Home » » Mwandishi MCL ahukumiwa kwa rushwa

Mwandishi MCL ahukumiwa kwa rushwa


Mwandishi Wetu, Songea

MWANDISHI wa Gazeti la Mwananchi mkoani Ruvuma, Kwirunus Mapunda amehukumiwa kwenda jela miaka sita au kulipa faini ya Sh 1,000,000 baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa kutoka Shirika la Watawa Wabenediktine la Peramiho. 

Mapunda ametiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Songea wiki iliyopita chini ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya hiyo, Elizabeth Misana. Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Christa Kabekenga alidai kwamba Mapunda alitenda kosa hilo Desemba mwaka jana kwa kuomba rushwa ya Sh2 milioni ili asiandike habari mbaya za shirika hilo la Wabenediktine, lililo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Songea. 

Ilidaiwa kwamba baada ya kuomba kiasi hicho uongozi wa shirika hilo ulitoa taarifa Takukuru ambayo ilimwekea mtego na kumnasa. 

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Misana alisema baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, mahakama yake iliamua kutoa adhabu kali kwa kila kosa miaka mitatu ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo. Hata hivyo baada ya hukumu hiyo, Mapunda alilipa faini ya Sh1,000,000 na kunusurika kwenda jela.
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa