WAKUFUNZI na wafanyakazi wa Chuo cha Ualimu Songea,
wameilalamikia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kitendo cha
kushindwa kushughulikia mgogoro uliopo chuoni hapo na kusababisha
shughuli mbalimbali za kiutendaji kudorora.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao wameelezea hofu ya kutofanikisha
mpango mkakati wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa na kuitaka serikali
kumuondoa madarakani Mkuu wa Chuo hicho, Ubaya Suleiman, ili kukinusuru
chuo hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa wanafunzi hao
ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walisema kuwa katika chuo hicho
kuna mgogoro ambao umeshindwa kuchukuliwa hatua na kusababisha amani na
utulivu kukosekana chuoni hapo kwa zaidi ya miezi saba sasa.
Walisema kuwa mgogoro huo umetokana na uongozi mbovu usiozingatia
misingi ya uongozi na demokrasia katika vyuo vya ualimu nchini kwani
mkuu wa chuo hicho, amekuwa mbabe, lugha chafu na mtu wa vitisho kwa
wafanyakazi na wanachuo.
“Pamoja na hayo, mkuu huyo wa chuo amediriki kuwapeleka baadhi ya
wafanyakazi wake kwenye vyombo vya dola (polisi), akiwatuhumu kuwa
wanataka kumuua.
“Baada ya mgogoro huo kutopata suluhu kupitia vikao vya ndani,
jitihada zifuatazo zilifanyika na wafanyakazi wa chuo hicho ili kuleta
hali ya amani na utulivu.”
Walifafanua kuwa Aprili 27 mwaka huu, walifanya kikao na mkuu wa
wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, Mei 15 na Juni mosi mwaka huu,
walifanya kikao na bodi ya ushauri ya chuo, hata hivyo suluhu ya mgogoro
huo haikupatikana.
Walisema kuwa kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome aliunda tume ya watu watano
ikiongozwa na mkaguzi mkuu wa shule na vyuo wa nyanda za juu kusini
ambaye alifahamika kwa jina moja la Lyapambile, kuja kufanya utafiti wa
chanzo cha mgogoro, lakini mpaka sasa tume hiyo haijatoa majibu ya
uchunguzi wa jambo hilo.
“Hata hivyo wakufunzi hawakuishia hapo Agosti 13, 2013 walifanya kikao
na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu, ambaye baada ya kusikiliza
mgogoro huo aliahidi kuleta suluhisho la kudumu mapema iwezekanavyo ili
kuleta amani na utulivu chuoni hapo. Lakini cha kushangaza hadi sasa
yapata miezi mitatu hakuna kilichofanyika hali ambayo imeendelea
kuwavunja moyo wafanyakazi wa chuo hicho,” walisema.
Mkuu wa chuo hicho, Ubaya Suleiman, alipoulizwa kuhusu mgogoro huo,
alisema hana jambo la kuzungumza kwani mgogoro huo uko kwenye Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hivyo
hawezi kusema chochote.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo ambaye
amejitambulisha kwa jina la H. Lugome ameonyesha masikitiko makubwa sana
juu ya utendaji wa mkuu wa chuo hicho na kuahidi kukutana na
wafanyakazi hao ili kuweza kufanya kikao cha mwisho cha majadiliano.
Naye Naibu Waziri wa Elimu Philipo Mulugo alipotafutwa kupitia simu
yake ya kiganjani, alisema swala hilo bado halijafika mezani kwake na
endapo likifika basi atachukua hatua stahiki
Chanzo;Tanzania Daima
|
0 comments:
Post a Comment