Home » » RC awasihi wana Ruvuma kuwakubali wawekezaji

RC awasihi wana Ruvuma kuwakubali wawekezaji



Kwirinus Mapunda, Songea

SERIKALI mkoani Ruvuma imewataka wananchi kutowakatisha tamaa wawekezaji wanaofika kwenye maeneo yao kwa lengo la kuwekeza badala yake wawaunge mkono kwa kushirikiana nao ili kuinua hali ya uchumi wao na mkoa kwa ujumla.

Akizungumzia hali ya uwekezaji mkoani mwake, Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alisema Serikali imekuwa mstari wa mbele kuweka mazingira bora ya kuwavutia wawekezaji mkoani humo na kwamba kinachotakiwa ni kwa wananchi nao kuhakikisha wanatoa ushirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Jitihada za Serikali katika kuhamasisha wawekezaji mkoani hapa zinapaswa kuungwa mkono na wananchi wote kwani zitawapa manufaa makubwa,’’ alisema na kufafanua kwamba mkoa huo upo nyuma kwa uwekezaji ukilinganishwa na mikoa ya kaskazini ambapo wawekezaji ni wengi na wapo siku nyingi.

Alisema hivi karibuni wawekezaji walionekana kupenda kufanya shughuli za uwekezaji mkoani humo na kwamba sekta mbalimbali hususani kilimo na mifugo ni eneo muhimu linalofaa kwa uwekezaji.

Mwambungu alitoa mfano katika Kijiji cha Lutukira ambacho kipo katika Kata ya Mkongotema ambako kuna mwekezaji aliyepatikana, lakini baadhi ya wananchi wanadiwa kuwashawishi wengine wasikubaliane na wawekezaji.

Alisema jambo hilo linarudisha nyuma maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

 “Wakati umefika kwa kila anayependa maendeleo ya mkoa wetu asisite kuchangia mawazo ya kimaendeleo na kuachana na wale ambao wanataka wananchi waendelee kukaa katika hali ya umasikini”, alisema.

Naye Mwenyekiti wa mradi wa Lutukira Mixed Farm Ltd, Said Kilahama ambaye ni mwekezaji akizungumza na wananchi wa kijiji hicho alisema kuwa lengo la kuwekeza katika kijiji hicho ni kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

Kilahama alisema kuwa yeye atahakikisha makubaliano yale ambayo watatiliana saini kwenye mkataba anayatekeleza.

Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa