Home » » DIRA: Kikwete na woga wa kufanya uamuzi mgumu

DIRA: Kikwete na woga wa kufanya uamuzi mgumu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wakati Rais Jakaya Kikwete akifungua Bunge Maalumu la Katiba wiki iliyopita mjini Dodoma alisema kuwa asingependa kuona muundo wa Serikali tatu ukitokea wakati bado akiwa madarakani.
Alisema angependa ikitokea hivyo iwe ni baada ya yeye kumaliza muda wake.
Ilikuwa baada ya kutoa ufafanuzi mrefu wa athari za kuchagua muundo wa serikali tatu huku akisisitiza msimamo wa chama chake, CCM wa serikali mbili.
Hotuba yake ilikuja siku chache tu baada ya mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuhutubia Bunge hilo.
Katika hotuba yake, Warioba alielezea jinsi tume yake ilivyokusanya maoni na mwelekeo wake katika hilo.
Alisema kati ya wananchi 38,000 waliotoa maoni yao kuhusu Muungano visiwani (Zanzibar), watu 19,000 walizungumzia suala la muundo huku zaidi ya nusu wakitaka marekebisho ya Katiba yatakayowezesha uwepo wa serikali tatu.
Kwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 61 ya waliotoa maoni juu ya Muungano walipendekeza serikali tatu na kwa upande wa Zanzibar asilimia 60 walipendekeza serikali ya mkataba.
Suala la  Muungano ni nyeti katika mchakato huu wa Katiba, hasa kwa kuwa limekuwa na malalamiko mengi kwa pande zote mbili, yaani Tanganyika na Zanzibar.
Ili kuonyesha kuwa Wazanzibari hawaridhishwi na Muungano huo, ndiyo maana mwaka 2010 walibadili Katiba yao iliyopora kabisa madaraka ya Serikali ya Muungano.
Kwa maana nyingine Katiba ya Muungano imeshavunjwa. Hapo tena kuna Muungano gani kama siyo kujifariji?
Kama kweli Rais Kikwete angekuwa na uchungu wa Muungano, mbona hakuchukua hatua dhidi ya kitendo hicho cha Wazanzibari? Huyu ndiye Rais aliyeapa kuilinda Katiba? Upo wapi ujasiri wake?
Ilitegemewa kuwa Rais Kikwete angetumie fursa hii kulipatia ufumbuzi wa kudumu, lakini anaogopa kuonekana mbaya kwa wana CCM wenzake na ndiyo maana ameamua kutoa maoni yake ya faida za serikali mbili katika muda ambao Bunge la Katiba linajiandaa kuanza kujadili Rasimu ya Katiba.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa