake na utoaji wa ajira za kudumu kwa wenye taaluma.

“Eneo hili nilianza kulifuatilia mwaka 1991 na 1992 nilifanikisha kulipata na mliokuwa mkiniongoza ni ninyi wenzangu na nikapata vibali, sasa leo hii nashangaa kuona maneno mengi yanajitokeza bila sababu wakati mimi ni mwenzenu,” alisema Kilahama.

Alisema shamba hilo ni la kimataifa na lina ekari 50,000, zinazotakiwa kulimwa ni ekari 15,000, kwa kuwa sehemu nyingine haifai kulimwa kwa ushauri wa wataalamu.

Katika hatua nyingine, kampuni hiyo imetoa msaada wa madirisha yenye thamani ya Sh milioni 3.6 kwenye jengo la mtandao wa polisi jamii la wanawake, ambalo limejengwa kwa nguvu ya wananchi ambapo hadi sasa limegharimu Sh milioni 10.5.
Chanzo: Mtanzania

Bilioni 105 kujenga uwanja wa Ndege Mwanza
Na John Maduhu, Mwanza
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesaini mkataba wa Sh bilioni 105 na Kampuni ya Ujenzi ya Beijing Construction Engineering ya China, kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Mkataba wa ujenzi huo umesainiwa Mwanza mbele ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, ambapo upande wa TAA ulisainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Suleiman Suleiman na upande wa Kampuni ya Beijing ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Geng Bingjian.

Akizungumza baada ya utiaji saini mkataba huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Suleiman, alisema ujenzi wa uwanja huo unatarajiwa kuanza wiki ijayo na utahusisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege, jengo la abiria, maegesho ya ndege na mkataba wa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili.

Alisema katika mradi huo Serikali ya Tanzania imetoa Sh bilioni 85 na fedha nyingine kiasi cha Sh bilioni 20 zimetolewa na Benki ya BADEA pamoja na marafiki wengine wa Tanzania.

Akizungumza katika utiaji saini mkataba huo, Dk. Tizeba, alimtaka mkandarasi kuhakikisha anafanya kazi zake kwa mujibu wa mkataba na kueleza kuwa Serikali haitasita kusitisha mkataba huo endapo atashindwa kutekeleza majukumu yake.

“Fedha zipo, hivyo mkandarasi unapaswa ufanye kazi zako kama ambavyo mkabata unaeleza na kamwe serikali haiko tayari kupokea visingizio vya aina yoyote ambavyo vitasababisha mradi ushindwe kukamilika kwa wakati,” alisema Dk. Tizeba.

Naye Mkurugenzi wa Uhandisi na Ufundi wa Viwanja vya Ndege, White Majula, alisema kujengwa kwa uwanja huo kutazifanya ndege kubwa kutua na kuruka bila tatizo lolote na kukuza uchumi wa Mwanza na mikoa jirani.

Alisema uwanja huo utaongezewa mita 5,000 toka mita 3,000 zilizopo kwa sasa katika sehemu ya kurukia na kuufanya kuwa mojawapo ya viwanja vikubwa hapa nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.
Chanzo: Mtanzania

RC awasihi wana Ruvuma kuwakubali wawekezaji



Kwirinus Mapunda, Songea

SERIKALI mkoani Ruvuma imewataka wananchi kutowakatisha tamaa wawekezaji wanaofika kwenye maeneo yao kwa lengo la kuwekeza badala yake wawaunge mkono kwa kushirikiana nao ili kuinua hali ya uchumi wao na mkoa kwa ujumla.

Akizungumzia hali ya uwekezaji mkoani mwake, Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alisema Serikali imekuwa mstari wa mbele kuweka mazingira bora ya kuwavutia wawekezaji mkoani humo na kwamba kinachotakiwa ni kwa wananchi nao kuhakikisha wanatoa ushirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Jitihada za Serikali katika kuhamasisha wawekezaji mkoani hapa zinapaswa kuungwa mkono na wananchi wote kwani zitawapa manufaa makubwa,’’ alisema na kufafanua kwamba mkoa huo upo nyuma kwa uwekezaji ukilinganishwa na mikoa ya kaskazini ambapo wawekezaji ni wengi na wapo siku nyingi.

