Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewataka Watanzania wasikubali
kuchagua viongozi wanaotafuta uongozi kwa kutumia fedha kwani zinaweza
kuleta machafuko.
Alisema hayo jana wakati wa ibada maalumu ya
kumsimika Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Dayosisi ya Ruvuma, Amon Mwenda kwenye kanisa hilo la Usharika wa Songea
iliyohudhuriwa na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali.
“Ndugu zangu ninawaambia kuwa msigeuze uchaguzi
kuwa mtaji, bali tuzingatie taratibu na sheria za uchaguzi ambazo ndiyo
mwongozo unaoweza kutusaidia.
“Ninawasihi wananchi wawe makini na viongozi
wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye
Uchaguzi Mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza ni kwa nini atumie
fedha ili kupata nafasi ya uongozi?” alisema na kuongeza:
“Tatizo ni kwamba hata wananchi hivi sasa
wanakubali kupokea kile kinachotolewa na wagombea. Atakuja huyu atakupa
hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue akiingia madarakani
anaanza kurudisha haraka vile alivyowagawia.”
Aliwaomba viongozi wa dini na waumini kuendelea kuliombea taifa ili Mungu aliepushe na janga la watu kupenda rushwa.
Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea
mchakato wa kupata Katiba Mpya ili wajumbe wote warejee ndani ya Bunge
na kuikamilisha kazi waliyoianza.
Alisema Watanzania kwa sasa hivi wanahitaji kumwomba Mungu ili waendelee kuwa na amani.
Waziri Mkuu pia aliwataka Watanzania kujikita zaidi katika kilimo ambacho kitaweza kuwakomboa na kuondoa umaskini unaowakabili.
Alisema kila mwananchi anapaswa kufanya kazi kwa
bidii ili aweze kumudu maisha yake ya kila siku akitolea mfano wa
shughuli za kilimo na ujasiriamali badala ya kusubiri kusaidiwa.
Waziri Pinda alisema Dayosisi mpya ya Ruvuma
inapaswa kuweka mipango yakinifu ya maendeleo ambayo itaweza kuisaidia
Serikali kupunguza changamoto zilizopo kwa kuanzisha miradi ya elimu,
afya na shughuli mbalimbali za kijamii.
Awali, akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya
kusimikwa rasmi, Askofu Mwenda alisema dayosisi mpya ya Ruvuma imezaliwa
katika kipindi chenye changamoto nyingi za kidunia na utandawazi
ukiwamo mmomonyoko mkubwa wa maadili.
Hata hivyo, akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo anakuwa
Askofu wake wa kwanza, Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno la
Mungu, dayosisi hiyo itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na
akiba ya chakula cha kutosha.
Alisema watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani na nje kutoa huduma za kijamii hasa elimu na afya.
Aliahidi kukabiliana na changamoto za sasa ambazo
alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji ya albino,
unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa
hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa alisema Kanisa lingependa
kupata viongozi ambao ni wacha Mungu.
Askofu Malasusa alisema inashangaza kuona kuna
baadhi ya watu wanagombea nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na
Mungu aliyewaumba watu anaotaka kuwaongoza
Chanzo:Mwananchi