Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Bijampola ni kijana
aliyekuwa na bidii sana shuleni, ndoto yake ilikuwa awe rubani pindi akimaliza
masomo yake ya taaluma hiyo. Kwa bahati mbaya kwa kijana huyo, wazazi wake
walikosa ada ya kumsomesha, hivyo akaishia darasa la nne na ndoto yake ikaishia
hapo, kwa sasa ni mtoto wa mitaani, inasikitisha. Je Bijampola angekuwa anasoma
kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano ndoto yake ingezimika au ingetimia!
Bila shaka ingetimia kwani Serikali hii imeamua kutoa Elimu ya Msingi bure.
Kati ya mambo ya
kupongezwa na kuungwa mkono ni hili suala la ELIMU BURE. Hakika Rais John Pombe
Joseph Magufuli na Serikali yake wanawajali wananchi na hasa wa kipato cha
chini ambao ndio wengi. Hili nalisema bila kificho kwani kutoa elimu kuanzia
awali, msingi hadi sekondari ni jambo la kushukuru sana na litafanya vipaji
vingi viweze kuibukka kwani wazazi hawatashindwa kuwapeleka watoto wao shule
kwa kisingizio cha kukosa ada. Hongera Mzee wa Hapa Kazi Tu.
Kwa msingi huu au mfumo
huu ndoto za akina Bijampola haziwezi kufa tena ni lazima zitimie. Ni dhahiri
kwamba watoto wengi walikuwa wanazagaa mitaani pasipo kwenda shule kwa sababu
wazazi wao hawakuwa na uwezo wa kuwasomesha. Baada ya elimu kutolewa bure
tunaona watoto wa mitaani kupungua kwa kiwango kikubwa.
Katika hotuba ya Mhe. Rais ya kufungua Bunge la
11 mnamo Novemba 20, 2015 mjini Dodoma, Dkt. Magufuli alisema yafuatayo kuhusu
elimu, “Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali,
msingi, sekondari na vyuo vikuu. Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza
katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo
katika masomo ya sayansi. Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya
kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu,
madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la
kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye
kampeni. Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu
wanapata mikopo kwa wakati. Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa
ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga
mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha zaidi”.
Wahenga husema haja ya
mja hunena, muungwana ni vitendo. Usemi huu umedhihirika na Serikali ya Awamu
ya Tano kutekeleza kwa vitendo yale wanayoahidi ikiwemo hili la elimu bure.
Ni ukweli usiopingika
kuwa kila mwenye kuthamini utu wa Mtanzania ni lazima akubaliane na kitendo cha
kiungwana kilichofanya na Serikali ya Magufuli kama Mhe. Mwenyewe anavyoinadi
cha kutoa elimu bure.
Ukweli huu
unadhihirishwa na Mkazi wa Mbweni ambaye ni mzazi wa watoto wawili, Bi Pelagia
Mpanda anayetoa ya moyoni kuhusu elimu bure. “ Kwa kweli ninamshukuru sana Mhe.
John Pombe Magufuli kwa kutoa elimu bure kwa watoto wetu, mimi nina watoto mapacha
ambao nimewasomesha kwa taabu sana kuanzia chekechea hadi darasa la saba.
Mamilioni ya pesa yamenitoka na si kwamba nilikuwa tajiri la hasha nimekuwa
nikikopa huku na kule na fedha nyingine nikipata kwenye shughuli za
ujasiriamali, lakini cha moto nilikiona.” Ameendelea kusema, “Nilivyosikia
Elimu inatolewa bure hadi sekondari nilishukuru sana nikashauriana na mume
wangu watoto wetu tukawapeleka sekondari ya serikali ambapo wanafanya vizuri,
kwa kweli nasema Magufuli umetujali sisi watu wa hali ya chini na Mungu
akulinde uendelee kutuongoza na kutusaidia,”
Mzazi huyu anaendela
kusema kwa sasa hapa presha na anasomesha watoto wake kwa raha na fedha
anayoipata anaielekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo. Amemwomba Mhe. Rais
atupie jicho hata kwenye shule binafsi wapunguze viwango vya ada ili wale ambao
bado wanasomeshja watoto wao katika shule hizo waweze nao kupata unafuu.
Elimu bure imegusa watu
wengi na kuwafurahisha, hapa Mratibu Elimu Kata ya Keko, Bi Happines Elias
jijini Dar es Salaam naye anasema haya kuhusu Elimu Bure, “Kwa kweli suala la
Elimu bure nimelipokea kwa mikono miwili, mimi kama mwalimu najua jinsi ambavyo
wazazi wamekuwa wakiangahika na michango mbali mbali kwa ajili ya watoto wao
shuleni, lakini baada ya vitu hivi kuondolewa wazazi na watoto wan amani na
watoto wanafanya vizuri darasani kwa sasa kwani hawana wasi wasi wa kufukuzwa.”
Mratibu huyu ameongeza
kusaema kuwa anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujali elimu na hasa
baada ya kuondoa ada haikuishia hapo bali imetoa madawati kwa kila shule,
watoto hawakai chini tena. Ameongeza kuwa yeye kipindi anafundisha aliwahi
kudondoka darasani wakati akipitapita katikati ya wanafunzi katika harakati za
kukwepa kuwakanyaga akadondoka chini. Hivyo kwa sasa anasema adha hiyo haipo tena
na anataraji ata viwango vya ufaulu vitaongezeka kwani mazingira ya kusomea
yameboreshwa.
Kuhusu furaha ya Elimu
bure, binti Mariam Yahaya, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Bunju Sekondari
yeye anasema suala la Elimu bure amelifurahia sana kwani baada ya kumaliza darasa la saba hakuwa na uhakika wa kuendelea
na masomo ya sekondari kwani wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumlipia ada.
Hivyo anasema, “Kwa kweli nimeruha sana kuwa Serikali inatoa elimu bure, hivyo
nina hakika nitaendelea na masomo yangu bila wasi wasi.”
Picha
ya Wanafunzi wakiwa Darasani
Naye
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), George Simbachawene ambaye ndiye msimamizi wa shule za msingi na
sekondari nchini anafafanua jinsi serikali ilivyojipanga kugharamia elimu ya
msingi, “SERIKALI inapeleka Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kugharimia
elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.”
Simbachawene anabainisha kuwa katika mpango huo,
Serikali itagharimia gharama zote za mtihani wa kidato cha nne kwa
wanafunzi wote, tofauti na miaka yote ambapo wanafunzi hutozwa gharama za
mitihani. Anasema fedha hizo zitatolewa moja kwa moja na Serikali kupia
Baraza la Mitihani (NECTA).
“Majukumu ya Serikali kuhusu utoaji elimu bila
malipo yameelezwa katika waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2015, Serikali
itabeba jukumu hili. Kutokana na kuwabana mafisadi tumeweza kupata fedha za
kutosha,”anasisitiza Simbachawene.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali inatoa ruzuku
ya uendeshaji wa shule Sh 10,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh 25,000
kwa mwanafunzi wa sekondari kila mwaka.
Simbachawene anaongeza kuwa Serikali itatoa fedha
kwa ajili ya fidia ya ada Sh 20,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya kutwa na Sh
70,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.
Ama kweli Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha
dhamira ya dhati ya kumkomboa mwanachi hasa wa kipato cha chini. Elimu Kwanza
na maendeleo yanafuata. Hii inadhihirisha kuwa Serikali hii imezidi kutambua
kuwa Elimu ni Ufunguo wa Maisha na ndio maana suala la elimu limepewa
kipaumbele na kuingizwa kwenye mradi wa matokeo makubwa sasa (BRN)
Ni mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano chini
ya Rais John Pombe Magufuli ambapo mengi mazuri yameonekana katika Elimu hasa
ili lililowaondolea wazazi wengi adha ya mikopo ili wawapelek watoto wao shule.
Heko JPM na Falsafa yako ya Hapa Kazi Tu
imedhihirika kwa vitendo.
MWISHO