Alisema hivi karibuni wawekezaji walionekana kupenda kufanya shughuli za uwekezaji mkoani humo na kwamba sekta mbalimbali hususani kilimo na mifugo ni eneo muhimu linalofaa kwa uwekezaji.

Mwambungu alitoa mfano katika Kijiji cha Lutukira ambacho kipo katika Kata ya Mkongotema ambako kuna mwekezaji aliyepatikana, lakini baadhi ya wananchi wanadiwa kuwashawishi wengine wasikubaliane na wawekezaji.

Alisema jambo hilo linarudisha nyuma maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

 “Wakati umefika kwa kila anayependa maendeleo ya mkoa wetu asisite kuchangia mawazo ya kimaendeleo na kuachana na wale ambao wanataka wananchi waendelee kukaa katika hali ya umasikini”, alisema.

Naye Mwenyekiti wa mradi wa Lutukira Mixed Farm Ltd, Said Kilahama ambaye ni mwekezaji akizungumza na wananchi wa kijiji hicho alisema kuwa lengo la kuwekeza katika kijiji hicho ni kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

Kilahama alisema kuwa yeye atahakikisha makubaliano yale ambayo watatiliana saini kwenye mkataba anayatekeleza.

Chanzo: Mwananchi

Ufunguzi wa soko la Tumbaku Mkoani Ruvuma


Kaimu meneja wa chama cha ushirika cha wilaya ya Namtumbo na Songea(sonamcu) akimkabidhi risala ya wakulima wa chama hicho mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Abdala Lutavi.
Mwenyekiti wa SONAMCU,Awami Ngonyani akizumngumza wakati wa ufunguzi wa soko la Tumbaku katika kijiji cha Matepwende wilayani Namtumbo ,kulia mkuu wa wilaya hiyo Abdala Lutavi.
Baadhi ya wakulima wa tumbaku wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wakikagua tumbaku yao kabla ya kuuza kwa makampuni yanayonunua tumbaku kwenye ufunguzi wa mauzo ya zao hilo katika kijiji cha Matepwende wilayani humo.
Wakulima wa Tumbaku kutoka katika kata ya Lwinga wilayani Namtumbo wakiangalia tumbaku yao kabla ya kuanza kwa zoezi la kuuza kwa makampuni yanayonunua tumbaku wilayani humo.Picha na Muhidin Amri,Globu ya Jamii-Ruvuma.
Picha kwa Hisani ya Michuzi Blog

MWENGE WA UHURU WAKIMBIZWA WILAYA YA NAMTUMBO





Mwenge wa Uhuru ukikimbizwa kuingia katika wilaya ya Namtumbo
kuanza kazi ya kuhamasisha shughuli za maendeleo ukitokea wilaya ya
Songea.Jumla ya miradi  11 yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 400
imezinduliwa,imewekewa mawe ya msingi na kufunguliwa.



Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kapteni Honest Mwanossa akichanganya
mbolea wakati wa uzinduzi wa shamba la michungwa  kwa kutumia  mbolea
vunde kwa kuongeza ubora wa mazao na hifadhi ya mazingira katika kijiji
cha Msindo wilaya ya Namtumbo.Shamba hilo lenye ukubwa wa hekari mbili
na nusu linamilikiwa na Mzee Venant Haule (mwenye fulana nyekundu).
Mtoto Mezea Seif wa darasa la kwanza katika shule ya msingi
Njalamatata akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru  wakati ulipokuwa katika
kijiji hicho wilaya ya Namtumbo kwa kazi ya kuhimiza shughuli za
maendeleo  jana.
-Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kapteni Honest Mwanossa akizindua
mradi wa kisima cha maji safi ya kunywa kwa ajili ya wanafunzi wa shule
ya sekondari ya Utwango wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.Kulia ni Mbunge
wa jimbo la Namtumbo Vita Kawawa.
 Raia wa Marekani aliyefahamika kwa jina moja la Penzia akiwa
ameshika Mwenge wa Uhuru wakati uliposimama katika kijiji cha Hanga
kutoa ujumbe kwa wananchi kuhusu umuhimu wa wananchi kujiandaa
kuhesabiwa ifikiapo Agosti 26,2012.






Na Revocatus A.Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Ruvuma


 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa