KIGOGO CHADEMA APANGUA KESI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbozi, imemwachia huru Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Harode Langisa “Jivava”, baada ya kumkuta hana hatia katika kesi ya jinai iliyokuwa ikimkabili namba 326 ya mwaka jana.
Mjumbe huyo, alikuwa akikabiliwa na kesi ya jinai ambapo alidaiwa kufanya makosa mawili ya shambulio la mwili na kuharibu mali, kesi iliyofunguliwa dhidi yake na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salome Ngusa, Oktoba 10, mwaka jana.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Rahim Mushi alisema Jivava alifikishwa mahakani hapo Oktoba 16 mwaka jana akituhumiwa kumshambulia Salome Ngusa wakati akitokea kwenye mkutano wa hadhara wa CCM na kuharibu mali zake eneo la mwaka mjini Tunduma.
Hakimu Mushi alisema kuwa baada ya upande wa mlalamikaji kutoa ushahidi mahakani hapo, mtuhumiwa Jivava alionekana na kesi ya kujibu na hivyo kutakiwa alete utetezi wake.
Alisema kuwa baada ya mahakama kusikiliza pande zote mbili, ilibaini kuwa upande wa mlalamikaji pamoja na Jamhuri umeshindwa kuithibitishia mahakama hiyo bila kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alitenda kosa.
Akifafanua zaidi hakimu huyo alisema kuwa mahakama iliridhika na upande wa utetezi ambao ulipelekwa vilelezo mbalimbali ikiwemo picha iliyomwoshesha mtuhumiwa akiwa juu ya kisima na kuthibitisha kuwa sio yeye aliyehusika kwenye tuhuma zilizofikishwa mahakani hapo.
Aliongeza kuwa, mahakama imeshindwa kumtia hatiani baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha fomu namba 3 ya Polisi (PF3) inayotolewa na ili kuwezesha mlalamikaji aweze kutibiwa.
Kwa mujibu wa hakimu huyo, mashahidi wa upande wa mashtaka walitofautiana katika kutoa maelezo, na hivyo baada ya mahakama kujirisha kuwa mshitakiwa hana hatia, imeamua kumwachia huru.
Mara baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Jivava ambaye alikuwa meneja kampeni wa mbunge wa Mbozi Magharibi, Dived Silinde katika uchaguzi mkuu wa 2010, alisema kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kisiasa kwa shinikizo ili afungwe.
“Kesi hiii ilifunguliwa kwa shinikizo na wala si kwa utashi wake huyu mama, lakini namshukuru Mungu kwa kunisaidia na kumuongoza hakimu katika kutenda haki na hatimaye nikashinda,” alisema Jivava.
Chanzo;Tanzania Daima

BRELA YAWAFUNDA WAFANYABIASHARA SONGEA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Brela yawafunda wafanyabiashara Songea
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (Brela) imeendelea kuwasisitiza wafanyabiashara kujitokeza kusajili majina ya biashara zao, ili ziweze kurasimishwa.
Akizungumza kwenye semina ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara mjini hapa juu ya umuhimu wa kusajili majina ya biashara zao, Msajili Msaidizi wa Brela, Seka Kasera, alisema wakisarasimisha biasha zao kunaisaidia serikali kuwatambua katika mikoa husika.
“Ni muhimu kwa wafanyabiashara kusajili, ili kutoa wigo mpana kwa serikali kuweka mipango yake ikiwa ni pamoja na suala nzima la ukusanyaji wa kodi,” alisema Kasera.
Alisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia wafanyabiashara hao kuweza kupata mikopo kwa urahisi katika taasisi mbalimbali za kibenki ambazo zimekuwa hazina imani kwa kiasi kikubwa na watu ambao hawajasajili biashara zao.
Kasera alisema mafunzo ambayo Brela imekuwa ikiyatoa kwa wafanyabiashara yamewasidia kuwajengea uwezo na kutambua umuhimu wa kusajili majina ya biashara.
chanzo:Tanzania Daima

MSAADAI UNAHITAJIKA ILI KUOKOA UHAI WA MTOTO HUYU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mtoto  Zabibu Salum Abdalah
---------------
Na Steven Augustino wa demasho.com, Tunduru.
MZAZI wa mtoto wa miezi sita Zabibu Salum Abdalah ,ambaye kichwa chake kina kuwa kikubwa kila siku tangu azaliwe ameomba msaada wa fedha ili kufanikisha kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.

Mama mzazi wa Mtoto Bi. Zainabu Mustafa Rajab,alisema kuwa Binti yake huyo alizaliwa April 24 mwaka huu katika hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Tunduru,na kwambatatizo hilo la kuanza kukua kwa kichwa chake lilianza kujitokeza mwezi mmoja baadaye.

Alisem abaada ya tukio hilo,walianza kuhangaika kutafutamatibabu katika hospitali mbalimbali ,lakini hadi leo juhudi zao zimegongamwamba ,baada ya kuandikiwa barua ya Rufaa inayowata kakumpeleka kijana wao huyo katika Hospitali ya TaifaMuhimbili.
Alisema kutokana na wanafamilia hao kutokuwa na uwezo kifedha taarifa hiyo imewakatisha tamaa ya kuokoa maisha ya kijana wao huyo hali ambayo imewafanya kuwaangukia Watanzania wenzao,ili kuomba msaada huo utakao jumuisha nauli ya kutoka Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma kwenda Jijini Dar es Salaam, pamoja na gharama za matibabu.

Bi Zainabu aliendelea kufafanua kuwa baada ya kuandikiwa barua hiyo ,yeye na mzazi mwenzie , walienda katika ofisi ya MkuuwaWilaya , ilikuomba msaada la kini waliambulia kupewa barua ya utambulisho wa kuwaomba msaada wananchi mjini humo, 
 Lakini hadi sasa hakuna msaada wowote walioupata kupitia mfumo huo wa barua.

Alisema kwa mtu atakaye guswa na tukio hilo anaweza kutuma msaada wake kwa kutumia Simu na mba 0685179479 ya animtandao wa Airtel money.
Akizungumzia tukio hilo ,Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya yaTunduru Dr. Alex Kazula, pamoja na kuthibitisha kuwepo kwa tukio la mgonjwa huyo, alisema kuwa Hospitali yake imechukuwa uamuziwa kumpatia Rufaa hiyo, baada ya maafisa tabibu waliopo Hospitalini hapo kutokuwa na ujuzi wakutibu maradhi hayo.

MAKAMANDA VIJANA KATA WATAKIWA KUWA WABUNIFU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KAMANDA wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Kalambo, Rosweeter Kasikila amewataka viongozi walioteuliwa hivi karibuni kuwa makamanda wa vijana ngazi za kata kuwa wabunifu kwa  kuandaa mazingira mazuri kiuchumi yatakayowezesha kuundwa kwa vikundi vya vijana wajasiriamali.
Amesema, kwa kufanya hivyo ni njia moja ya mbinu za kukabiliana na umaskini na kujiepusha na vitendo vya uhalifu.
Akizungumza na vijana wa CCM Kata ya Matai kwenye mji mdogo wa Matai makao makuu ya wilaya ya Kalambo baada ya kukamilika zoezi la kuwasimika makamanda wa kata 17, alisema makamanda hao wana wajibu wa kuwahudumia vijana katika kata zao bila kujali itikadi zao za  vyama vya siasa na kuwahamasisha juu ya elimu ya kujitegemea.
Kasikila, alisema uamuzi huo wa kuwateua makamanda hao katika ngazi za kata, unalenga kukabiliana na wimbi la vijana wengi wanaohitimu elimu katika shule za Msingi na Sekondari kukosa fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu na kujikuta wanajihusisha katika vitendo mbalimbali vya uhalifu.
Kasikila ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu mkoani Rukwa, alisema changamoto inayowakabili vijana hivi sasa ni jinsi ya kupata mitaji ya kuanzisha miradi ya kiuchumi, kutokana na kukosa umoja utakaowawezesha kuaminika na vyombo mbalimbali vya fedha na hata halmashauri za Wilaya ambazo zina utaratibu wa kuvisaidia vikundi vya vijana na wanawake.


Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kalambo, Credo Mpondela, alisema alipewa jukumu hilo la kuwapa mamlaka hayo ya kichama ili kujenga fikra za kuajiriwa miongoni mwa vijana na kuwawezesha kujipanga kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ambavyo itakuwa rahisi kwao kukopesheka.
Chanzo:Tanzania Daima

LAPF YATAKA UHURU KWA WATUMISHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
LAPF yataka uhuru kwa watumishi
MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), umewataka waajiri kuacha tabia ya kuwalazimisha watumishi wao kujiunga na mifuko mingine badala yake watekeleza sheria namba 8 ya mwaka 2008, kifungu namba 30 kinachotoa uhuru kwa waajiriwa kuchagua mfuko wanaoutaka.
Wito huo ulitolewa na Meneja wa LAPF kanda ya Kaskazini, Rajabu Kinande wakati akitoa mafunzo kwa watumishi wa idara mbalimbali wa halmashauri hiyo ambao ni wanachama wa mfuko huo.
Alisema kuwa waajiri watende haki kwa kuwaacha wananchama waamue sehemu ya kwenda kujiunga kwani mifuko ya kijamii sio maadui, hivyo kila mtumishi anayo haki ya kuchagua mfuko anaotaka kujiunga nao.
Kinande alifafanua kuwa, lengo la mafunzo hayo kwa wananchama wake ni kutoa elimu kwani wamegundua kuwa kuna baadhi ya wanachama hawafahamu vizuri juu ya mfuko huo.
Kwamba, wanataka pia kujua wanachama wao wana maoni gani pamoja na kero zao ili waweze kuzifanyia kazi na kuboresha huduma za LAPF kwa lengo la kuleta tija.
Baadhi ya wanachama wa mfuko huo, walipongeza hatua hiyo ya kupatiwa elimu mara kwa mara tofauti na mifuko mingine ya kijamii, kwamba hawana mashaka kutokana na elimu wanayoipata juu ya mikopo na mafao yao.
Chanzo:Tanzania daima

WAPINZANI WAKIMDHARAU KINANA, CCM ITASHINDA KIRAHISI 2015

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), amekamilisha awamu nyingine ya ziara zake mikoani. Katika awamu hii, alitumia siku 28 kutembelea mikoa ya Pwani, Tanga na Iringa.
Wapo ambao wanazibeza ziara hizi kwa sababu za kisiasa, lakini kwa wanaozifuatilia kwa karibu, wameshagundua kuwa zitakuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa CCM katika uchaguzi ziku za usoni.
Kuna mambo mengi ambayo Kinana na timu yake wanayafanya katika ziara hizo ambayo yanarudisha imani ya wananchi kwa CCM.
Siyo siri kuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, wananchi wengi walianza kupoteza imani na chama tawala kwa sababu mbalimbali, kubwa ikiwa chama hicho kushindwa kutekeleza kile inachokiahidi.
Hata Kinana anakiri katika hotuba zake kwenye ziara kuwa ni kweli CCM ilipoteza mwelekeo kidogo katika miaka ya hivi karibuni.
Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kinana anasema ni kweli chama hicho kiliingia mushkeli.
“Moja kati ya madhumuni ya ziara zangu mikoani ni kukagua uhai wa chama na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi… hapa katikati CCM iliacha kufanya yale yanayostahili kufanywa na chama tawala,” anasema.
Hata hivyo, Kinana haishii kukagua utekelezaji wa ilani tu.
Pale anapobaini makosa husema waziwazi na huwa hamwonei mtu yeyote aibu.
Anawakosoa kuanzia viongozi wa CCM wenyewe na watendaji katika halmashauri za wilaya au hata serikali kuu pale anapobaini wametenda makosa.
Ndiyo maana mara nyingi katika hotuba zake, ukimsikiliza Kinana wakati anahutubia, unaweza kudhani anayezungumza ni mpinzani.
Ile lugha ya kuwasema viongozi wa Serikali na CCM ambayo kwa miaka mingi imezoeleka kutoka kwenye vinywa vya wanasiasa wa upinzani, sasa inatolewa na Kinana, tena si kwa kificho, bali kwenye mikutano ya hadhara
Hilo linaanza kuwafanya baadhi ya watu kuona kuwa kumbe hata CCM inaweza kupingana na makosa makubwa serikalini kama vile rushwa, uzembe, umangimeza na hata ufisadi.

Msimamo wa Kinana
Akizungumza na katika ziara yake, Kinana anasema kazi ya kuikosoa Serikali iliyopo madarakani inapaswa kufanywa na viongozi wa CCM kwa sababu Serikali hiyo imewekwa na chama hicho ili kutekeleza mkataba baina ya CCM na wananchi.
Jambo jingine ambalo liliwafanya watu waanze kupoteza imani na CCM ni kitendo chake cha kukumbatia watu wa tabaka la juu.
Wafanyabiashara na watu wenye madaraka serikalini au kwenye chama walionekana kuwa ni bora zaidi kuliko wakulima na wafanyakazi ambao ndiyo msingi mkuu wa uanachama wa CCM.
Katika ziara zake, Kinana anajitahidi kufika maeneo ambako anakutana na watu wa kawaida moja kwa moja. Wala hakuna urasimu kwa watu kuzungumza naye.

Mbinu anazotumia
Mwenyewe amekuwa na utamaduni wa kuwaruhusu watu wa kawaida kuuliza maswali katika mikutano ya hadhara. Kinana anasema hapendi kuendelea na mtindo wa viongozi ambao kazi yao ni kuwahutubia tu wananchi.
“Wakati mwingine unaweza kutoa hotuba ndefu sana lakini isiyogusa masilahi ya wananchi unaowahutubia. Watu wanaweza kukushangilia lakini baadaye wanakuponda kwa sababu hukusema mambo yanayowahusu,” anasema.
Wananchi ambao wanapata nafasi ya kuuliza maswali katika mikutano ya Kinana, huwa wanajisikia furaha kwa kupata fursa ya kuzungumza na kiongozi mkubwa moja kwa moja
Wengi wanawataka viongozi wengine kuiga utamaduni huo kwa sababu unawapa furaha na fursa ya kuibua masuala mengi ya msingi yanayowasumbua.
Mtindo huu wa maswali ya papo kwa hapo unageuka kuwa kama mahakama ya wazi kwani wananchi wanaweza si tu kueleza matatizo yao, bali pia kuwasema na wakati mwingine kuwachukulia hatua viongozi wao ambao hawawajibiki.

athalan, katika mkutano uliofanyika katika eneo la Mponde katika Jimbo la Bumbuli, wananchi walimfukuza kutoka kwenye mkutano huo wa hadhara diwani wao, RichardMbuguni kwa maelezo kuwa amekuwa akiwasaliti katika kushughulikia matatizo ya kiwanda cha chai kilichofungwa tangu Mei mwaka huu.

Anavyojichanganya na wananchi
Pamoja na kuwaruhusu watu kuuliza maswali moja kwa moja, pia Kinana amekuwa akishiriki shughuli na wananchi. Mara kadhaa amethubutu kufanya mambo ambayo viongozi wengine wakuu wa chama au Serikali hawawezi kuyafanya.
Wakati mwingine, Kinana aliamua kutumia usafiri wa boti za kawaida alipotembelea Kisiwa cha Mafia. Ingawa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani ilimuonya kuwa usafiri huo si salama, lakini Kinana aliamua kuutumia.
Alipotakiwa aeleze kwa nini ameamua kufanya hivyo, alisema: “Kama wananchi wanautumia usafiri huu kila siku, kwa nini mimi nisiutumie?
“Kama kiongozi sitautumia usafiri huu, hivi nitawezaje kufahamu kwa undani matatizo yanayowakabili wananchi wanaoutumia usafiri wa aina hii?
Kusafiri kwangu kwa boti kumenifanya nijue matatizo yake kwa undani hivyo inakuwa rahisi zaidi pale mnapoamua kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo.”
Alipokuwa katika Kijiji cha Mlola, Lushoto, mkazi mmoja alimtaka aende kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuwa wananchi wa huko wanamtaka awatembelee.
“Mimi hapa ni mzee sana lakini ukiniuliza nikuelezee viongozi naweza kumwelezea (Mwalimu Julius) Nyerere pekee kwa sababu ndiye kiongozi wa juu niliyewahi kumuona.
Hawa wengine nawasikia kwenye vyombo vyahabari tu,” alisema mzee mmoja wakati alipopatiwa nafasi ya kuuliza swali kwenye mkutano wa hadhara.
Mzee huyo alimpongeza Kinana kwa kupita kwenye barabara yenye milima, mabonde na kona nyingi ili kufika kijijini hapo.
Katika ziara zake mikoani, Kinana hutembelea kila jimbo la uchaguzi ambako mbali na mikutano ya hadhara, pia hufanya mikutano ya ndani na viongozi wa CCM na kwa kiasi kikubwa, huangalia matatizo ya chama hicho na kupanga mikakati ya kukabiliana nayo.
Haya ni baadhi ya mambo ambayo Kinana anayafanya na kwa mujibu wa tathimini ya CCM, yanasaidia kurejesha imani ya wananchi ambao walianza kukiona kimewageuka.
Jambo moja ni dhahiri kuwa ingawa ziara hizi za Kinana haziwezi kuwa silaha pekee kwa CCM, lakini zina mchango mkubwa katika kukirejesha mioyoni mwa wale wanaomini kuwa kipo kwa ajili ya kuwatetea wanyonge.

Elimu ya awali Tunduru na changamoto zake‏

Mwalimu wa darasa la awali wa Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi (kulia) akiwa na wanafunzi wake eneo ambalo hutumika kama darasa la wanafunzi hao. Mwalimu wa darasa la awali wa Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi (kulia) akiwa na wanafunzi wake eneo ambalo hutumika kama darasa la wanafunzi hao. WADAU wa elimu nchini Tanzania wanaamini kwa kiasi kikubwa kwamba endapo elimu ya awali (chekechea) nchini Tanzania itatolewa katika misingi inayostahiki itakuwa ni njia moja wapo madhubuti ya kuimarisha ubora wa elimu. Hii ndiyo maana wanaendelea kupaza sauti wakiitaka serikali kupitia vyombo husika kuboresha kwanza elimu ya awali kabla ya kupanda ngazi nyingine za juu. Huenda kilio hiki cha wadau wa elimu kimeanza kusikika serikalini. Kwani tayari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliagiza tangu mwaka 2010 kuwa kila shule zake za msingi ni lazima lianzishwe darasa la awali ili kuwenza kuwaandaa wanafunzi kuingia na darasa la kwanza. Awali elimu hii ilikuwa ikitolewa kwa kiasi kikubwa na taasisi na vikundi mbalimbali na hata watu binafsi nje ya shule za msingi, tena kwa hiyari. Kwa sasa sera na miongozo ya elimu inatamka wazi kuwa nilazima kila shule ya msingi iwe na darasa la awali kwa ajili ya elimu hiyo muhimu. Changamoto kubwa iliyoibuka kwa sasa baada ya utekelezaji wa agizo hilo ni namna elimu hiyo inavyoendeshwa kwa kusuasua kwenye baadhi ya shule za Serikali. Hivi karibuni mwandishi wa makala haya alitembelea baadhi ya shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kuangalia hali ya utekelezaji wa zoezi hilo. Uchunguzi ulibaini zipo shule ambazo licha ya kusajili wanafunzi wa awali kila mwaka hazina madarasa ya kusomea kwa watoto hao, hali ambayo inafanya wanafunzi hao wadogo kufundishwa katika mazingira magumu na kudhohofisha lengo zima la utoaji wa elimu hiyo. Wapo wanafunzi ambao hulazimika kufundishiwa nje, yaani chini ya mti ama kwenye magofu (majengo ya shule ambayo hayajakamilika) iwe madarasa au nyumba za walimu. Teckla Milanzi ni mwalimu wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya. Anasema kimsingi wanafunzi wa darasa la awali shuleni hapo wanasomea chini ya mti kwa kuwa hawana darasa maalum kwa wanafunzi hao. Anasema wakati wa mvua ama jua kali mara nyingine hulazimika kuhairisha masomo kwa siku kutokana na hali ya hewa. Baadhi ya wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko wakiwa darasani kama walivykutwa na mwandishi wa makala haya hivi karibuni. Baadhi ya wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko wakiwa darasani kama walivykutwa na mwandishi wa makala haya hivi karibuni.[/caption] Anasema anashukuru kwa sasa wanajihifadhi kwenye jengo moja ambalo linaendelea na ujenzi shuleni hapo, jengo ambalo hata hivyo mara baada ya ujenzi kukamilika na wahusika kukabidhiwa darasa watarudi kusomea chini ya mti kama ilivyo ada. Hata hivyo, anasema licha ya changamoto hiyo darasa hilo halina vitabu kwa ajili ya kufundishia wanafunzi, bali kuna nakala moja moja kwa baadhi ya masomo ambavyo vilitafutwa kwa jitihada za mwalimu mwenyewe. “Mfano kwa vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Hisabati kuna nakala moja moja tu, ambazo hutumiwa na mwalimu mwenyewe. Anasema darasa hilo licha ya kuwa na changamoto kedekede hata kwenye mgao wa fedha zinazoletwa shuleni kila mara halimo hivyo hakuna kinacholetwa tofauti na wanafunzi wengine,” anasema Bi. Teckla Milanzi. Kwa upande wake, Mwalimu Christina Komba wa darasa la awali Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko anasema madarasa ya elimu ya awali Wilayani Tunduru yanakabiliwa na changamoto nyingi. Anabainisha kuwa madarasa mengi likiwemo lake hawana vitabu wala miongozo ya namna ya ufundishaji kabisa zaidi ya kila mwalimu anayefundisha kubuni nini afundishe kila uchao. “…Kwanza licha ya kutokuwa na vifaa vingine hatuna chumba maalumu cha wanafunzi hawa (darasa) kwa sasa tunatumia jengo la darasa ambalo bado linaendelea na ujenzi na hata hivyo jengo hili halijengwi kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” anasema mwalimu Christina Komba. Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya, wakiwa katika darasa lao. Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya, wakiwa katika darasa lao.[/caption] “Madarasa ya elimu ya awali hayana vitabu, hayana miongozo…huwa tunaanzima au ukipata hela yako wewe binafsi unaenda kununua kitabu kimoja au viwili ili uweze kuwasaidia watoto. Na baadhi ya masomo hayana vitabu kabisa hata ukienda madukani katika Wilaya yetu (Wilaya ya Tunduru) vitabu kama Haiba na Michezo, pamoja na Sanaa hazipo kabisa madukani. Anasema uongozi wa juu wilayani unalitambua hilo. Batadhari Mkwela ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka anasema usajili wa wanafunzi wa awali kila mwaka huongezeka japokuwa bajeti ya kuendesha elimu hiyo ni changamoto. “…Darasa la awali linahitaji vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha, vyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini, hatuna madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” anasema Mkuu huyo wa Shule ya Nanjoka. Hadija Makamla ni mwalimu wa darasa la awali Shule ya Msingi Majengo. Mwalimu huyu ambaye amehitimu kozi ya kufundisha darasa hilo, anasema anavyo baadhi tu ya vitabu vinavyoitajika katika darasa hilo. Anabainisha kuwa darasa hilo lina jumla ya wanafunzi 48 lakini hutumia darasa la wanafunzi wa kawaida maana hawana darasa lililojengwa maalum kwa wanafunzi wa awali. “…Ninazo nakala chache kwa ajili ya mwalimu tu ila wanafunzi hawana hata kimoja…lakini kuna masomo mengine sina vitabu kabisa kama vile Sanaa na Haiba ya Michezo sina kabisa hata mimi,” anasema mwalimu Makamla. “…Unajua watoto kwa kiasi kikubwa wanajifunza kwa vitendo, picha na uhalisia, sasa huenda tunavyowapa ni vikubwa zaidi au vidogo sana kwa sababu ya kubuni mada kwa baadhi ya masomo. Dorothea George ni mwalimu wa darasa la awali shule ya Msingi Nanjoka Wilayani Tunduru. Yeye anasema japokuwa hakuwahi kufanya kozi ya ualimu wa awali kwa sasa amekabidhiwa darasa hilo kulifundisha katika shule yake. Anasema darasa hilo kwa sasa lina wanafunzi 98 ambao wanasomea darasa moja chini ya mwalimu mmoja. Anasema licha ya darasa hilo kuwa na madawati kadhaa lakini si maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali bali ni ya wanafunzi wa kubwa, hata hivyo bado kuna watoto wanalazimika kukaa chini kwa kile kukosa madawati ya kutosha katika shule hiyo. Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Madina Mkali anasema uendeshaji wa darasa la awali shuleni hapo ni wa kusuasua kutokana na changamoto anuai zinazowakabili. Hakuna bajeti inayoingia kuisaidia elimu hiyo, ispokuwa mwaka huu waliletewa madawati kumi kwa ajili ya elimu ya awali. Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe akizungumza na mwandishi wa makala haya (hayupo pichani) ofisini kwake hivi karibuni. Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe akizungumza na mwandishi wa makala haya (hayupo pichani) ofisini kwake hivi karibuni “…Uendeshaji elimu ya awali hapa ni wa wastani kwa kweli kutokana na changamoto zinazotukabili, kwanza vifaa vya kuwafundishia watoto hawa ni tatizo na wazazi kwa eneo hili wamekuwa hawana mwamko wa elimu hii kabisa. Kwanza hawachangii michango ya chakula kama inavyotakiwa ili mtoto apate chochote awapo shuleni,” anasema mwalimu Mkali. Anabainisha kuwa watoto pia wanatakiwa kupata uji wawapo shuleni lakini uchangiaji kwa wazazi nao umekuwa tatizo kubwa. “…Wapo wanaochangia wengine wanagoma tunasukumana hivyo hivyo na mambo yanasonga mbele…lakini kutokana na uchangiaji duni kuna baadhi ya siku wanapata uji na sikunyingine hawanywi kutokana na ugumu wa michango,” anasema mwalimu George. Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko, Adam Hausi katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anasema uendeshaji wa elimu ya awali katika shule hiyo ni juhudi binafsi za mwalimu wa darasa hilo. Anasema darasa hilo halina bajeti yoyote kutoka serikalini hivyo hakuna vitabu na vitendea kazi vingine vinavyohitajika. “…Vitendea kazi ndio tatizo kabisa, ila mwalimu anafundisha kwa jitihada zake na darasa linaendelea. Alafu lina idadi kubwa sana ya wanafunzi (84) na anafundisha peke yake…,” anasema Hausi. Anasema uboreshaji elimu ya msingi ni suala la ushirikiano kati ya Serikali na jamii yenyewe lakini wakati mwingine Serikali inakwamisha juhudi hizo kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo baadhi ya maeneo. “…Mfano sisi tulijenga madarasa mawili kwa nguvu za wananchi hadi yamekamilika ilipofika suala kuezekwa tokaomba msaada wa Serikali pamoja na kumaliziwa ili yaanze kutumika ilikuwa kazi kweli tulizunguzwa sana hadi tukaanza kuyatumia hivyo hivyo,” alisema. Bi. Thabita Farara ni Mkazi wa Kata ya Mringoti Mashariki anasema bado mwamko wa elimu ya awali kwa wazazi ni mdogo, maana wazazi wengi wamekuwa wakijiandaa na darasa la kwanza tu kumuandikisha mtoto. Kwa upande wake Asha Komba Mkazi wa Tunduru Stendi anasema yeye anaitambua elimu ya awali na kuikubali lakini ni ile inayotolewa na shule binafsi kama za taasisi. Lakini ile inayotolewa kwenye shule za Serikali ni tatizo kubwa maana hazizingatii ubora wa elimu zaidi ya kuwalundika watoto tu darasani. “…Mimi naitambua elimu ya awali na watoto wangu wote wamepitia lakini huwa tunawapeleka kwenye chekechea za taasisi mbalimbali kama zinazomilikiwa na makanisa majeshi na zinginezo maana huku ndiyo kidogo mtoto anaandaliwa…kule Serikalini kwanza unakuta darasani wapo kibao alafu muda wote wanacheza tu si kujifunza,” anasema Bi. Komba. Abdul Kazembe ni Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, anasema kwa sasa kila shule ya msingi sera inaelekeza lazima iwe na darasa la awali. Anasema hata katika usajili wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa sasa watoto wa mwanzo kusajiliwa ni wale waliopata elimu ya awali katika shule husika. “…Kwa hiyo kuna umuhimu wa kila shule kuwa na darasa la awali…changamoto sasa inakuja kwenye vitendea kazi, kwa mwaka 2013 na kurudi nyuma uwepo wa ‘capitation’ ulikuwa pia unaelekeza watoto wa awali wapo mule na hata tunapotoa takwimu za awali tulianza na ‘pre-primary’ (wanafunzi wa awali) hivyo wenyewe wapo, tatizo hapa ni ujaji wa pesa yenyewe ya ‘capitation’ haitimii kama inavyo elekeza, yaani ile wastani ya kwamba kila mtoto apate shilingi 10,000 kwa mwaka hautimii,” anasema. Anatolea mfano mwaka 2013/14 kiwango cha fedha ambacho kilitakiwa kuja katika halmashauri ya wilaya hiyo ni zaidi ya milioni 366.7. Kiwango hiki ni kile kilichoidhinishwa katika bajeti tu lakini ukirudi kwenye mahitaji halisi ni zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa. Anasema kilichokuja ni zaidi ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu ya kiasi kilichopitishwa kwenye bajeti. Anabainisha hilo ndilo tatizo kubwa kwani hata fedha ambazo zimepitishwa haziji kama ilivyopitishwa kwenye bajeti. “…Kwa hiyo unaweza kuona kwamba ni ngumu kuigawa fedha hii katika matumizi maana kwanza haitoshi na pili hata kilichotegemewa kuja ni pungufu zaidi tena sana, sasa sijui unaweza kugawa kila shule ipate shilingi ngapi…kwani haitoshelezi,” anasema. Anasema kwa upande mwingine miundombinu ya madarasa ni changamoto kubwa. Kwa mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa wilaya nzima ilikuwa ni 1,715 lakini ukiangalia vyumba vya madarasa vilivyopo ni kama 900 na kitu na mengine ni ya muda mrefu sana kiasi ambacho yanaelekea kuchakaa jambo ambalo pia yanapungua. Aidha anaeleza kuwa ukienda kwenye bajeti ya ujenzi wa madarasa mapya milioni 171 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na miundombinu mbalimbali kiasi hiki cha fedha waweza kuta kinauwezo wa kujenga madarasa kama nane tu. Kiasi hicho cha fedha ni pamoja na ujenzi wa nyumba tano za walimu. Na kiasi hicho cha fedha za ujenzi ni pamoja na kumalizia miradi viporo za nyumba za walimu na vyumba vya madarasa. Anasema upungufu wa vyumba vya madarasa eneo hilo ni karibia madarasa 800. “Sasa kwa ujumla unaweza kuona kuwa miundombinu pale shuleni haitoshelezi, ni jambo la kawaida kuona walimu wakiacha ofisi itumike kama darasa au darasa litumike kama ofisi. Huku kwa awali ni changamoto zaidi maana licha ya upungufu wa vyumba hata wazazi hasa vijijini wanashindwa kuchangia chakula (uji) kwa watoto wao unaweza kukuta wameandikishwa wengi Januari lakini kila muda unavyozidi kwenda watoto wanapungua na unaweza kukuta hadi mwezi Juni darasa linapotea kabisa kwa utoro,” anasema. Kazembe anabainisha kuwa kuna jumla ya shule za msingi 144 katika wilaya hiyo, huku shule zilizo na vyumba maalumu vya madarasa ya awali zikiwa 16 tu. Anasema shule nyingine zote hazina vyumba vya madarasa ya awali na matokeo yake ama wanatumia madarasa ya msingi kwa kupishana. Anaongeza kuwa uhamasishaji wa ujenzi wa madarasa ya awali na umuhimu wa elimu hiyo unatolewa kwa walimu, wazazi na kamati za shule kupitia vikao mbalimbali ambapo mara nyingi uongozi uhimiza wazazi kuchangia zaidi nguvu zao katika kukamilisha ujenzi wa madarasa ya awali, utengenezaji wa madawati na upatikanaji wa chakula cha mchana na uji shuleni. “…lakini tunaangalia sana chakula maana watoto hata kwenye mti wanaweza kukaa wakasoma endapo wanamadawati pale au wamekaa chini kwenye kivuli, japokuwa si mazingira mazuri sana shuleni…lakini wakiwa na chakula hata utoro unapungua,” anasema. Anasema kwa mwaka 2013 serikali ilikumbuka kuleta fedha kwa ajili ya ununuzi madawati ya wanafunzi wa awali, fedha ambazo tulizigawa na kununua baadhi ya vitabu vya awali na madawati kwenye shule ambazo zinamadarasa hai ya awali. Shule zilizonufaika na mgao huo ni shule za mjini Tunduru tu ambazo nyingi ndizo zenye madarasa hai ya awali. Anasema ili kukabiliana na hali ya upungufu wa walimu wa awali; imepitishwa walimu wa gredi ‘A’ kufundisha madarasa hayo kwa kuwa wao mafunzo yao katika kozi hujumuisha ufundishaji darasa la awali, tangu walioitimu mwaka 2013. “…sasa wakati mwingine unaweza kukuta mwalimu ni gradi A na kimsingi yeye anao uwezo wa kufundisha darasa la awali, lakini wengine hawakubali hadi aone ana cheti kabisa maalumu cha kufundisha darasa la awali…ukimuuliza huyu atakwambia yeye hana taaluma ya kufundisha awali jambo ambalo si sawa,” anasema Ofisa Elimu huyo wa Msingi. “..Kwa suala la vitabu kweli hii ni changamoto, hapo nyuma tulikuwa tunanunua vitabu wenyewe wakini kwa sasa TAMISEMI wenyewe moja kwa moja wananunua na kuvileta. Sasa huku kwetu ni nadra sana kuona wazabuni wetu wanaleta vitabu vya awali kwa sababu soko lake ni dogo sana kutokana na idadi ndogo ya uwepo wa elimu hii ya awali eneo husika,” anasema. Hata hivyo umeona unafuu maeneo ya mjini mzazi anatambua umuhimu wa elimu hivyo anaweza kuchonga dawati kwa ajili ya mtoto wake lakini kwa vijijini hali ni mbaya zaidi. Mzazi ukimwambia achangie dawati anakushangaa na pia haoni umuhimu huo. “…Nikwambie unajua Wilaya ya Tunduru mzazi mtoto wake akifeli anafurahi sana…tena baadhi wanaona kama ni sherehe, kwanza wakifanya mtihani tu wa la saba barabarani akina mama wanashangilia wanaona wametua mzigo, unaweza kujiuliza wazazi wanaoshangilia inamaana walikuwa wakiona ni adhabu watoto wao kuwa shule? Lakini pia mtoto akisha faulu kwenda shule hapelekwi hadi DC aunde kamati, atembee na hakimu na polisi kukamata wazazi wanaogoma kusomesha watoto watishiwe ndo wanakubali kusomesha…lakini kitendo cha wazazi kukamatwa kushikiliwa kwa kushindwa kuwapeleka watoto shule wamegeuka na kuwarubuni watoto wao wasifaulu,” anasema. Anabainisha kuwa ni kweli Serikali ina jukumu la elimu, lakini mzazi kwa upande wake anajukumu zaidi, kuangalia mtoto wake anapata elimu gani na ya kiwango gani na kama mzazi hayupo tayari basi haiwezekani na wakati mwingine inakuwa ngumu. Kimsingi jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia watoto wa awali zipo, lakini upatikanaji wa fedha ndio. Salum Mtutula ni Mbunge wa Tunduru Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge huyu katika mahojiano anakiri kuwa elimu ya awali ni muhimu na msingi mzuri wa mtoto kielimu. Anasema mtoto anapopata elimu nzuri ya awali huwa na msingi mzuri kielimu katika masomo yake ya mbele. “…Ili mtoto apate elimu bora ni lazima apate elimu ya awali inayostahiki…hakiwa na msingi mbaya wa elimu ya awali kuna uwezekano mkubwa way eye kufanya vibaya pia,” anasema Mtutula. Hata hivyo anaishauri Serikali kuingiza suala hili katika sheria na kanuni zake kuwa kila shule ya msingi inapoanzishwa ianze na darasa la awali kwanza ndipo madarasa mengine yafuate. “…Mimi nitafurahi kama suala hili tutaliweka kwenye sheria au kanuni zetu kuwa kila shule ya msingi inapoanzishwa basi lazima ianze na darasa la awali ndipo madarasa mengine yafuate iwe shule za Serikali au binafsi,” anasema Mbunge Mtutula. *Imeandaliwa na: www.thehabari.com  

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WATUHUMIWA WIZI WA PIKIPIKI WAUAWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WATU wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi wameuwawa na wananchi wenye hasira baada ya kutaka kupora pikipiki mbili walizokuwa nao madereva wa bodaboda, mtaa wa Mahilo kata ya Matogoro Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alithibitisha kutokea kwa mauaji ya watu hao juzi saa 3 usiku na kusema majina ya marehemu hao hayakufahamika mara moja.
Kamanda Msikhela alisema siku ya tukio Furko Alfonsi (24) dereva wa pikipiki yenye namba za usajili T.558 CJJ na Vasco Dagama (21) ambaye ni fundi na dereva wa pikipiki yenye namba za usajili T.363 BPL walioporwa pikipiki hizo kwa muda tofauti.
Alisema waliporwa pikipiki hizo baada ya kuwekewa kizuizi cha kamba ya manila iliyofungwa kwenye miti miwili mikubwa pembezoni mwa barabara.
Kamanda huyo alidai kwamba waporaji wanakadiriwa kuwa watano, walikuwa na silaha za jadi ambazo ni mapanga, nondo na kamaba za Manila ambao walijipanga kando ya barabara wakiwa na matawi ya miti yalitumika kuwapiga usoni waendesha pikipiki hao.
Alisema baada ya majambazi hayo kugundua kuwa Furko amepoteza fahamu na baadae walidhani amekufa walimbeba na kumtupa korongoni kisha waliendelea na uporaji wao ambapo walimzuia Vasco ambaye naye alishushiwa kipigo na kutoroka wakiwa na pikipiki hizo.
Kwa mujibu wa kamanda huyo Furko alipata fahamu baadaye na kujivuta hadi kwenye makazi ya watu na kuwajulisha yaliyojiri ndipo wananchi hao walipojikusanya kwa lengo la kuwasaka watuhumiwa hao kwa kuweka kizuizi kwenye barabara ya kutoka Mahilo kwenda  Songea mjini ghafla watuhumiwa wakiendesha pikipiki hizo huku wamemebana walisimamishwa na wanachi hao kabla ya kushushiwa kipigo ambapo watatu kati yao walitokomea kusikojulikana.
Alisema kuwa majambazi hao wawili walifariki dunia njiani wakati wanakimbizwa kwenda kwenye hospitali mkoa ya Songea na maiti zao zimehifadhiwa hapo huku wananchi wakitakiwa kwenda kuzitambua.
Chanzo:Tanzania Daima

WALIODHURIKA KWA TOGWA SONGEA SASA WAFIKIA WATU 340

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Idadi ya watu waliolazwa hospitalini kwa kunywa togwa inayosadikiwa kuwa na sumu katika Kijiji cha Litapwasi, Kata ya Mpitimbi mkoani Ruvuma imeongezeka kutoka 270 hadi 340.
Tukio hilo lilitokea Jumapili baada ya watu kushiriki sherehe ya Kipaimara ambako walikula, kunywa pombe na togwa na baadaye wale waliokunywa togwa walianza kuumwa matumbo, kuhara na kutapika.
Hadi jana, watu 102 walikuwa bado wamelazwa katika Zahanati ya Lyangweni, Hospitali ya St. Joseph Peramiho na Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.
Tayari watu watano wanashikiliwa na Polisi kwa upelelezi kuhusiana na tukio hilo, akiwamo Baba Mzazi wa mtoto Dickson aliyepata kipaimara, Enes Nungu (47).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Mskhiela aliwataja watu wengine wanaoshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Songea kwa mahojiano kuwa ni Benedict Nungu (76), Esebius Komba (36), Sadiki Masodi (65) na John Kaulangudidi. Mtu anayedaiwa kukabidhiwa ufunguo chumba cha vinywaji kabla ya kugawiwa kwa wananchi, Ridhiwani Shawa haijulikani alipo.
Mabaki ya chakula, togwa na pombe ya kienyeji vilichukuliwa juzi na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Kamanda Mskhiela alitoa wito kwa wananchi wanaoandaa sherehe kuhakikisha wanafanya hivyo katika mazingira mazuri na yenye usalama ili kuepuka athari kama hizo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Peramiho, Dk Vanace Mushi alisema hadi jana, watu waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo walikuwa 34 na hakukuwa na mgonjwa aliyeruhusiwa kurudi nyumbani.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Majuto Mlawa alisema wagonjwa tisa wa rufaa walipokewa na kupatiwa matibabu huku hali zao zikiwa mbaya.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema: “Jambo hili limenisikitisha sana, nimeumizwa sana nawapa pole wote waliopatwa na tatizo hilo naamini Mwenyezi Mungu atawasaidia na watapona na kurejea katika hali zao za kawaida.”
Hata hivyo, Mwambungu alisema hiyo ni ajali kama nyingine, hivyo anaviachia vyombo vya usalama na wataalamu wa afya kupata ukweli. Pia aliwataka wananchi kuwa makini pindi wanapoandaa vyakula na pombe za kienyeji katika sherehe mbalimbali
Chanzo:Mwananchi
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa