Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, amepongeza mradi wa ujenzi
wa majengo ya Shule ya Sekondari Unberkant iliyopo kwenye Kata ya
Mtipwili wilayani Nyasa mkoani hapa unaofanywa na Kampuni ya Ovans
Construction (Ltd) ya Mbinga.
Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kupitia Serikali ya Tanzania kwa thamani ya sh 288,254,380.
Mwambungu alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki baada ya kutembelea
shuleni hapo kwa lengo la kujionea maendeleo ya ujenzi alipofanya ziara
wilayani Nyasa.
Alisema mkandarasi anayesimamia mradi huo anastahili pongezi kwa
kuonyesha uzalendo na uaminifu katika ujenzi huo wa kiwango
kinachotakiwa ambapo amewataka wengine kuiga mfano huo kwa madai kwamba
hali hiyo itasaidia kuokoa fedha nyingi za serikali ambazo zinapotea
kutokana na baadhi yao kujenga miradi chini ya kiwango.
Kutokana na hali hiyo mkuu wa mkoa huyo amezitaka halmashauri zote
mkoani hapa kuhakikisha zinatoa kazi za ujenzi kwa makandarasi
wazalendo, huku akionya matendo ya rushwa kwa madai kwamba kufanya
hivyo kunasababisha kupata makandarasi wabovu.
Kwa upande wake, mkuu wa shule hiyo ya sekondari, David Kilowoko,
akisoma taarifa ya shule yake mbele ya mkuu wa mkoa huyo, alisema mradi
huo wa ujenzi wa nyumba moja ya mwalimu, maabara moja, matundu nane ya
vyoo vya wanafunzi, mfumo wa uwekaji wa umeme wa jua na mfumo wa maji
ya kisima na ukarabati wa vyumba sita vya madarasa umefanikiwa kupitia
mpango wa matokeo makubwa sasa unaotekelezwa katika sekta ya elimu.
Kilowoko alisema kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari wa
awamu ya pili (SEDP II), shule hiyo pia imepata kiasi cha shilingi
milioni 26 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba moja ya mwalimu ambayo
itatumiwa na familia za walimu wawili.
Akizungumzia kwa upande wa taaluma, alisema kuwa shule hiyo
inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi
ambapo hadi sasa shule hiyo ina mwalimu mmoja tu wa somo hilo na kudai
kwamba hali hiyo imesababisha kupata matokeo yasiyoridhisha ambayo
yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na upungufu wa walimu.
Aidha mkuu huyo wa shule ameishukuru serikali kwa jitihada zake za
kuboresha miundombinu ya shule jambo ambalo amedai kuwa hali hiyo
itakuwa chachu ya maendeleo ya elimu kutokana na kuwa mazingira ya
kusomea na kufundishia yatakuwa rafiki.
Chanzo;anzania Daima
0 comments:
Post a Comment