Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Baadhi ya wafanyabiashara wa mjini Songea wamelazimishwa na
wenzao kuingia katika mgomo wa kupinga matumizi ya mashine za
kielektroniki za kutolea risiti za EFD.
Waliolazimishwa ni wamiliki wa baa na vituo vya
kuuza mafuta ambao wamekuwa wakiendelea kufanya biashara zao kabla ya
baadhi ya wenzao kukodisha ‘mabaunsa’ kuwalazimisha kufunga biashara zao
kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wasaliti.
Pamoja na serikali mkoani Ruvuma kutumia polisi
kufanya doria katika maeneo mbalimbali ya mji mgomo huo umeendelea huku
wahusika wakishinikiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa
wa Ruvuma, Apily Mbaruku afukuzwe kazi au ache kuwaandikia barua za
vitisho za kutumia mashine hizo.
Akizungumzia shinikizo hilo, Mbaruku alisema
hatishwi na wafanyabiashara hao na kusema kuwa TRA inawataka
wafanyabiashara kuendelea kutumia mashine hizo.
Akizungumza wakati wa kikao kilichofanyika kwenye
Ukumbi wa Bombambili jana, msemaji wa wafanyabiashara hao, John Oscar
alisema wamechoka kuburuzwa na TRA na safari hii mgomo walioitisha ni
mkubwa ukihusisha wafanyabiashara wa kada mbalimbali.
Alidai kuwa mashine hizo ni mpango wa wakubwa
ambao wanataka kupata fedha kupitia wao na kumtaka meneja wa TRA wa mkoa
kuacha tabia ya kuwakejeli kuwa hawana uwezo wa kufunga maduka kwa wiki
moja.
Akisoma maazimio ya mkutano huo, makamu mwenyekiti
wa umoja wa wafanyabiashara hao, Wilson Mbilinyi alisema hawatafungua
maduka yao kwa siku mbili na baada ya hapo wataandamana kwenda ofisi za
TRA kwa ajili ya kuzifunga kutokana na kushindwa kusikiliza matatizo
yao.
0 comments:
Post a Comment