Home » » Ukopaji pembejeo za tumbaku Namtumbo wawekewa masharti

Ukopaji pembejeo za tumbaku Namtumbo wawekewa masharti

SERIKALI wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma imeanza kuchukua hatua za kuzuia kuporomoka kwa kasi kwa zao la tumbaku kunasababishwa na kuchezewa kwa hesabu za mikopo hivyo kumbebesha deni hewa mkulima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Rajab Lutav na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu wamesema kwa kuanzia wamepiga marufuku vyama vya tumbaku wilayani humo kukopa katika benki zilizo nje ya Namtumbo.
Wanasema uozo huo unaolalamikiwa na wakulima unafanywa kwa ushirikiano kati ya maofisa wa benki zinazokopesha wakulima pembejeo na viongozi wa vyama vya ushirika. Mkuu wa Wilaya ya Namtombo, Rajab Lutav anasema lengo la hatua hizo ni kurejesha matumaini ya wakulima yaliyovia kutokana na kuzidiwa na madeni hewa huku wilaya yake ikizidi kukosa mapato kutokana na kuporomoka kwa uzalishaji wa tumbaku.
Akitoa mfano anasema kwa misimu mitatu iliyopita zao hilo limeporomoka umaarufu wake wa kutoka kilo milioni nane hadi kufikia milioni mbili na hana uhakika kama msimu huu wanaweza kubahatisha hata kilo milioni mbili. Anasema wanunuzi kwa upande wao wamekuwa wakitekeleza wajibu wao na wala hawadaiwi, lakini mchezo unaofanywa kati ya benki na vyama vya ushirika umesababisha wakulima kupoteza imani na zao hilo na hivyo kuacha kulilima.
Akifafanua anasema kinachoonekana katika makaratasi ya mikopo ni takwimu kuchezewa na wajanja wachache, kisha benki kuvilipa vyama vya msingi fedha nyingi ambazo haziendani na ainisho la mkutano mkuu kuhusu kiasi cha pembejeo wanachokihitaji.
“Mwisho wa siku yanazuka matatizo ya wakulima kutolipwa fedha sawa kwa jasho lao, matatizo yaliyosababishwa na mikopo ambayo imetolewa na mabenki kinyume na wakulima wanaoishia kubebeshwa mzigo mkubwa wasiostahili,” anasema.
Anasema maagizo ya vyama vya ushirika kukopa katika benki za Namtumbo yamelenga kuijengea uwezo halmashauri kufuatilia mapato yanayotokana na zao hilo pamoja na matatizo yanayoambatana na mikopo hiyo sambamba na marejesho yake.
“Tulipoomba lianzishwe hili tawi hapa sababu ilikuwa kusaidia kilimo cha tumbaku, ili wanaonunua waweze kuwalipa wakulima kwa mujibu wa mkataba na halmashauri yetu ijue hilo, lakini wakopeshaji wamekuwa wajanja na wanafanya kila hila kudidimiza kilimo hiki,” anasema Lutav.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu anasema maamuzi ya Wilaya ya Namtumbo yamekuja wakati muafaka kwani yanalenga kuliinua zao la tumbaku ambalo ndilo msingi wa uchumi wa wilaya. Anasema vyama vya msingi vitaendelea kukopa benki kwa jinsi taratibu zao zinavyotaka na Serikali inachofanya ni kuhakikisha kwamba wakulima wanapata jasho lao na si wajanja kuwafanyisha kazi na wao kuneemeka kwa mgongo wa wakulima.
Mkoa wa Ruvuma umekuwa na vikao kadhaa vya maendeleo vilivyojadili madeni ya vyama vya ushirika na juhudi za kuondokana nayo mara moja na suala la uaminifu wa wafanyakazi wa benki lilijadiliwa sana hasa kutokana na vyama vya msingi vya Namtumbo vipatavyo 29 vingi kuonekana maombi yake ya mikopo kuna walakini.
“Tuligundua kwamba hati za maombi ya mikopo zilikuwa zimefutwa futwa kutoka katika maelekezo ya awali na kuongezewa kiwango kingine, tofauti na maamuzi ya mikutano mikuu ya vyama hivyo vya msingi,” anasema na kuongeza kwamba hayo ndiyo mambo wanayolenga kuyakomesha.
Katika siku za karibuni Serikali imevunja APEX ambayo ilikuwa inalalamikiwa kwa kuongeza mzigo wa madeni kwa wakulima wa tumbaku katika mikoa inayolima tumbaku kwa wingi. Mikoa hiyo ni Tabora na Shinyanga ambapo kwa Shinyanga wilaya inayolima zao hilo ni Kahama. Mikoa mingine inayolima tumbaku ni Mbeya ambako inalimwa katika Wilaya ya Chunya huku katika Mkoa wa Ruvuma tumbaku ikilimwa hasa katika Wilaya ya Namtumbo.
Miaka iliyopita kampuni zinazonunua tumbaku ndiyo yaliyokuwa yanatoa pembejeo kwa wakulima na kuja kukutana baada ya mavuno. Hata hivyo, baadaye ilionekana kama kuna tatizo kati ya wakulima na kampuni hizo ambapo ikakubalika kwamba vyama vya msingi kuwawezesha wakulima katika kilimo na wakishauza tumbaku kuwapatia wao fedha.
Ukopaji pembejeo za tumbaku Namtumbo wawekewa masharti
Chanzo;Habari Leo


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa