Home » » Mgogoro wa ardhi wamalizika

Mgogoro wa ardhi wamalizika


Na Amon Mtega, Songea
MGOGORO wa ardhi kati ya wananchi wa Kijiji cha Lutukila, Kata ya Mkongotema, Songea Vijijini na mwekezaji wa shamba la Kampuni ya Lutukila Mixed Farm umekwisha, baada ya mwekezaji huyo kukubali kukaa meza moja na wanakijiji hao kwa kukubaliana masuala ya msingi yaliyokuwa yakihitajika kabla ya kusaini mkataba wa umiliki wa shamba hilo.

Makubaliano hayo yalifanyika mjini hapa jana, wakati wa mkutano uliofanyika katika kijiji hicho, baada ya wananchi hao kumtaka mwekezaji huyo akubaliane na mahitaji waliyokuwa wakihitaji.

Akiwakilisha madai yao, Mwenyekiti wa Kamati ya Kufuatilia Makubaliano, Eligius Danda, alisema mambo wanayotaka wafanyiwe ni maji ya bomba, kuchangia utengenezaji wa barabara ziendazo mashambani, ukarabati wa madarasa ya shule za sekondari na msingi, trekta litakalosaidia kubadili kilimo cha mkono kwenda cha kisasa, ujenzi wa kituo cha afya na vitabu vya shule.

“Naomba ndugu zangu tusieleweke vibaya, wanakijiji wa Lutukila hatukusema hatumtaki mwekezaji, hapana, bali tunahitaji mwekezaji ambaye naye anashiriki mambo ya kijamii katika sehemu husika aliyowekeza, ikiwamo kutoa michango mbalimbali inayotakiwa,” alisema Danda.

Alisema kama wanakubaliana hayo, basi mgogoro haupo, kwa kuwa wana uelewa mkubwa kuwa uchumi katika kijiji hicho utapanda kwa baadhi ya vijana wao kupata ajira na wengine kulima kilimo chenye tija kutokana na elimu watakayoipata kutoka kwa mwekezaji huyo. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Said Kilahama, alisema yeye ni mmoja wa familia ya wanakijiji cha Lutukila, kwa kuwa ana dhamira ya wazi kuwekeza katika kijiji hicho.

Alisema kwa upande wa maji, trekta, vitabu vya ziada na kiada, vitaanza mara moja iwezekanavyo pindi mkataba utakaposainiwa na vitu vingine vinahitaji viende taratibu, kama ujenzi wa kituo cha polisi na nyumba zake na utoaji wa ajira za kudumu kwa wenye taaluma.

“Eneo hili nilianza kulifuatilia mwaka 1991 na 1992 nilifanikisha kulipata na mliokuwa mkiniongoza ni ninyi wenzangu na nikapata vibali, sasa leo hii nashangaa kuona maneno mengi yanajitokeza bila sababu wakati mimi ni mwenzenu,” alisema Kilahama.

Alisema shamba hilo ni la kimataifa na lina ekari 50,000, zinazotakiwa kulimwa ni ekari 15,000, kwa kuwa sehemu nyingine haifai kulimwa kwa ushauri wa wataalamu.

Katika hatua nyingine, kampuni hiyo imetoa msaada wa madirisha yenye thamani ya Sh milioni 3.6 kwenye jengo la mtandao wa polisi jamii la wanawake, ambalo limejengwa kwa nguvu ya wananchi ambapo hadi sasa limegharimu Sh milioni 10.5.
Chanzo: Mtanzania

Bilioni 105 kujenga uwanja wa Ndege Mwanza
Na John Maduhu, Mwanza
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesaini mkataba wa Sh bilioni 105 na Kampuni ya Ujenzi ya Beijing Construction Engineering ya China, kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Mkataba wa ujenzi huo umesainiwa Mwanza mbele ya Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba, ambapo upande wa TAA ulisainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Suleiman Suleiman na upande wa Kampuni ya Beijing ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Geng Bingjian.

Akizungumza baada ya utiaji saini mkataba huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Suleiman, alisema ujenzi wa uwanja huo unatarajiwa kuanza wiki ijayo na utahusisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege, jengo la abiria, maegesho ya ndege na mkataba wa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili.

Alisema katika mradi huo Serikali ya Tanzania imetoa Sh bilioni 85 na fedha nyingine kiasi cha Sh bilioni 20 zimetolewa na Benki ya BADEA pamoja na marafiki wengine wa Tanzania.

Akizungumza katika utiaji saini mkataba huo, Dk. Tizeba, alimtaka mkandarasi kuhakikisha anafanya kazi zake kwa mujibu wa mkataba na kueleza kuwa Serikali haitasita kusitisha mkataba huo endapo atashindwa kutekeleza majukumu yake.

“Fedha zipo, hivyo mkandarasi unapaswa ufanye kazi zako kama ambavyo mkabata unaeleza na kamwe serikali haiko tayari kupokea visingizio vya aina yoyote ambavyo vitasababisha mradi ushindwe kukamilika kwa wakati,” alisema Dk. Tizeba.

Naye Mkurugenzi wa Uhandisi na Ufundi wa Viwanja vya Ndege, White Majula, alisema kujengwa kwa uwanja huo kutazifanya ndege kubwa kutua na kuruka bila tatizo lolote na kukuza uchumi wa Mwanza na mikoa jirani.

Alisema uwanja huo utaongezewa mita 5,000 toka mita 3,000 zilizopo kwa sasa katika sehemu ya kurukia na kuufanya kuwa mojawapo ya viwanja vikubwa hapa nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa