Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean
Ndumbaro akitoa maelekezo mbalimbali ya masuala ya kiutumishi katika
Halmashauri ya Wilaya ya Madaba katika siku ya kwanza ya ziara yake ya
kikazi ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Ruvuma. Kulia kwake ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Hamashauri ya Wilaya ya Madaba Bw. Shafi Mpenda na kushoto
kwakwe ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Bw. Bwai Biseko.
Baadhi
ya watumishi wa Hamashauri ya Wilaya ya Madaba wakisikiliza kwa makini
maelekezo ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) aliyoyatoa katika
halmashauri hiyo, wakati ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji
mkoani Ruvuma.
Kaimu
Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Bw. Biseko Bwai akitoa taarifa ya
utekelezaji wa masuala ya kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro katika siku ya
kwanza ya ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu huyo mkoani Ruvuma yenye lengo
la kuhimiza uwajibikaji.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijiji Bw. Simon
Bulenganija akitoa taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.
Laurean Ndumbaro katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu
huyo mkoani Ruvuma, yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Mkurugenzi
wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini wa Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Ibrahim Mahumi
akitoa maelekezo kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea
Vijijini kuhusu taratibu zinazohusu menejimenti ya Rasilimaliwatu
serikalini, wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais -
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ya kuhimiza
uwajibikaji.
Baadhi
ya watumishi wa Hamashauri ya Wilay ya Songea Vijiji wakimsikiliza
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt.
Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) katika siku ya kwanza ya ziara ya
kikazi ya katibu mkuu huyo ya kuhimiza uwajibikaji katika Hamashauri
hiyo.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean
Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma nchini kuzingatia uadilifu katika
utendaji kazi, kujituma, kuwajibika kwa wananchi na kwa Serikali ili
kujenga Utumishi wa Umma uliotukuka.
Dkt.
Ndumbaro amesema hayo, katika ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani
Ruvuma yenye lengo mahususi la kubaini changamoto zinazowakabili
Watumishi wa Umma katika maeneo yao ya kazi na kuzitafutia ufumbuzi ili
kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ikiwa ni pamoja
na kuwasisitiza Watumishi wa Umma juu ya mwelekeo wa Serikali ya Awamu
ya Tano.
Dkt.
Ndumbaro akiwa katika Halmashauri za Wilaya ya Madaba na Songea
Vijijini amewaeleza watumishi wa halmashauri hizo kuwa, misingi ya
uadilifu na uwajibikaji itajengwa na watumishi hao kwa kubadili
utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea (business as usual).
Dkt.
Ndumbaro amesema kwamba, Wakurugenzi pamoja na Wakuu wa Idara nchini
wana jukumu kubwa la kusimamia utendaji kazi katika maeneo yao ya kazi
ili kubadilisha tabia za baadhi ya watumishi wasiowajibika ipasavyo, na
kuwafanya watekeleze wajibu wao kwa bidii na kwa uadilifu mkubwa.
“
Ninyi Wakurugenzi na Wakuu wa Idara mhakikishe mnahimiza nidhamu kwa
Watumishi wa Umma katika maeneo yenu, mtumishi akikosea achukuliwe hatua
mara moja kwa mujibu wa Sheria , Kanuni na Taratibu za Utumishi wa umma
zilizopo” Dkt. Ndumbaro amefafanua.
Dkt.
Ndumbaro amebainisha kuwa, kama kuna watumishi wasiotimiza wajibu wao
na hawachukuliwi hatua zozote za kinidhamu au za kisheria dhidi yao,
kitendo hicho huwakatisha tamaa watumishi wanaojituma katika utendaji
kazi wao.
Aidha,
Dkt. Ndumbaro amekemea tabia iliyojengeka kwa baadhi ya watumishi ya
kuwakatisha tamaa watumishi wanaojituma na wanaozingatia maadili.
“Viongozi tusipokemea na kuwachulia hatua watumishi wenye tabia ya
kuwabeza na kuwakatisha tamaa watumishi wanaojituma kazini, ni dhahiri
kuwa itashusha morali ya utendaji kazi wa watumishi wanaochapakazi” Dkt.
Ndumbaro amesisitiza.
Dkt.
Ndumbaro amewataka Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kuwatambua watumishi
wanaofanya kazi kwa bidii kwa kuwapa moyo na motisha, ikiwa ni pamoja na
kuwaandikia barua za kuwapongeza ama kuwapa vyeti ikiwa ni mkakati wa
kukuza utamaduni wa watumishi kupenda kufanya kazi.
Pia,
Dkt. Ndumbaro hakusita kuwasisitiza Maafisa Utumishi, Watumishi wa
Masijala na Makatibu Mahususi kuwa na lugha nzuri wakati wa kuwahudumia
wateja wa ndani na wa nje pindi wanapofika kwao kupata huduma.
Dkt.
Ndumbaro anaendelea na ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji mkoani
Ruvuma katika Halmashauri za Wilaya ya Songea Mjini, Tunduru, Mbinga,
Nyasa, na Namtumbo.
0 comments:
Post a Comment