Home » » PSPF YAZAWADIA MADAWATI 90 KWA SHULE ZA TUNDURU

PSPF YAZAWADIA MADAWATI 90 KWA SHULE ZA TUNDURU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mfuko wa Pensheni kwa Umma (PSPF)
Mfuko wa Pensheni kwa Umma (PSPF) umetoa msaada wa madawati 90 yenye thamani ya shilingi milioni tano kwa ajili ya kusaidia kupunguza tatizo la madawati katika baadhi ya  shule za msingi za Wilaya ya Tunduru.
 
Akikabidhi msaada huo jana, Mwakilishi wa mfuko huo Mkoa wa Ruvuma, Deogratius Njuu, alisema, PSPF ni mdau mkubwa wa elimu wamegushwa na tatizo hilo hivyo wameona wasaidiane na halmashauri hiyo ili kupunguza tatizo hilo.
 
Njuu ameongeza kuwa, mfuko huo unaamini kuwa taifa lolote lenye maendeleo lazima libebwe na elimu na ndiyo maana nao wamepanga kusaidia katika kuinua kiwango cha elimu katika maendeleo mbali mbali nchini.
 
Aidha, amewashauri kuyatunza madawati hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kuwasaidia wanafunzi wote.
 
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Tunduru Kaskazini, Ramo Makani, amewapongeza PSPF kwa kutoa msaada huo kwa kuwa utasaidia kupunguza tatizo la  madawati na kuwataka wadau wengine watakao sikia waige mfano mzuri na bora  uliofanywa na mfuko huo.
 
Alisema, bado halmashauri inakabiliwa na changamoto nyingi kama upungufu wa madawati ambapo watoto wa shule za msingi wanakaa chini, upungufu wa matundu ya vyoo, meza, viti pamoja na miundombinu, hivyo amewaomba watu wenye uwezo wasaidiane na halmashauri kutatua matatizo hayo. 
 
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Kenneth Haule, alisema  kuwa halmashauri hiyo ina upungufu wa madawati 4537 ili kufanikisha utoaji elimu bora kwa watoto ni muhimu kuwapo kwa miundombinu na samani za kutosha zenye viwango kwa wanafunzi na walimu.
 
Alisema, wilaya hiyo inaupungufu mkubwa wa miundombinu na samani za kielimu vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, vyoo  pamoja na madawati ambapo jitihada kubwa za kupunguza tatizo hilo kwa kushirikiana na serikali kuu na jamii husika bado zinaendelea  kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi  wanaosajiliwa kila mwaka.
 
Aidha, alisema bado wilaya ina upungufu mkubwa wa samani za shule hivyo ameomba waendelee kusaidia kila wanapopata fursa ili kuendeleza sekta ya elimu nchini.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa