Mwalimu wa darasa la awali wa Shule ya Msingi Nakayaya, Teckla Milanzi
(kulia) akiwa na wanafunzi wake eneo ambalo hutumika kama darasa la
wanafunzi hao.
WADAU wa elimu nchini Tanzania wanaamini kwa kiasi kikubwa kwamba
endapo elimu ya awali (chekechea) nchini Tanzania itatolewa katika
misingi inayostahiki itakuwa ni njia moja wapo madhubuti ya kuimarisha
ubora wa elimu. Hii ndiyo maana wanaendelea kupaza sauti wakiitaka
serikali kupitia vyombo husika kuboresha kwanza elimu ya awali kabla ya
kupanda ngazi nyingine za juu.
Huenda kilio hiki cha wadau wa elimu kimeanza kusikika serikalini. Kwani
tayari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliagiza tangu mwaka 2010
kuwa kila shule zake za msingi ni lazima lianzishwe darasa la awali ili
kuwenza kuwaandaa wanafunzi kuingia na darasa la kwanza. Awali elimu hii
ilikuwa ikitolewa kwa kiasi kikubwa na taasisi na vikundi mbalimbali na
hata watu binafsi nje ya shule za msingi, tena kwa hiyari. Kwa sasa
sera na miongozo ya elimu inatamka wazi kuwa nilazima kila shule ya
msingi iwe na darasa la awali kwa ajili ya elimu hiyo muhimu.
Changamoto kubwa iliyoibuka kwa sasa baada ya utekelezaji wa agizo hilo
ni namna elimu hiyo inavyoendeshwa kwa kusuasua kwenye baadhi ya shule
za Serikali. Hivi karibuni mwandishi wa makala haya alitembelea baadhi
ya shule za msingi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
kuangalia hali ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Uchunguzi ulibaini zipo shule ambazo licha ya kusajili wanafunzi wa
awali kila mwaka hazina madarasa ya kusomea kwa watoto hao, hali ambayo
inafanya wanafunzi hao wadogo kufundishwa katika mazingira magumu na
kudhohofisha lengo zima la utoaji wa elimu hiyo. Wapo wanafunzi ambao
hulazimika kufundishiwa nje, yaani chini ya mti ama kwenye magofu
(majengo ya shule ambayo hayajakamilika) iwe madarasa au nyumba za
walimu.
Teckla Milanzi ni mwalimu wa darasa la awali, Shule ya Msingi Nakayaya.
Anasema kimsingi wanafunzi wa darasa la awali shuleni hapo wanasomea
chini ya mti kwa kuwa hawana darasa maalum kwa wanafunzi hao. Anasema
wakati wa mvua ama jua kali mara nyingine hulazimika kuhairisha masomo
kwa siku kutokana na hali ya hewa.
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Tunduru
Mchanganyiko wakiwa darasani kama walivykutwa na mwandishi wa makala
haya hivi karibuni.[/caption]
Anasema anashukuru kwa sasa wanajihifadhi kwenye jengo moja ambalo
linaendelea na ujenzi shuleni hapo, jengo ambalo hata hivyo mara baada
ya ujenzi kukamilika na wahusika kukabidhiwa darasa watarudi kusomea
chini ya mti kama ilivyo ada. Hata hivyo, anasema licha ya changamoto
hiyo darasa hilo halina vitabu kwa ajili ya kufundishia wanafunzi, bali
kuna nakala moja moja kwa baadhi ya masomo ambavyo vilitafutwa kwa
jitihada za mwalimu mwenyewe.
“Mfano kwa vitabu vya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Hisabati kuna
nakala moja moja tu, ambazo hutumiwa na mwalimu mwenyewe. Anasema darasa
hilo licha ya kuwa na changamoto kedekede hata kwenye mgao wa fedha
zinazoletwa shuleni kila mara halimo hivyo hakuna kinacholetwa tofauti
na wanafunzi wengine,” anasema Bi. Teckla Milanzi.
Kwa upande wake, Mwalimu Christina Komba wa darasa la awali Shule ya
Msingi Tunduru Mchanganyiko anasema madarasa ya elimu ya awali Wilayani
Tunduru yanakabiliwa na changamoto nyingi. Anabainisha kuwa madarasa
mengi likiwemo lake hawana vitabu wala miongozo ya namna ya ufundishaji
kabisa zaidi ya kila mwalimu anayefundisha kubuni nini afundishe kila
uchao.
“…Kwanza licha ya kutokuwa na vifaa vingine hatuna chumba maalumu cha
wanafunzi hawa (darasa) kwa sasa tunatumia jengo la darasa ambalo bado
linaendelea na ujenzi na hata hivyo jengo hili halijengwi kwa ajili ya
wanafunzi wa awali,” anasema mwalimu Christina Komba.
Wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya, wakiwa
katika darasa lao.[/caption]
“Madarasa ya elimu ya awali hayana vitabu, hayana miongozo…huwa
tunaanzima au ukipata hela yako wewe binafsi unaenda kununua kitabu
kimoja au viwili ili uweze kuwasaidia watoto. Na baadhi ya masomo hayana
vitabu kabisa hata ukienda madukani katika Wilaya yetu (Wilaya ya
Tunduru) vitabu kama Haiba na Michezo, pamoja na Sanaa hazipo kabisa
madukani. Anasema uongozi wa juu wilayani unalitambua hilo.
Batadhari Mkwela ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka anasema
usajili wa wanafunzi wa awali kila mwaka huongezeka japokuwa bajeti ya
kuendesha elimu hiyo ni changamoto. “…Darasa la awali linahitaji
vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya kutosha,
vyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka Serikalini,
hatuna madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” anasema Mkuu
huyo wa Shule ya Nanjoka.
Hadija Makamla ni mwalimu wa darasa la awali Shule ya Msingi Majengo.
Mwalimu huyu ambaye amehitimu kozi ya kufundisha darasa hilo, anasema
anavyo baadhi tu ya vitabu vinavyoitajika katika darasa hilo.
Anabainisha kuwa darasa hilo lina jumla ya wanafunzi 48 lakini hutumia
darasa la wanafunzi wa kawaida maana hawana darasa lililojengwa maalum
kwa wanafunzi wa awali.
“…Ninazo nakala chache kwa ajili ya mwalimu tu ila wanafunzi hawana hata
kimoja…lakini kuna masomo mengine sina vitabu kabisa kama vile Sanaa na
Haiba ya Michezo sina kabisa hata mimi,” anasema mwalimu Makamla.
“…Unajua watoto kwa kiasi kikubwa wanajifunza kwa vitendo, picha na
uhalisia, sasa huenda tunavyowapa ni vikubwa zaidi au vidogo sana kwa
sababu ya kubuni mada kwa baadhi ya masomo.
Dorothea George ni mwalimu wa darasa la awali shule ya Msingi Nanjoka
Wilayani Tunduru. Yeye anasema japokuwa hakuwahi kufanya kozi ya ualimu
wa awali kwa sasa amekabidhiwa darasa hilo kulifundisha katika shule
yake. Anasema darasa hilo kwa sasa lina wanafunzi 98 ambao wanasomea
darasa moja chini ya mwalimu mmoja.
Anasema licha ya darasa hilo kuwa na madawati kadhaa lakini si maalum
kwa ajili ya wanafunzi wa awali bali ni ya wanafunzi wa kubwa, hata
hivyo bado kuna watoto wanalazimika kukaa chini kwa kile kukosa madawati
ya kutosha katika shule hiyo. Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Majengo, Madina Mkali anasema uendeshaji wa darasa la awali
shuleni hapo ni wa kusuasua kutokana na changamoto anuai zinazowakabili.
Hakuna bajeti inayoingia kuisaidia elimu hiyo, ispokuwa mwaka huu
waliletewa madawati kumi kwa ajili ya elimu ya awali.
Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe akizungumza na
mwandishi wa makala haya (hayupo pichani) ofisini kwake hivi karibuni
“…Uendeshaji elimu ya awali hapa ni wa wastani kwa kweli kutokana na
changamoto zinazotukabili, kwanza vifaa vya kuwafundishia watoto hawa ni
tatizo na wazazi kwa eneo hili wamekuwa hawana mwamko wa elimu hii
kabisa. Kwanza hawachangii michango ya chakula kama inavyotakiwa ili
mtoto apate chochote awapo shuleni,” anasema mwalimu Mkali.
Anabainisha kuwa watoto pia wanatakiwa kupata uji wawapo shuleni lakini
uchangiaji kwa wazazi nao umekuwa tatizo kubwa. “…Wapo wanaochangia
wengine wanagoma tunasukumana hivyo hivyo na mambo yanasonga
mbele…lakini kutokana na uchangiaji duni kuna baadhi ya siku wanapata
uji na sikunyingine hawanywi kutokana na ugumu wa michango,” anasema
mwalimu George.
Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko, Adam Hausi
katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anasema uendeshaji wa
elimu ya awali katika shule hiyo ni juhudi binafsi za mwalimu wa darasa
hilo. Anasema darasa hilo halina bajeti yoyote kutoka serikalini hivyo
hakuna vitabu na vitendea kazi vingine vinavyohitajika.
“…Vitendea kazi ndio tatizo kabisa, ila mwalimu anafundisha kwa jitihada
zake na darasa linaendelea. Alafu lina idadi kubwa sana ya wanafunzi
(84) na anafundisha peke yake…,” anasema Hausi. Anasema uboreshaji elimu
ya msingi ni suala la ushirikiano kati ya Serikali na jamii yenyewe
lakini wakati mwingine Serikali inakwamisha juhudi hizo kwa kushindwa
kuwajibika ipasavyo baadhi ya maeneo.
“…Mfano sisi tulijenga madarasa mawili kwa nguvu za wananchi hadi
yamekamilika ilipofika suala kuezekwa tokaomba msaada wa Serikali pamoja
na kumaliziwa ili yaanze kutumika ilikuwa kazi kweli tulizunguzwa sana
hadi tukaanza kuyatumia hivyo hivyo,” alisema.
Bi. Thabita Farara ni Mkazi wa Kata ya Mringoti Mashariki anasema bado
mwamko wa elimu ya awali kwa wazazi ni mdogo, maana wazazi wengi
wamekuwa wakijiandaa na darasa la kwanza tu kumuandikisha mtoto. Kwa
upande wake Asha Komba Mkazi wa Tunduru Stendi anasema yeye anaitambua
elimu ya awali na kuikubali lakini ni ile inayotolewa na shule binafsi
kama za taasisi. Lakini ile inayotolewa kwenye shule za Serikali ni
tatizo kubwa maana hazizingatii ubora wa elimu zaidi ya kuwalundika
watoto tu darasani.
“…Mimi naitambua elimu ya awali na watoto wangu wote wamepitia lakini
huwa tunawapeleka kwenye chekechea za taasisi mbalimbali kama
zinazomilikiwa na makanisa majeshi na zinginezo maana huku ndiyo kidogo
mtoto anaandaliwa…kule Serikalini kwanza unakuta darasani wapo kibao
alafu muda wote wanacheza tu si kujifunza,” anasema Bi. Komba.
Abdul Kazembe ni Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, anasema kwa sasa
kila shule ya msingi sera inaelekeza lazima iwe na darasa la awali.
Anasema hata katika usajili wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa sasa
watoto wa mwanzo kusajiliwa ni wale waliopata elimu ya awali katika
shule husika.
“…Kwa hiyo kuna umuhimu wa kila shule kuwa na darasa la awali…changamoto
sasa inakuja kwenye vitendea kazi, kwa mwaka 2013 na kurudi nyuma uwepo
wa ‘capitation’ ulikuwa pia unaelekeza watoto wa awali wapo mule na
hata tunapotoa takwimu za awali tulianza na ‘pre-primary’ (wanafunzi wa
awali) hivyo wenyewe wapo, tatizo hapa ni ujaji wa pesa yenyewe ya
‘capitation’ haitimii kama inavyo elekeza, yaani ile wastani ya kwamba
kila mtoto apate shilingi 10,000 kwa mwaka hautimii,” anasema.
Anatolea mfano mwaka 2013/14 kiwango cha fedha ambacho kilitakiwa kuja
katika halmashauri ya wilaya hiyo ni zaidi ya milioni 366.7. Kiwango
hiki ni kile kilichoidhinishwa katika bajeti tu lakini ukirudi kwenye
mahitaji halisi ni zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa. Anasema kilichokuja
ni zaidi ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu ya kiasi
kilichopitishwa kwenye bajeti. Anabainisha hilo ndilo tatizo kubwa kwani
hata fedha ambazo zimepitishwa haziji kama ilivyopitishwa kwenye
bajeti.
“…Kwa hiyo unaweza kuona kwamba ni ngumu kuigawa fedha hii katika
matumizi maana kwanza haitoshi na pili hata kilichotegemewa kuja ni
pungufu zaidi tena sana, sasa sijui unaweza kugawa kila shule ipate
shilingi ngapi…kwani haitoshelezi,” anasema.
Anasema kwa upande mwingine miundombinu ya madarasa ni changamoto kubwa.
Kwa mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa wilaya nzima ilikuwa
ni 1,715 lakini ukiangalia vyumba vya madarasa vilivyopo ni kama 900 na
kitu na mengine ni ya muda mrefu sana kiasi ambacho yanaelekea kuchakaa
jambo ambalo pia yanapungua.
Aidha anaeleza kuwa ukienda kwenye bajeti ya ujenzi wa madarasa mapya
milioni 171 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na miundombinu mbalimbali
kiasi hiki cha fedha waweza kuta kinauwezo wa kujenga madarasa kama nane
tu. Kiasi hicho cha fedha ni pamoja na ujenzi wa nyumba tano za walimu.
Na kiasi hicho cha fedha za ujenzi ni pamoja na kumalizia miradi viporo
za nyumba za walimu na vyumba vya madarasa. Anasema upungufu wa vyumba
vya madarasa eneo hilo ni karibia madarasa 800.
“Sasa kwa ujumla unaweza kuona kuwa miundombinu pale shuleni
haitoshelezi, ni jambo la kawaida kuona walimu wakiacha ofisi itumike
kama darasa au darasa litumike kama ofisi. Huku kwa awali ni changamoto
zaidi maana licha ya upungufu wa vyumba hata wazazi hasa vijijini
wanashindwa kuchangia chakula (uji) kwa watoto wao unaweza kukuta
wameandikishwa wengi Januari lakini kila muda unavyozidi kwenda watoto
wanapungua na unaweza kukuta hadi mwezi Juni darasa linapotea kabisa kwa
utoro,” anasema.
Kazembe anabainisha kuwa kuna jumla ya shule za msingi 144 katika wilaya
hiyo, huku shule zilizo na vyumba maalumu vya madarasa ya awali zikiwa
16 tu. Anasema shule nyingine zote hazina vyumba vya madarasa ya awali
na matokeo yake ama wanatumia madarasa ya msingi kwa kupishana.
Anaongeza kuwa uhamasishaji wa ujenzi wa madarasa ya awali na umuhimu wa
elimu hiyo unatolewa kwa walimu, wazazi na kamati za shule kupitia
vikao mbalimbali ambapo mara nyingi uongozi uhimiza wazazi kuchangia
zaidi nguvu zao katika kukamilisha ujenzi wa madarasa ya awali,
utengenezaji wa madawati na upatikanaji wa chakula cha mchana na uji
shuleni.
“…lakini tunaangalia sana chakula maana watoto hata kwenye mti wanaweza
kukaa wakasoma endapo wanamadawati pale au wamekaa chini kwenye kivuli,
japokuwa si mazingira mazuri sana shuleni…lakini wakiwa na chakula hata
utoro unapungua,” anasema.
Anasema kwa mwaka 2013 serikali ilikumbuka kuleta fedha kwa ajili ya
ununuzi madawati ya wanafunzi wa awali, fedha ambazo tulizigawa na
kununua baadhi ya vitabu vya awali na madawati kwenye shule ambazo
zinamadarasa hai ya awali. Shule zilizonufaika na mgao huo ni shule za
mjini Tunduru tu ambazo nyingi ndizo zenye madarasa hai ya awali.
Anasema ili kukabiliana na hali ya upungufu wa walimu wa awali;
imepitishwa walimu wa gredi ‘A’ kufundisha madarasa hayo kwa kuwa wao
mafunzo yao katika kozi hujumuisha ufundishaji darasa la awali, tangu
walioitimu mwaka 2013.
“…sasa wakati mwingine unaweza kukuta mwalimu ni gradi A na kimsingi
yeye anao uwezo wa kufundisha darasa la awali, lakini wengine hawakubali
hadi aone ana cheti kabisa maalumu cha kufundisha darasa la
awali…ukimuuliza huyu atakwambia yeye hana taaluma ya kufundisha awali
jambo ambalo si sawa,” anasema Ofisa Elimu huyo wa Msingi.
“..Kwa suala la vitabu kweli hii ni changamoto, hapo nyuma tulikuwa
tunanunua vitabu wenyewe wakini kwa sasa TAMISEMI wenyewe moja kwa moja
wananunua na kuvileta. Sasa huku kwetu ni nadra sana kuona wazabuni wetu
wanaleta vitabu vya awali kwa sababu soko lake ni dogo sana kutokana na
idadi ndogo ya uwepo wa elimu hii ya awali eneo husika,” anasema.
Hata hivyo umeona unafuu maeneo ya mjini mzazi anatambua umuhimu wa
elimu hivyo anaweza kuchonga dawati kwa ajili ya mtoto wake lakini kwa
vijijini hali ni mbaya zaidi. Mzazi ukimwambia achangie dawati
anakushangaa na pia haoni umuhimu huo.
“…Nikwambie unajua Wilaya ya Tunduru mzazi mtoto wake akifeli anafurahi
sana…tena baadhi wanaona kama ni sherehe, kwanza wakifanya mtihani tu wa
la saba barabarani akina mama wanashangilia wanaona wametua mzigo,
unaweza kujiuliza wazazi wanaoshangilia inamaana walikuwa wakiona ni
adhabu watoto wao kuwa shule? Lakini pia mtoto akisha faulu kwenda shule
hapelekwi hadi DC aunde kamati, atembee na hakimu na polisi kukamata
wazazi wanaogoma kusomesha watoto watishiwe ndo wanakubali
kusomesha…lakini kitendo cha wazazi kukamatwa kushikiliwa kwa kushindwa
kuwapeleka watoto shule wamegeuka na kuwarubuni watoto wao wasifaulu,”
anasema.
Anabainisha kuwa ni kweli Serikali ina jukumu la elimu, lakini mzazi kwa
upande wake anajukumu zaidi, kuangalia mtoto wake anapata elimu gani na
ya kiwango gani na kama mzazi hayupo tayari basi haiwezekani na wakati
mwingine inakuwa ngumu. Kimsingi jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa
vifaa vya kufundishia na kujifunzia watoto wa awali zipo, lakini
upatikanaji wa fedha ndio.
Salum Mtutula ni Mbunge wa Tunduru Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Mbunge huyu katika mahojiano anakiri kuwa elimu ya awali ni
muhimu na msingi mzuri wa mtoto kielimu. Anasema mtoto anapopata elimu
nzuri ya awali huwa na msingi mzuri kielimu katika masomo yake ya mbele.
“…Ili mtoto apate elimu bora ni lazima apate elimu ya awali
inayostahiki…hakiwa na msingi mbaya wa elimu ya awali kuna uwezekano
mkubwa way eye kufanya vibaya pia,” anasema Mtutula.
Hata hivyo anaishauri Serikali kuingiza suala hili katika sheria na
kanuni zake kuwa kila shule ya msingi inapoanzishwa ianze na darasa la
awali kwanza ndipo madarasa mengine yafuate. “…Mimi nitafurahi kama
suala hili tutaliweka kwenye sheria au kanuni zetu kuwa kila shule ya
msingi inapoanzishwa basi lazima ianze na darasa la awali ndipo madarasa
mengine yafuate iwe shule za Serikali au binafsi,” anasema Mbunge
Mtutula.
*Imeandaliwa na: www.thehabari.com
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment