Home » » Mbambabay wapata boti mpya

Mbambabay wapata boti mpya

UMOJA wa wakazi wa wilaya mpya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, waishio jijini Dar es salaam, umetoa msaada wa boti moja yenye thamani ya sh milioni 16 kwa wananchi wa Mbambabay wilayani humo kwa ajili ya kuendeshea shughuli za uvuvi wa kisasa.
Boti hiyo ilikabidhiwa mwishoni mwa wiki na mwenyekiti wa umoja huo Cassian Njowoka, kwa mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi ili litolewe kwa kikundi kimojawapo ambacho kinajishughulisha na shughuli ya uvuvi kwa madai kwamba mapato yatakayopatikana yaweze kununulia boti nyingine ambayo itagawiwa kwa kikundi kingine.
Njowoka alisema kuwa lengo la chama chao ni kuhakikisha kila kikundi cha uvuvi kinapata boti ya kisasa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika shughuli zao tofauti na ilivyo sasa ambapo wanaendesha uvuvi wa hatari wa kutumia mitumbwi ambayo wakati wa dhoruba inashindwa kuhimili na kusababisha maafa kwa wavuvi.
Alisema mpango wa chama hicho ni kuhamasishana juu ya kuwekeza wilayani humo na kusaidia nyanja mbalimbali ikiwemo vikundi vya vijana wanaofanya shughuli ya uvuvi, kilimo kwa kugawa miche ya kahawa kwa kila mwananchi ambaye ana shamba ili waondokane na dhana ya kutegemea uvuvi peke yake.
Njowoka aliendelea kusema kuwa endapo wananchi hao watalitumia boti hilo ipasavyo na kurejesha mapato kwa uaminifu walao kila wanapofikisha shilingi milioni saba, watakuwa tayari kusaidia tena boti moja kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vingine.
Aidha chama hicho kina mikakati mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu wilayani humo ikiwa ni pamoja na kuanzisha Shule ya Sekondari ya Wasichana Lituhi ambayo itakuwa na kidato cha kwanza hadi cha sita.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Ernest Kahindi, alikipongeza chama hicho kwa msaada wake na kusema kwamba ni cha kizalendo na kwamba wilaya itajenga karakana ya boti ili wakazi wa mwambao mwa Ziwa Nyasa wapate fursa ya kutengeneza na kujifunza juu ya uvuvi wa kisasa.
Imeandikwa na Julius Konala, Ruvuma
Source: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa