Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAFANYABIASHARA wa kampuni za ununuzi wa kahawa katika Halmashauri
ya Wilaya ya Mbinga, Ruvuma, wamekataa kuendelea kukatwa sh 20 kwa kila
kilo ya zao hilo kuchangia mfuko wa ununuzi wa dawa za kuthibiti
vidung’ata.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima Jumatano, baadhi
ya wafanyabiashara hao (majina yamehifadhiwa) walidai kuwa fedha
zinazokatwa kwa ajili ya kuchangia mfuko huo zinatumika kwa manufaa ya
wajanja wachache kwa sababu ugonjwa huo umetoweka miaka mitatu
iliyopita.
Walisema fedha zilipangwa kukatwa kipindi cha dharura kwa ajili ya
kulinusuru zao hilo lisishambuliwe na ugonjwa wa vidung’ata, lakini sasa
wamegeuza sheria licha ya ugonjwa huo kutoweka.
“Suala linalotakiwa ni kukaa mezani kati ya halmashauri na
wafanyabiashara wa kahawa badala ya kutumia ubabe kukata fedha hizo na
kufanya urasimu katika utoaji wa vibali vya kununulia zao hilo kwa sisi
tunaopinga suala hilo,” alisisitiza mmoja wao.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga, alisema madai ya
wafanyabiashara hao hayana ukweli, badala yake ametaka makato hayo
yaendelee hadi ugonjwa huo utakapotokomea kabisa huku akibainisha
kwamba baadhi ya maeneo yanasumbuliwa na vidung’ata.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment