Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), amekamilisha awamu nyingine ya ziara zake mikoani. Katika awamu hii, alitumia siku 28 kutembelea mikoa ya Pwani, Tanga na Iringa.
Wapo ambao wanazibeza ziara hizi kwa sababu za kisiasa, lakini kwa wanaozifuatilia kwa karibu, wameshagundua kuwa zitakuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa CCM katika uchaguzi ziku za usoni.
Kuna mambo mengi ambayo Kinana na timu yake wanayafanya katika ziara hizo ambayo yanarudisha imani ya wananchi kwa CCM.
Siyo siri kuwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita, wananchi wengi walianza kupoteza imani na chama tawala kwa sababu mbalimbali, kubwa ikiwa chama hicho kushindwa kutekeleza kile inachokiahidi.
Hata Kinana anakiri katika hotuba zake kwenye ziara kuwa ni kweli CCM ilipoteza mwelekeo kidogo katika miaka ya hivi karibuni.
Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kinana anasema ni kweli chama hicho kiliingia mushkeli.
“Moja kati ya madhumuni ya ziara zangu mikoani ni kukagua uhai wa chama na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi… hapa katikati CCM iliacha kufanya yale yanayostahili kufanywa na chama tawala,” anasema.
Hata hivyo, Kinana haishii kukagua utekelezaji wa ilani tu.
Pale anapobaini makosa husema waziwazi na huwa hamwonei mtu yeyote aibu.
Anawakosoa kuanzia viongozi wa CCM wenyewe na watendaji katika halmashauri za wilaya au hata serikali kuu pale anapobaini wametenda makosa.
Ndiyo maana mara nyingi katika hotuba zake, ukimsikiliza Kinana wakati anahutubia, unaweza kudhani anayezungumza ni mpinzani.
Ile lugha ya kuwasema viongozi wa Serikali na CCM ambayo kwa miaka mingi imezoeleka kutoka kwenye vinywa vya wanasiasa wa upinzani, sasa inatolewa na Kinana, tena si kwa kificho, bali kwenye mikutano ya hadhara
Hilo linaanza kuwafanya baadhi ya watu kuona kuwa kumbe hata CCM inaweza kupingana na makosa makubwa serikalini kama vile rushwa, uzembe, umangimeza na hata ufisadi.
Msimamo wa Kinana
Akizungumza na katika ziara yake, Kinana anasema kazi ya kuikosoa Serikali iliyopo madarakani inapaswa kufanywa na viongozi wa CCM kwa sababu Serikali hiyo imewekwa na chama hicho ili kutekeleza mkataba baina ya CCM na wananchi.
Jambo jingine ambalo liliwafanya watu waanze kupoteza imani na CCM ni kitendo chake cha kukumbatia watu wa tabaka la juu.
Wafanyabiashara na watu wenye madaraka serikalini au kwenye chama walionekana kuwa ni bora zaidi kuliko wakulima na wafanyakazi ambao ndiyo msingi mkuu wa uanachama wa CCM.
Katika ziara zake, Kinana anajitahidi kufika maeneo ambako anakutana na watu wa kawaida moja kwa moja. Wala hakuna urasimu kwa watu kuzungumza naye.
Mbinu anazotumia
Mwenyewe amekuwa na utamaduni wa kuwaruhusu watu wa kawaida kuuliza maswali katika mikutano ya hadhara. Kinana anasema hapendi kuendelea na mtindo wa viongozi ambao kazi yao ni kuwahutubia tu wananchi.
“Wakati mwingine unaweza kutoa hotuba ndefu sana lakini isiyogusa masilahi ya wananchi unaowahutubia. Watu wanaweza kukushangilia lakini baadaye wanakuponda kwa sababu hukusema mambo yanayowahusu,” anasema.
Wananchi ambao wanapata nafasi ya kuuliza maswali katika mikutano ya Kinana, huwa wanajisikia furaha kwa kupata fursa ya kuzungumza na kiongozi mkubwa moja kwa moja
Wengi wanawataka viongozi wengine kuiga utamaduni huo kwa sababu unawapa furaha na fursa ya kuibua masuala mengi ya msingi yanayowasumbua.
Mtindo huu wa maswali ya papo kwa hapo unageuka kuwa kama mahakama ya wazi kwani wananchi wanaweza si tu kueleza matatizo yao, bali pia kuwasema na wakati mwingine kuwachukulia hatua viongozi wao ambao hawawajibiki.
athalan, katika mkutano uliofanyika katika eneo la Mponde katika Jimbo la Bumbuli, wananchi walimfukuza kutoka kwenye mkutano huo wa hadhara diwani wao, RichardMbuguni kwa maelezo kuwa amekuwa akiwasaliti katika kushughulikia matatizo ya kiwanda cha chai kilichofungwa tangu Mei mwaka huu.
Anavyojichanganya na wananchi
Pamoja na kuwaruhusu watu kuuliza maswali moja kwa moja, pia Kinana amekuwa akishiriki shughuli na wananchi. Mara kadhaa amethubutu kufanya mambo ambayo viongozi wengine wakuu wa chama au Serikali hawawezi kuyafanya.
Wakati mwingine, Kinana aliamua kutumia usafiri wa boti za kawaida alipotembelea Kisiwa cha Mafia. Ingawa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani ilimuonya kuwa usafiri huo si salama, lakini Kinana aliamua kuutumia.
Alipotakiwa aeleze kwa nini ameamua kufanya hivyo, alisema: “Kama wananchi wanautumia usafiri huu kila siku, kwa nini mimi nisiutumie?
“Kama kiongozi sitautumia usafiri huu, hivi nitawezaje kufahamu kwa undani matatizo yanayowakabili wananchi wanaoutumia usafiri wa aina hii?
Kusafiri kwangu kwa boti kumenifanya nijue matatizo yake kwa undani hivyo inakuwa rahisi zaidi pale mnapoamua kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo.”
Alipokuwa katika Kijiji cha Mlola, Lushoto, mkazi mmoja alimtaka aende kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuwa wananchi wa huko wanamtaka awatembelee.
“Mimi hapa ni mzee sana lakini ukiniuliza nikuelezee viongozi naweza kumwelezea (Mwalimu Julius) Nyerere pekee kwa sababu ndiye kiongozi wa juu niliyewahi kumuona.
Hawa wengine nawasikia kwenye vyombo vyahabari tu,” alisema mzee mmoja wakati alipopatiwa nafasi ya kuuliza swali kwenye mkutano wa hadhara.
Mzee huyo alimpongeza Kinana kwa kupita kwenye barabara yenye milima, mabonde na kona nyingi ili kufika kijijini hapo.
Katika ziara zake mikoani, Kinana hutembelea kila jimbo la uchaguzi ambako mbali na mikutano ya hadhara, pia hufanya mikutano ya ndani na viongozi wa CCM na kwa kiasi kikubwa, huangalia matatizo ya chama hicho na kupanga mikakati ya kukabiliana nayo.
Haya ni baadhi ya mambo ambayo Kinana anayafanya na kwa mujibu wa tathimini ya CCM, yanasaidia kurejesha imani ya wananchi ambao walianza kukiona kimewageuka.
Jambo moja ni dhahiri kuwa ingawa ziara hizi za Kinana haziwezi kuwa silaha pekee kwa CCM, lakini zina mchango mkubwa katika kukirejesha mioyoni mwa wale wanaomini kuwa kipo kwa ajili ya kuwatetea wanyonge.
0 comments:
Post a Comment