Home » » MWENYEKITI WA CHADEMA KANDA YA KUSINI AJIUZULU WADHIFA WAKE

MWENYEKITI WA CHADEMA KANDA YA KUSINI AJIUZULU WADHIFA WAKE



MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya  kusini  ambaye pia ni Mchungaji  wa Kanisa la Avangelisitic Assemblies of God Tanzania(EAGT),Joseph Matare  amejiuzulu nafasi yake hiyo kutokana na Kanisa lake hilo Kuagiza Wachungaji wake ambao ni Viongozi wa  Vyama vya Siasa kuachana na Nafasi zao za Kisiasa.

 Joseph Matare akizungumza na Waandishi wa habari Mjini Songea amesema kuwa ameamua kujuzulu Nafasi yake ya Uongozi wa  CHADEMA Kanda ya Kusini inayojumuisha Mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma kufuatia  Kanisa lake katika  Mkutano wake wa Kanda kuagiza Wachungaji wake wote ambao ni Viongozi wa Kisiasa kuachia nafasi zao na badala yake wasimamie Kazi ya Mungu  Katika Makanisa yao.


 ‘Kufuatia maagizo  ya Mkutano huo wa Kanisa uliofanyika Njombe nimeamua kutii na  leo tarehe 10 Julai  2014 nimeamua kujiuzulu  na  Katibu wangu Mkuu Dr Wilbroad Slaa nilimjulisha tangu tarehe 04 Juni mwaka huu’ alisema  Matare katika taarifa yake ya kujiuzulu.

 Anafafanua kuwa muda  wa Viongozi wa Kanda ulikuwa ni wa muda na wa mpito hadi  uchaguzi wa Kanda utakapopita  ambao ulipaswa kufanyika Juni 2014 na kwamba muda umeongezwa hivyo ameona aheshimu  maagizo yaliyomuweka madarakani.

 Hata hivyo Matare anasema kuwa anawatia moyo Makamanda wote wa CHADEMA  waliobaki kuendelea kupigania Nchi ili iondokane na uovu  unaotendeka sasa na kwamba Mungu atakuwa nao wale wote wanaotafuta haki kwa ajili ya Wananchi walio wengi.

 Anasema  kuwa ameondoka bila kuwa na Ugomvi na Kiongozi yeyote wa CHADEMA   hivyo wataendelea kushirikiana kutafuta  haki akiwa Mwanachama wa Kawaida na Mchungaji.

 Matare ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT  Mkuzo la Mjini Songea la Mkoani Ruvuma  amesema kuwa anatambua juhudi za Viongozi wa CHADEMA katika kupigania haki za Wananchi na Wabunge wote wa CHADEMA katika kupigania haki na kwamba ipo siku Mungu atawalipa ujira wa kazi wanayofanya.

 Anasema kuwa Mungu anatambua kazi  nzito wanayofanya Viongozi wa CHADEMA ambayo amesema ni ya kutafuta Ukombozi kamili wa Nchi na itakuwa  ni uendawazimu kubeza kazi hiyo.


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa