Mwandishi Wetu, Songea
KAMPUNI ya Lutukira Mixed Farm Project yenye makao yake jijini Dar es Salaam imepanga kutoa mafunzo ya shamba darasa kwa wakulima 100,000 watakaozunguka eneo la mradi wa uwekezaji wa kilimo cha karanga,ufuta na alizeti wilayani Songea.
Mradi huo tayari umepata eneo la ekari 20,000 za kulima mazao ya kibiashara na kujenga kiwanda cha kukamua mafuta ya mbegu. Wakulima watakaofundishwa watalima mazao mbalimbali na kuyauza kwenye kampuni hiyo ambayo itayakamua na kuyaunza nje ya nchi.
Mwenyekiti ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Alhaji Said Kilahama alisema hayo jana jijini hapa alipozungumzia mkakati ya kutekeleza mradi wa kilimo Lutukira Mixed Farm Project.
Alisema mafunzo hayo yatatolewa katika kipindi cha miaka 10 ijayo kwa njia ya vitendo.
Kilahama alisema kampuni yake itatekeleza mpango huo katika Kijiji cha Lutukira ambako imepata ekari 50,000 za mradi wa kilimo cha kibiashara kwa mazao ya karanga, ufuta na alizeti na kwamba kwa sasa tayari ekari 300 zimelimwa.
“Ndugu waandishi, kampuni yangu kwa ushirikiano na Kampuni ya Montara Land Limited iliyoandikishwa Seychelles ilianza mradi kwa kutenga Dola 3 milioni za Marekani ili kupata eneo la kilimo cha kibiashara ikiwa ni kuitikia wito wa Serikali ya Tanzania kuboresha kilimo nchini’’ alisema.
Alisema mradi huo utaajiri wafanyakazi 61 wa kudumu na wengine 100 watakuwa wakiajiriwa wakati wa kipindi maalumu cha kazi nyingi.
Mwenyekiti huyo alipongeza ushirikiano mzuri alioanza kuupata kutoka kwa wananchi wa Lutukira ,viongozi wa Wilaya ya Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla katka kutekeleza mpango huo.
Kuhusu huduma za jamii, Kilahama alisema mradi huo utashirikiana kwa karibu na wananchi ambapo sasa inawapatia trekta wananchi ili walitumie katika kilimo na kwamba pia itashirikiana na Serikali katika kupunguza kero za jamii hususan masuala ya afya, elimu, maji na kuondoa njaa nchini.
Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa kulima mazao ya alizeti na karanga ambayo yatakuwa na soko la uhakika katika kampuni yake.Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ,Said Mwambungu alinukuliwa akiwataka wakazi wa mkoa huo kushirikiana vizuri na wawekezaji.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment