Home » » January atinga Songea kusaka urais

January atinga Songea kusaka urais

Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Tekenolojia,January Makamba
 
Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Tekenolojia, January Makamba amekutana na baadhi ya wafanyabiashara mjini hapa Mkoa wa Ruvuma  ambao inadaiwa amewaomba wamuunge mkono katika nia yake ya kugombea urais mwaka 2015.
Hayo yamefahamika mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya January ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kudai kufanya kikao na wafanyabiashara hao   kwenye hoteli  ya TOP ONE INN iliyopo Msamala Manispaa ya Songea.

Inadaiwa kuwa January aliwaangukia wafanyabiashara hao kwa kuwaomba kuwa kipindi cha uchaguzi kitakapofika, wamsaidie kumpa ushirikiano ili ashinde katika kinyang'anyiro cha urais.

Baadhi ya wafanyabiashara waliliambia NIPASHE  kwa masharti ya kutotajwa majina yao gazetini kuwa    muda mfupi kabla ya kikao hicho kufanyika, walipigiwa simu wakitaarifiwa kuwa wanahitajika kwenye hoteli hiyo kwa mazungumzo.

Walisema walipofika kwenye eneo la hoteli hiyo, walikaribishwa kwenye ukumbi wa mikutano na kigogo mmoja wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ambaye walimtaja kwa jina la Halfan Kigwenembe.

Walisema wakiwa kwenye ukumbi huo, kikao kilianza baada ya mmoja wa wafanyabiashara hao kusimama na kumtambulisha kiongozi huyo na  kuelezea lengo la kuwaita baadhi yao.

Alisema wafanyabiashara hao waliofika kwenye kikao hicho walianza kuwa na maswali mengi wakitaka kujua kwanini waitwe wao badala ya kufuata utaratibu.

Alisema baadaye Janaury alipewa nafasi ya kujieleza akisema amefika mjini Songea kukutana na wafanyabiashara hao akiwa na lengo la kuomba aungwe mkono kipindi uchaguzi mkuu utakapofika.

Alisema wafanyabiashara wengine walimuuliza maswali ambayo yalimtaka kiongozi huo atoe ufafanuzi wa sababu za kuchukua uamuzi kama huo mapema hivyo kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake na CCM kutangaza kuanza kumsaka mgombea wake wa urais.

Pia alihojiwa kama haoni wadhifa wake wa Naibu Waziri na majukumu aliyonayo hauonyeshi kuwa hana uwezo mkubwa wa kufikia kuomba nafasi ya kuongoza nchi.

Alisema walimtolea mfano kuwa haoni kuwa hana ubavu katika kuchapa kazi kama mawaziri wa Uchukuzi,  Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Ujenzi,  Dk. John Mgufuli ambao wamemudu vilivyo nafasi walizopewa na Rais Kikwete na Watanzania, hivyo yeye hana cha kuonyesha kwa Watanzania.

Mpashaji wa habari hizi alisema kuwa January alisema serikali ya awamu ya nne inafahamu kwa dhati umuhimu wake na kuwa kwenye kampeni ya uchaguzi mkuu wa 2010 yeye alikuwa ni mmoja wa wanakamati wa kumsaidia Kikwete kuhakikisha  anashinda na kufanikiwa.

Alisema alidai ndiye aliyekuwa akiandika ratiba za kampeni na hotuba za mikutano ya kampeni aliyokuwa akifanya Kikwete katika majimbo mbalimbali nchini,  hivyo anazo sifa za kutosha kugombea nafasi urais kwa mwaka 2015.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya CCM Songea Mjini, Gerald Mhenga, alipohojiwa na NIPASHE kwa njia ya simu kuhusu ujio wa January, alisema hana taarifa kwa sababu hakupitia ofisini kwake.

Mhenga alisema kama kweli January ana nia ya kugombea urais kupitia CCM hasingeweza kukwepa kufika ofisi za Chama hicho labda atagombea kupita vyama vingine.
Naye Katibu wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma, Velena Shumbusho, alipohojiwa na NIPASHE kwa njia ya simu,  alisema hana taarifa za ujio huo wala za kikao chake na wafanyabiashara hao.
Hata hivyo, Shumbusho alikataa kuzungumzia kwa undani kwa madai kuwa yupo katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM wa Taifa, Abdallahiman Kinana.
Kwa upande wake, January alipohojiwa na NIPASHE kwa simu alithibitisha kufika mjini Songea na kukutana na wafanyabiashara hao.
Alifafanua kuwa alifanya hivyo baada ya wafanyabiashara hao kumuita kwa lengo la kuwasilisha malalamiko yao na kufanya nao mazungumzo kwa muda mrefu kujadili ajenda nne walizompelekea.

Alitaja malalamiko hayo kuwa ni kuhangaishwa kwa kubebeshwa mahindi kutoka vijijini hadi kwenye  Hifadhi ya Taifa ya Chakula (SGR) mjini Songea na yakifikishwa hapo wanatafutwa wafanyabiashara wakubwa kuyapeleka mikoa mingine ikiwamo Dar es Salaam na Dodoma.

Alisema wafanyabiashara hao walimlalamikia kuwa kitendo hicho kinaashiria kuwapo kwa mianya ya rushwa zinazotolewa na wafanyabiashara wakubwa kwa baadhi ya viongozi wa kitengo hicho na serikali.

Kuhusu kugombea urais, January alisema aliombwa na wafanyabiashara hao kujitosa katika kinyang'anyiro hicho mwaka 2015, lakini aliwajibu  wakati ukifika ataangalia kama ataamua au.

Alisema aliwataka wafanyabiashara hao kuvuta subira kwa madai kuwa kwa sasa bado ni mapema mno kuzungumzia kama ana dhamira hiyo au la.

"Ndugu mwandishi mimi niliitwa na wafanyabiashara wenyewe na waliniomba niwape ukweli kama ninahitaji kugombea urais 2015, lakini mimi sikuja kutafuta watu wa kunisaidia kugombea," alisisitiza.

NIPASHE ilizungumza na Kigwenembe kwa njia ya simu juu ya kuratibu mkutano wa January, alithibitisha Naibu Waziri huyo kufika Songea na kukutana na baadhi ya wafanyabiashara na kukataa kuzungumzia zaidi akidai hakuwapo kwenye kikao hicho.

Ujio wa January mji hapa na kikao hicho na wafanyabiashara hao, umeacha maswali kwa baadhi ya wananchi na wanasiasa wakihoji kuwa wizara yake haina dhamana ya kufanya hivyo.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti walisema wanajiuliza maswali mengi kwa sababu hana dhamana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Biashara na Viwanda na Wizara ya Uchukuzi ambazo kwa namna moja au nyingine zingeweza kupelekewa malalamiko hayo na kuyapatia ufumbuzi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa