Baada ya kumaliza Mkwawa nilingia Chuo Kikuu cha Dar e Salaam kuchukua Sayansi ya Jamii, lakini nilisoma mwaka mmoja nikaacha.
Mwandishi:Baada ya kuacha chuo kikuu ulikuwa unafanya nini?
Rubani:Nilikuwa nyumbani nikijishughulisha na
uandishi na pia kuchora jambo ambalo lilinifanya niitwe kwenye mafunzo
ya siku sita kuhusu uandishi Chuo Kikuu cha Makerere ambako nikawa mmoja
wa watu wa kwanza tulioandika jarida la kwanza la chuo hicho.
Niliporudi nchini nilipata kazi kwenye Shirika la British America
Tobacco Company (BAT) ambako nilifanya kazi karibu mwaka mmoja na
baadaye niliacha.
Mwandishi: Ni kwa nini uliacha?
Rubani: Sikumbuki.
Mwandishi: Baada ya hapo ulikwenda wapi?
Rubani: Nakumbuka mwaka 1970 nikiwa nyumbani
Songea, alikuja Jenerali Luis ambaye alikuwa mwenyeji wa Mkoa wa Rukwa
na kuniambia kwamba walikuwa wakihitaji vijana waliosoma ili wawe
marubani wa jeshi. Hoja hiyo niliipenda na nikakubali, hivyo
aliniandikisha na kunitaka niende kwenye mafunzo ya kijeshi (TMA) Dar es
Salaam kwa ajili ya uofisa.
Nilimaza mafunzo kwenye kikosi cha anga Dar es
Salaam na baada ya hapo pamoja na wenzangu karibu 14 tuliendelea na
mafunzo ya kuendesha ndege kwa chini (Ground School) kwa mwaka mmoja na
baada ya hapo tulianza mafunzo ya awali ya kurusha ndege.
Mwandishi: Tangu mafunzo hadi kuanza kazi, je uliwahi kupata ajali?
Rubani: Ndiyo, nilipata ajali mwaka 1978
nikiwasafrisha askari 26 kutoka Dar es Salaam kwenda Beira Nover Freesco
Msumbiji ingawa sikujua askari wale walikuwa wakienda nchi gani. Sijui
walikuwa wa Zimbabwe au Angola sijui. Injini ya kushoto ilizimika ghafla
na baadaye injini ya kulia ikazima hivyo nililazimika kutua kwenye
shamba dogo porini na askari wote tulitoka salama isipokuwa mmoja
alipata michubuko kutokana na bawa la ndege kugonga kichuguu. Kipande
hiki (anainuka kuchukua na kukionyesha kichuma cha bawa la ndege)
nilipewa kama kumbukumbu.
Baada ya ajali hiyo, mwishoni mwa mwaka 1978 nilikwenda Uingereza kusoma utaalamu wa ndege aina ya Hauca Cidre748
.
Mwandishi:Je, vita dhidi ya Idd Amin Dada ulishiriki?
Ruban: Tangu mwanzo hadi mwisho mimi nilikuwa mmoja wa walioshiriki mchana na usiku hadi vilipoisha.
Mwandishi: Unakumbuka nini kwenye vita hivyo?
Rubani: Nakumbuka siku moja nilikuwa off
(napumzika kidogo), nikaamua kunywa bia. Na ratiba ilikuwa ikionyesha
nitakuwa kazini kesho yake. Lakini ghafla kiongozi wangu alinijia na
kunitaka nirushe ndege. Mimi nilikataa katakata kwa sababu nilikuwa
nimekunywa pombe. Niliwahi kumwendesha Nyerere.
Mwandishi: Je, ni kweli ulimwendesha Nyerere? Na kazi ya jeshi iliendelea hadi lini?
Rubani: Ni kweli baada ya vita vya Amini
niliendelea kurusha ndege za jeshi na pia kufanya kazi ya kuendesha
ndege ya Rais Nyerere. Mwaka 1983 Januari 7, nilikamatwa na wanajeshi
wengine wengi kwa tuhuma za uhaini. Tulidaiwa tulitaka kumuua Rais
Julius Nyerere. Nilikamatwa nikiwa eneo la Airwing Dar es Salaam.
Tulikaa kizuizini hadi Julai mwaka 1983 Mahakama ilipotangaza kwamba
hatukuwa na kesi ya kujibu. Lakini cha kushangaza mwaka 1985 watu tisa
kati ya wale walioshikiliwa mara ya kwanza, tulikamatwa tena na
kufikishwa mahakamani kwa kosa la kutaka kumuua Rais Nyerere.
Mwandishi: Je, kiukweli mpango huo ulikuwapo?
Rubani. Aaa...ulikuwapo haukuwapo, ‘it was planned
by high official (ulipangwa na baadhi ya maofisa za ngazi za juu)’,
unajua baada ya vita vya Uganda nchi ilikuwa imefilisika. Haikuwa na
unga, sabuni, sukari na hata nguo, karibu kila kitu hakikuwapo. Hivyo
Watanzania wengi walikuwa wamechanganyikiwa na hali ile.
Mwandishi: Kwa maana hiyo mpango huo ungefanikiwa je bidhaa hizo zingeonekana?
Rubani: Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi
aliiokoa nchi baada ya kuruhusu kila kitu kiingie nchini hata bila ya
kutoza kodi. Mwinyi aliituliza nchi. Pia Serikali iligundua kwamba
waliokamatwa walitaka mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kuishtua CCM
ambayo ilikuwa imejisahau na hivyo kuanzishwa kwa vyama vingi jambo
ambalo lilitekelezwa baadaye.
Mwandishi: Matatizo yaliyokuwapo enzi hizo na sasa unatofautishaje?
Rubani:Kama nilivyosema, enzi za Nyerere nchi
ilifilisika, Mzee Mwinyi aliiokoa nchi, Rais Mkapa akaweka msingi wa
kukusanya kodi, hivi sasa sijui kinachoendelea kwa kuwa sisomi sana
magazeti kwani sina fedha za kununua.
Mwandishi: Mama Robert ulifanikishaje safari yako kurudi Songea. ?
Mkewe: Mimi niliposikia anafungwa maisha nilipigwa
na butwaa na simanzi kubwa. Hivyo sikuwa na nguvu, lakini cha ajabu,
baada ya saa 12 kupita, mkuu wa kikosi aliniita na kunitaka niondoke
kwenye nyumba ndani ya saa 24. Kumbuka wakati ule mimi nilikuwa
nafundisha Chuo Cha Utumishi Magogoni Dar es Salaam, hivyo nilihitaji
kupata nafasi ya kuomba uhamisho na kufunga mizigo. Lakini mambo ya
jeshi ni amri na nilitolewa mizigo ili nisafirishwe kwa ndege ya Jeshi
ambayo nayo iliharibika. Lakini kwa bahati ilipona kabla ya saa 12
kumalizika, nikatakiwa nitaje niende wapi.
Suala hilo lilinifanya nitaje Songea kwa vile nilikuwa na watoto sita na Robert na watoto walikuwa wakiwafahamu ndugu wa Songea.
Hivyo mizigo na watoto walisafiri kwa ndege mimi
nikabaki Dar es Salaam nikiomba uhamisho wa kwenda kufundisha Shule ya
Sekondari ya Songea Wasichana.
Kwa kweli ilikuwa fedheha kubwa. Serikali
inampenda mfanyakazi mzuri, lakini huyohuyo akiteleza kidogo ni
takataka. Ipo haja ya kubadilisha msimamo huo.
Mwandishi: Kwako rubani, je unalo neno kwa Serikali?
Rubani:Aaaa , tangu nifike huku sijapata na wala
sina senti ya Serikali. Wapo wenzangu waliosema eti Serikali inafikiria
kutupatia chochote, lakini mpaka sasa sijasikia lolote.
Mwandishi: Kwa sasa afya yako ikoje na unajishughulisha na nini?
Rubani. Afya yangu nashukuru Mungu naendelea vyema, mambo mengine Mungu anasaidia.
Kapteni Mstaafu Rodrick Robert anasema ni suala la
msingi kwa watu kuwa na moyo wa kulitumikia taifa kwani ndio msingi wa
kuhakikisha tunakuwa na taifa lenye maendeleo makubwa.
“Jambo la msingi ambalo napenda kusisitiza ni moja
tu kwamba kwa kila kitu ambacho mtu anafanya, anapaswa kuweka mbele
maslahi ya taifa kwanza,” anasisitiza akiwaasa Watanzania kujenga tabia
ya kuheshimu mila na tamaduni za taifa, pia kujali maadili ya uongozi.
Aidha anawashauri vijana kufanya kazi kwa bidii
ili kuharakisha maendeleo nchini, kwani vijana ndio tegemeo kubwa kwa
taifa na ulimwengu kwa ujumla kwa vile wana nguvu za kutosha.
Chanzo;Mwananchi.