Home » » KIGOGO CHADEMA APANGUA KESI

KIGOGO CHADEMA APANGUA KESI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Mbozi, imemwachia huru Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Harode Langisa “Jivava”, baada ya kumkuta hana hatia katika kesi ya jinai iliyokuwa ikimkabili namba 326 ya mwaka jana.
Mjumbe huyo, alikuwa akikabiliwa na kesi ya jinai ambapo alidaiwa kufanya makosa mawili ya shambulio la mwili na kuharibu mali, kesi iliyofunguliwa dhidi yake na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salome Ngusa, Oktoba 10, mwaka jana.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Rahim Mushi alisema Jivava alifikishwa mahakani hapo Oktoba 16 mwaka jana akituhumiwa kumshambulia Salome Ngusa wakati akitokea kwenye mkutano wa hadhara wa CCM na kuharibu mali zake eneo la mwaka mjini Tunduma.
Hakimu Mushi alisema kuwa baada ya upande wa mlalamikaji kutoa ushahidi mahakani hapo, mtuhumiwa Jivava alionekana na kesi ya kujibu na hivyo kutakiwa alete utetezi wake.
Alisema kuwa baada ya mahakama kusikiliza pande zote mbili, ilibaini kuwa upande wa mlalamikaji pamoja na Jamhuri umeshindwa kuithibitishia mahakama hiyo bila kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alitenda kosa.
Akifafanua zaidi hakimu huyo alisema kuwa mahakama iliridhika na upande wa utetezi ambao ulipelekwa vilelezo mbalimbali ikiwemo picha iliyomwoshesha mtuhumiwa akiwa juu ya kisima na kuthibitisha kuwa sio yeye aliyehusika kwenye tuhuma zilizofikishwa mahakani hapo.
Aliongeza kuwa, mahakama imeshindwa kumtia hatiani baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha fomu namba 3 ya Polisi (PF3) inayotolewa na ili kuwezesha mlalamikaji aweze kutibiwa.
Kwa mujibu wa hakimu huyo, mashahidi wa upande wa mashtaka walitofautiana katika kutoa maelezo, na hivyo baada ya mahakama kujirisha kuwa mshitakiwa hana hatia, imeamua kumwachia huru.
Mara baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Jivava ambaye alikuwa meneja kampeni wa mbunge wa Mbozi Magharibi, Dived Silinde katika uchaguzi mkuu wa 2010, alisema kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kisiasa kwa shinikizo ili afungwe.
“Kesi hiii ilifunguliwa kwa shinikizo na wala si kwa utashi wake huyu mama, lakini namshukuru Mungu kwa kunisaidia na kumuongoza hakimu katika kutenda haki na hatimaye nikashinda,” alisema Jivava.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa