Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAMANDA wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Kalambo, Rosweeter Kasikila amewataka viongozi walioteuliwa hivi karibuni kuwa makamanda wa vijana ngazi za kata kuwa wabunifu kwa kuandaa mazingira mazuri kiuchumi yatakayowezesha kuundwa kwa vikundi vya vijana wajasiriamali.
Amesema, kwa kufanya hivyo ni njia moja ya mbinu za kukabiliana na umaskini na kujiepusha na vitendo vya uhalifu.
Akizungumza na vijana wa CCM Kata ya Matai kwenye mji mdogo wa Matai makao makuu ya wilaya ya Kalambo baada ya kukamilika zoezi la kuwasimika makamanda wa kata 17, alisema makamanda hao wana wajibu wa kuwahudumia vijana katika kata zao bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa na kuwahamasisha juu ya elimu ya kujitegemea.
Kasikila, alisema uamuzi huo wa kuwateua makamanda hao katika ngazi za kata, unalenga kukabiliana na wimbi la vijana wengi wanaohitimu elimu katika shule za Msingi na Sekondari kukosa fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu na kujikuta wanajihusisha katika vitendo mbalimbali vya uhalifu.
Kasikila ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu mkoani Rukwa, alisema changamoto inayowakabili vijana hivi sasa ni jinsi ya kupata mitaji ya kuanzisha miradi ya kiuchumi, kutokana na kukosa umoja utakaowawezesha kuaminika na vyombo mbalimbali vya fedha na hata halmashauri za Wilaya ambazo zina utaratibu wa kuvisaidia vikundi vya vijana na wanawake.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kalambo, Credo Mpondela, alisema alipewa jukumu hilo la kuwapa mamlaka hayo ya kichama ili kujenga fikra za kuajiriwa miongoni mwa vijana na kuwawezesha kujipanga kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ambavyo itakuwa rahisi kwao kukopesheka.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment