Kapteni Mstaafu Robert: Sitasahau nilipohukumiwa maisha jela

 
Rubani wa ndege aliyeonja kifo kwa ajali ya ndege na kifungo cha maisha, Rubani huyu ni Kapteni Mstaafu Rodrick Robert (69). 

Nje kidogo ya Mji wa Songea, kipo kijiji kinachoitwa Mateka. Bila shaka jina la kijiji hicho lina historia yake, lakini kubwa ni kwamba ndiko anakoishi rubani wa ndege aliyeonja kifo kwa ajali ya ndege na kifungo cha maisha.
Rubani huyu ni Kapteni Mstaafu Rodrick Robert (69) mrefu, mweupe ambaye si mnene na wala si mwembamba akiwa na nywele laini zinazoashiria wazi kwamba mmoja wa wazazi wake alikuwa mtu wa nje ya Bara la Afrika.
Ni mara ya kwanza kumwona alipokuwa akifungua mlango, lakini anatoka na tabasamu baada ya kuona wageni nje wakiwa na mkewe aitwaye May Daud Robert aliyeniongoza kufika hapo mara ya pili baada ya kumwomba aachie kidogo kazi yake mjini Songea na kunipeleka nyumbani kwake nikaonane na mumewe.
Kwa kweli ilikuwa mara ya pili kwangu kufika pale saa 11.00 jioni baada ya mara ya kwanza ya saa 4.00 asubuhi ya siku hiyo kuwakosa nilipopelekwa na msamaria kwa pikipiki mbili.
Robert anatukaribisha ndani huku akisema alipata taarifa za kuwapo kwa wageni wanaomtafuta tangu asubuhi. Tunaingia ndani na kufika kwenye sebule ikiwa na makochi ya kawaida na hatimaye Robert, mkewe na mimi tunaketi.
Akiwa anamwangalia mkewe aliyeketi upande wa kushoto kwake, Rubani Robert ananikaribisha.
Anasimulia kidogo historia yake.
Rubani: Nilizaliwa Mtaa wa Mtini mjini Songea mwaka 1944 na baba yangu alikuwa mhandisi wa kujenga barabara na nyumba za Serikali na alishiriki kujenga Uwanja wa Ndege za Jeshi Dar es Salaam.
Nilisoma chekechea mjini Songea, Shule ya Msingi Songea na Peramiho baadaye Sekondari ya Wavulana Songea kabla ya kujiunga St Michael ya Iringa ambayo baadaye ikawa Mkwawa Sekondari na sasa ni chuo.
Baada ya kumaliza Mkwawa nilingia Chuo Kikuu cha Dar e Salaam kuchukua Sayansi ya Jamii, lakini nilisoma mwaka mmoja nikaacha.
Mwandishi:Baada ya kuacha chuo kikuu ulikuwa unafanya nini?
Rubani:Nilikuwa nyumbani nikijishughulisha na uandishi na pia kuchora jambo ambalo lilinifanya niitwe kwenye mafunzo ya siku sita kuhusu uandishi Chuo Kikuu cha Makerere ambako nikawa mmoja wa watu wa kwanza tulioandika jarida la kwanza la chuo hicho. Niliporudi nchini nilipata kazi kwenye Shirika la British America Tobacco Company (BAT) ambako nilifanya kazi karibu mwaka mmoja na baadaye niliacha.
Mwandishi: Ni kwa nini uliacha?
Rubani: Sikumbuki.
Mwandishi: Baada ya hapo ulikwenda wapi?
Rubani: Nakumbuka mwaka 1970 nikiwa nyumbani Songea, alikuja Jenerali Luis ambaye alikuwa mwenyeji wa Mkoa wa Rukwa na kuniambia kwamba walikuwa wakihitaji vijana waliosoma ili wawe marubani wa jeshi. Hoja hiyo niliipenda na nikakubali, hivyo aliniandikisha na kunitaka niende kwenye mafunzo ya kijeshi (TMA) Dar es Salaam kwa ajili ya uofisa.
Nilimaza mafunzo kwenye kikosi cha anga Dar es Salaam na baada ya hapo pamoja na wenzangu karibu 14 tuliendelea na mafunzo ya kuendesha ndege kwa chini (Ground School) kwa mwaka mmoja na baada ya hapo tulianza mafunzo ya awali ya kurusha ndege.
Mwandishi: Tangu mafunzo hadi kuanza kazi, je uliwahi kupata ajali?
Rubani: Ndiyo, nilipata ajali mwaka 1978 nikiwasafrisha askari 26 kutoka Dar es Salaam kwenda Beira Nover Freesco Msumbiji ingawa sikujua askari wale walikuwa wakienda nchi gani. Sijui walikuwa wa Zimbabwe au Angola sijui. Injini ya kushoto ilizimika ghafla na baadaye injini ya kulia ikazima hivyo nililazimika kutua kwenye shamba dogo porini na askari wote tulitoka salama isipokuwa mmoja alipata michubuko kutokana na bawa la ndege kugonga kichuguu. Kipande hiki (anainuka kuchukua na kukionyesha kichuma cha bawa la ndege) nilipewa kama kumbukumbu.
Baada ya ajali hiyo, mwishoni mwa mwaka 1978 nilikwenda Uingereza kusoma utaalamu wa ndege aina ya Hauca Cidre748
.
Mwandishi:Je, vita dhidi ya Idd Amin Dada ulishiriki?
Ruban: Tangu mwanzo hadi mwisho mimi nilikuwa mmoja wa walioshiriki mchana na usiku hadi vilipoisha.

Mwandishi: Unakumbuka nini kwenye vita hivyo?
Rubani: Nakumbuka siku moja nilikuwa off (napumzika kidogo), nikaamua kunywa bia. Na ratiba ilikuwa ikionyesha nitakuwa kazini kesho yake. Lakini ghafla kiongozi wangu alinijia na kunitaka nirushe ndege. Mimi nilikataa katakata kwa sababu nilikuwa nimekunywa pombe. Niliwahi kumwendesha Nyerere.
Mwandishi: Je, ni kweli ulimwendesha Nyerere? Na kazi ya jeshi iliendelea hadi lini?
Rubani: Ni kweli baada ya vita vya Amini niliendelea kurusha ndege za jeshi na pia kufanya kazi ya kuendesha ndege ya Rais Nyerere. Mwaka 1983 Januari 7, nilikamatwa na wanajeshi wengine wengi kwa tuhuma za uhaini. Tulidaiwa tulitaka kumuua Rais Julius Nyerere. Nilikamatwa nikiwa eneo la Airwing Dar es Salaam. Tulikaa kizuizini hadi Julai mwaka 1983 Mahakama ilipotangaza kwamba hatukuwa na kesi ya kujibu. Lakini cha kushangaza mwaka 1985 watu tisa kati ya wale walioshikiliwa mara ya kwanza, tulikamatwa tena na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kutaka kumuua Rais Nyerere.
Mwandishi: Je, kiukweli mpango huo ulikuwapo?
Rubani. Aaa...ulikuwapo haukuwapo, ‘it was planned by high official (ulipangwa na baadhi ya maofisa za ngazi za juu)’, unajua baada ya vita vya Uganda nchi ilikuwa imefilisika. Haikuwa na unga, sabuni, sukari na hata nguo, karibu kila kitu hakikuwapo. Hivyo Watanzania wengi walikuwa wamechanganyikiwa na hali ile.
Mwandishi: Kwa maana hiyo mpango huo ungefanikiwa je bidhaa hizo zingeonekana?
Rubani: Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliiokoa nchi baada ya kuruhusu kila kitu kiingie nchini hata bila ya kutoza kodi. Mwinyi aliituliza nchi. Pia Serikali iligundua kwamba waliokamatwa walitaka mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kuishtua CCM ambayo ilikuwa imejisahau na hivyo kuanzishwa kwa vyama vingi jambo ambalo lilitekelezwa baadaye.
Mwandishi: Matatizo yaliyokuwapo enzi hizo na sasa unatofautishaje?
Rubani:Kama nilivyosema, enzi za Nyerere nchi ilifilisika, Mzee Mwinyi aliiokoa nchi, Rais Mkapa akaweka msingi wa kukusanya kodi, hivi sasa sijui kinachoendelea kwa kuwa sisomi sana magazeti kwani sina fedha za kununua.
Mwandishi: Mama Robert ulifanikishaje safari yako kurudi Songea. ?
Mkewe: Mimi niliposikia anafungwa maisha nilipigwa na butwaa na simanzi kubwa. Hivyo sikuwa na nguvu, lakini cha ajabu, baada ya saa 12 kupita, mkuu wa kikosi aliniita na kunitaka niondoke kwenye nyumba ndani ya saa 24. Kumbuka wakati ule mimi nilikuwa nafundisha Chuo Cha Utumishi Magogoni Dar es Salaam, hivyo nilihitaji kupata nafasi ya kuomba uhamisho na kufunga mizigo. Lakini mambo ya jeshi ni amri na nilitolewa mizigo ili nisafirishwe kwa ndege ya Jeshi ambayo nayo iliharibika. Lakini kwa bahati ilipona kabla ya saa 12 kumalizika, nikatakiwa nitaje niende wapi.

Suala hilo lilinifanya nitaje Songea kwa vile nilikuwa na watoto sita na Robert na watoto walikuwa wakiwafahamu ndugu wa Songea.
Hivyo mizigo na watoto walisafiri kwa ndege mimi nikabaki Dar es Salaam nikiomba uhamisho wa kwenda kufundisha Shule ya Sekondari ya Songea Wasichana.
Kwa kweli ilikuwa fedheha kubwa. Serikali inampenda mfanyakazi mzuri, lakini huyohuyo akiteleza kidogo ni takataka. Ipo haja ya kubadilisha msimamo huo.
Mwandishi: Kwako rubani, je unalo neno kwa Serikali?
Rubani:Aaaa , tangu nifike huku sijapata na wala sina senti ya Serikali. Wapo wenzangu waliosema eti Serikali inafikiria kutupatia chochote, lakini mpaka sasa sijasikia lolote.
Mwandishi: Kwa sasa afya yako ikoje na unajishughulisha na nini?
Rubani. Afya yangu nashukuru Mungu naendelea vyema, mambo mengine Mungu anasaidia.
Kapteni Mstaafu Rodrick Robert anasema ni suala la msingi kwa watu kuwa na moyo wa kulitumikia taifa kwani ndio msingi wa kuhakikisha tunakuwa na taifa lenye maendeleo makubwa.
“Jambo la msingi ambalo napenda kusisitiza ni moja tu kwamba kwa kila kitu ambacho mtu anafanya, anapaswa kuweka mbele maslahi ya taifa kwanza,” anasisitiza akiwaasa Watanzania kujenga tabia ya kuheshimu mila na tamaduni za taifa, pia kujali maadili ya uongozi.
Aidha anawashauri vijana kufanya kazi kwa bidii ili kuharakisha maendeleo nchini, kwani vijana ndio tegemeo kubwa kwa taifa na ulimwengu kwa ujumla kwa vile wana nguvu za kutosha.
Chanzo;Mwananchi.

Kigogo wa UVCCM akanusha kuhusika na January Makamba


Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba
Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kupitia Mkoa wa Ruvuma, Halfan Kigwenembe, amesema kuwa hakuhusika kwa namna yoyote na mapokezi ya Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba, mjini Songea.
Makamba alikwenda mjini Songea, mkoani Ruvuma katikati ya mwezi huu na kukutana na baadhi ya wafanyabiashara ambao inadaiwa aliwaomba wamuunge mkono katika nia yake ya kugombea urais mwaka 2015.

Katika toleo la gazeti hili Novemba 18, mwaka huu tulichapisha habari iliyokuwa na kicha cha habari “January Makamba atinga Songea kusaka urais” huku Kigwenembe akitajwa kuwa alihusika kuwakaribisha wafanyabiashara hao kwenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kukutana na Makamba.

Akitoa ufafanuzi kwa gazeti hili kuhusiana na ziara ya Makamba, Kigwenembe alisema kuwa hakushiriki kwa namna yoyote katika ziara ya Makamba, ikiwamo kuwapokea wafanyabiashara katika ukumbi wa mikutano.

Kada huyo alisema kuwa wakati huo alikuwa nje ya Songea kwa shughuli zake za biashara.

 “Nilikuwa Dar es Salaam, tiketi za hoteli na ndege ninazo, kwa hiyo ieleweke kwamba sikushiriki kwa namna yoyote katika shughuli hiyo,” alisema Kigwenembe.
CHANZO: NIPASHE



MTOTO WA MAIAKA 5 AJERUHIWA VIBAYA NA PANGA AKIMTHUMU KUIBA MAPERA HUKO SONGEA.


Mtoto Benson Tole akiwa na mama yake MTOTO Mmoja BENSON TOLE mwenye umri wa miaka Mitano mkaz...


Mtoto Benson Tole akiwa na mama yake
MTOTO Mmoja BENSON TOLE mwenye umri wa miaka Mitano mkazi wa Ruhuwiko mjini Songea mkoani Ruvuma, amenusurika kifo baada ya kukatwakatwa kwa kitu chenye ncha kali sehemu za usoni na Mzee mmoja LONGINUS HAULE mwenye miaka 51 akimtuhumu mtoto huyo kumuibia matunda aina ya Mapera shambani kwake. 

Mtoto BENSON TOLE kwa sasa amelazwa katika hospitali ya mkoa mjini Songea katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU), Madaktari wanaendelea kunusuru uhai wa mtoto huyu baada ya kupata mashambulio makali ya kucharangwacharangwa na kitu chenye ncha kali sehemu za usoni na mtuhumiwa mmoja LONGINUS HAULE mkazi wa Polisi Lizaboni mjini Songea. 

Mzee HAULE anatuhumiwa baada ya kumfanyia unyama wa kutosha mtoto huyo na kisha kupoteza fahamu akimtuhumu kumuibia matunda aina ya mapera shambani kwake alimtupia kwenye nyumba moja ambayo haijaisha ujenzi wake akidhani tayari ameshamuua. 
Afisa Muuguzi wa Hospitali ya mkoa mjini Songea, JOSEPH MTEWELE amesema kwa sasa mtoto huyo yupo chini ya uangalizi maalumu na kwamba madaktari wanaendelea na jitihada za kunusuru uhai wake kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata sehemu za kichwani. Jeshi la polisi mkoani Ruvuma limetihibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba linaendelea kuchukua hatua zaidi za kumfikisha Mzee LONGINUS HAULE kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi. 

Credit: Emmanuel Msigwa Channel Ten Songea.

CHANZO BLOG YA JESTINA GEORGE







Ukopaji pembejeo za tumbaku Namtumbo wawekewa masharti

SERIKALI wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma imeanza kuchukua hatua za kuzuia kuporomoka kwa kasi kwa zao la tumbaku kunasababishwa na kuchezewa kwa hesabu za mikopo hivyo kumbebesha deni hewa mkulima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Rajab Lutav na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu wamesema kwa kuanzia wamepiga marufuku vyama vya tumbaku wilayani humo kukopa katika benki zilizo nje ya Namtumbo.
Wanasema uozo huo unaolalamikiwa na wakulima unafanywa kwa ushirikiano kati ya maofisa wa benki zinazokopesha wakulima pembejeo na viongozi wa vyama vya ushirika. Mkuu wa Wilaya ya Namtombo, Rajab Lutav anasema lengo la hatua hizo ni kurejesha matumaini ya wakulima yaliyovia kutokana na kuzidiwa na madeni hewa huku wilaya yake ikizidi kukosa mapato kutokana na kuporomoka kwa uzalishaji wa tumbaku.
Akitoa mfano anasema kwa misimu mitatu iliyopita zao hilo limeporomoka umaarufu wake wa kutoka kilo milioni nane hadi kufikia milioni mbili na hana uhakika kama msimu huu wanaweza kubahatisha hata kilo milioni mbili. Anasema wanunuzi kwa upande wao wamekuwa wakitekeleza wajibu wao na wala hawadaiwi, lakini mchezo unaofanywa kati ya benki na vyama vya ushirika umesababisha wakulima kupoteza imani na zao hilo na hivyo kuacha kulilima.
Akifafanua anasema kinachoonekana katika makaratasi ya mikopo ni takwimu kuchezewa na wajanja wachache, kisha benki kuvilipa vyama vya msingi fedha nyingi ambazo haziendani na ainisho la mkutano mkuu kuhusu kiasi cha pembejeo wanachokihitaji.
“Mwisho wa siku yanazuka matatizo ya wakulima kutolipwa fedha sawa kwa jasho lao, matatizo yaliyosababishwa na mikopo ambayo imetolewa na mabenki kinyume na wakulima wanaoishia kubebeshwa mzigo mkubwa wasiostahili,” anasema.
Anasema maagizo ya vyama vya ushirika kukopa katika benki za Namtumbo yamelenga kuijengea uwezo halmashauri kufuatilia mapato yanayotokana na zao hilo pamoja na matatizo yanayoambatana na mikopo hiyo sambamba na marejesho yake.
“Tulipoomba lianzishwe hili tawi hapa sababu ilikuwa kusaidia kilimo cha tumbaku, ili wanaonunua waweze kuwalipa wakulima kwa mujibu wa mkataba na halmashauri yetu ijue hilo, lakini wakopeshaji wamekuwa wajanja na wanafanya kila hila kudidimiza kilimo hiki,” anasema Lutav.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu anasema maamuzi ya Wilaya ya Namtumbo yamekuja wakati muafaka kwani yanalenga kuliinua zao la tumbaku ambalo ndilo msingi wa uchumi wa wilaya. Anasema vyama vya msingi vitaendelea kukopa benki kwa jinsi taratibu zao zinavyotaka na Serikali inachofanya ni kuhakikisha kwamba wakulima wanapata jasho lao na si wajanja kuwafanyisha kazi na wao kuneemeka kwa mgongo wa wakulima.
Mkoa wa Ruvuma umekuwa na vikao kadhaa vya maendeleo vilivyojadili madeni ya vyama vya ushirika na juhudi za kuondokana nayo mara moja na suala la uaminifu wa wafanyakazi wa benki lilijadiliwa sana hasa kutokana na vyama vya msingi vya Namtumbo vipatavyo 29 vingi kuonekana maombi yake ya mikopo kuna walakini.
“Tuligundua kwamba hati za maombi ya mikopo zilikuwa zimefutwa futwa kutoka katika maelekezo ya awali na kuongezewa kiwango kingine, tofauti na maamuzi ya mikutano mikuu ya vyama hivyo vya msingi,” anasema na kuongeza kwamba hayo ndiyo mambo wanayolenga kuyakomesha.
Katika siku za karibuni Serikali imevunja APEX ambayo ilikuwa inalalamikiwa kwa kuongeza mzigo wa madeni kwa wakulima wa tumbaku katika mikoa inayolima tumbaku kwa wingi. Mikoa hiyo ni Tabora na Shinyanga ambapo kwa Shinyanga wilaya inayolima zao hilo ni Kahama. Mikoa mingine inayolima tumbaku ni Mbeya ambako inalimwa katika Wilaya ya Chunya huku katika Mkoa wa Ruvuma tumbaku ikilimwa hasa katika Wilaya ya Namtumbo.
Miaka iliyopita kampuni zinazonunua tumbaku ndiyo yaliyokuwa yanatoa pembejeo kwa wakulima na kuja kukutana baada ya mavuno. Hata hivyo, baadaye ilionekana kama kuna tatizo kati ya wakulima na kampuni hizo ambapo ikakubalika kwamba vyama vya msingi kuwawezesha wakulima katika kilimo na wakishauza tumbaku kuwapatia wao fedha.
Ukopaji pembejeo za tumbaku Namtumbo wawekewa masharti
Chanzo;Habari Leo


Kampuni 12 zaruhusiwa kununua korosho

KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imezipitisha kampuni 12 kuchuana katika ununuzi wa korosho za wakulima zikiwa ni juhudi za Serikali kuwaondolea kero hiyo.
Pamoja na maamuzi hayo, pia Kamati hiyo imetakiwa kuwalipa wakulima Sh 1,100 au zaidi kwa kilo moja na kwamba mfumo huo hautaruhusu utaratibu wa kuwakopa wakulima hao kuanzia Novemba 22 mwaka huu.
Akitangaza maamuzi hayo, Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho alisema maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao kilichoketi Novemba 21 mwaka huu.
Nalicho amewatahadharisha walanguzi walionunua korosho hizo kutoka kwa wakulima kwa kupitia vipimo haramu vya kangomba kuwa hawatapewa mwanya wa kuuza wala kusafirishaa korosho hizo kutoka nje ya wilaya hiyo na kwamba atakayenaswa Sheria itafuata mkondo wake.
Katika taarifa hiyo, Nalicho alizitaja kampuni hizo kuwa ni Export Trading Co. Limited, Prayosa, Kulaathool Co. Ltd, Shareeji Impex Ltd, Saidi Mohamed Said pamoja na Kampuni Kongwe ya Olam Tanzania Ltd.
Nyingine ni China Pesticide Tanzania Ltd, Amina Seti, Saweya Impex Tanzania Ltd, Alpha Choice Ltd, Sunrise Commodities pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa korosho Wilayani Tunduru (TAMCU Ltd).
Chanzo;Habari Leo




KINANA ATEMBELEA WILAYA YA SONGEA VIJIJINI‏

 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akipokelewa na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Ndugu Jestina Mhagama mara baada ya kuwasili katika eneo la Seminari Kuu wilaya ya Peramiho.
 Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Dk.Asha-Rose Migiro akisalimiana na Mbunge wa Peramiho Ndugu Jenista Mhagama .
 Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana akiwa kwenye mavazi ya jadi yajulikanayo kama Mgolole na kukabidhiwa silaha za jadi alipowasili katika kijiji cha Peramiho B.

 Wanachama wa shina namba 28 wakishangilia hotuba ya  Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana ambaye yupo kwenye ziara ya kukagua uhai wa chama katika Mkoa wa Ruvuma.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akinywa chai nyumbani kwa Balozi wa Nyumba 10 Issa Said,Katibu Mkuu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mabalozi wa nyumba 10 wanatembelewa na viongozi wa ngazi zote.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana pamoja na viongozi na wananchi wa Peramiho wakishiriki kubeba matofali ya ujenzi wa Zahanati ya Kahegwa.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akizungumza na wananchi wa kata ya Kahegwa baada ya kushiriki shughuli za kubeba matofali kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Kahegwa,Katibu Mkuu aliwaeleza wananchi hao kuimarisha moyo wa kujitegemea  kwani maendeleo ya Tanzania yataletwa na Watanzania wenyewe na si wahisani.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana  akizungumza na mmoja wa wananchi aliyefarijika sana kwa kumsikia Katibu Mkuu akizungumza maneno ya msingi na yenye kutia moyo sana hasa katika suala la kujitegemea.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akipanda mti kwenye zahanati ya Lusonga ambayo kwa asilimia kubwa imejengwa kwa nguvu za wananchi.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana ,akiwa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Ndugu Jenista Muhagama ,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Ndugu Oddo Mwisho na wakikata utepe wa kufungua jengo la Zahanati ya   Lusonga.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akisiliza taarifa ya kikundi cha akina mama wajasiriamali  watengeneza sabuni ambayo ilisomwa na Fransisca Andrea.
 Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana akiweka jiwe la msingi la jengo la  Ofisi ya tawi la Mlandizi, Peramiho wilaya ya  Songea vijijini.
 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akihutubia wakazi wa Peramiho ,wilaya ya Songea Vijijini  mkoani Ruvuma.
 Mbunge wa Jimbo la Peramiho  Ndugu Jestina Muhagama akihtubia wakazi wa Peramiho na kuzungumzia matatizo sugu yanayo wasunbua wananchi wa jimbo lake hasa ukosekanaji wa Pembejeo na kutolipwa pesa wanayodai serikali kwa wakati.

 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akihutubia wananchi wa Peramiho ambapo aliwapongea kwa kuwa wakulima wazuri


 Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Dk.Asha-Rose Migiro akiwa kwenye picha ya pamoja na Katibu Tarafa Ndugu Salima Mapunda baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara.



 Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana akikata utepe kama ishara ya kufungua jengo la CCM Tawi la Masangu.
 Katibu Mkuu wa CCm Ndugu Abdulrahman Kinana akisalimiana na masista  kutoka kanisa katoliki la Chikole,jimbo la Peramiho.


ZAIDI YA WANACHAMA 300 KUTOKA UPINZANI WAJIUNGA NA CCM PERAMIHO‏


 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana akiwapokea wanachama zaidi ya 300 kutoka vyama vya upinzani ambao wameamua kujiunga rasmi na CCM, ziara hii ya Katibu Mkuu wa CCM imekuwa na mafanikio ya hali ya juu kwani kila anapomaliza kuhutubia mamia ya wapinzani wanarudisha kadi.
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akimpa mkono wa pole Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Songea Vijijini Ndugu Neli Due aliyepata matatizo ya kupooza mkono na mguu,nyumbani kwake mtaa wa Mtakuja  Bombanbili.

January atinga Songea kusaka urais

Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Tekenolojia,January Makamba
 
Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Tekenolojia, January Makamba amekutana na baadhi ya wafanyabiashara mjini hapa Mkoa wa Ruvuma  ambao inadaiwa amewaomba wamuunge mkono katika nia yake ya kugombea urais mwaka 2015.
Hayo yamefahamika mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya January ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kudai kufanya kikao na wafanyabiashara hao   kwenye hoteli  ya TOP ONE INN iliyopo Msamala Manispaa ya Songea.

Inadaiwa kuwa January aliwaangukia wafanyabiashara hao kwa kuwaomba kuwa kipindi cha uchaguzi kitakapofika, wamsaidie kumpa ushirikiano ili ashinde katika kinyang'anyiro cha urais.

Baadhi ya wafanyabiashara waliliambia NIPASHE  kwa masharti ya kutotajwa majina yao gazetini kuwa    muda mfupi kabla ya kikao hicho kufanyika, walipigiwa simu wakitaarifiwa kuwa wanahitajika kwenye hoteli hiyo kwa mazungumzo.

Walisema walipofika kwenye eneo la hoteli hiyo, walikaribishwa kwenye ukumbi wa mikutano na kigogo mmoja wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ambaye walimtaja kwa jina la Halfan Kigwenembe.

Walisema wakiwa kwenye ukumbi huo, kikao kilianza baada ya mmoja wa wafanyabiashara hao kusimama na kumtambulisha kiongozi huyo na  kuelezea lengo la kuwaita baadhi yao.

Alisema wafanyabiashara hao waliofika kwenye kikao hicho walianza kuwa na maswali mengi wakitaka kujua kwanini waitwe wao badala ya kufuata utaratibu.

Alisema baadaye Janaury alipewa nafasi ya kujieleza akisema amefika mjini Songea kukutana na wafanyabiashara hao akiwa na lengo la kuomba aungwe mkono kipindi uchaguzi mkuu utakapofika.

Alisema wafanyabiashara wengine walimuuliza maswali ambayo yalimtaka kiongozi huo atoe ufafanuzi wa sababu za kuchukua uamuzi kama huo mapema hivyo kabla ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake na CCM kutangaza kuanza kumsaka mgombea wake wa urais.

Pia alihojiwa kama haoni wadhifa wake wa Naibu Waziri na majukumu aliyonayo hauonyeshi kuwa hana uwezo mkubwa wa kufikia kuomba nafasi ya kuongoza nchi.

Alisema walimtolea mfano kuwa haoni kuwa hana ubavu katika kuchapa kazi kama mawaziri wa Uchukuzi,  Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Ujenzi,  Dk. John Mgufuli ambao wamemudu vilivyo nafasi walizopewa na Rais Kikwete na Watanzania, hivyo yeye hana cha kuonyesha kwa Watanzania.

Mpashaji wa habari hizi alisema kuwa January alisema serikali ya awamu ya nne inafahamu kwa dhati umuhimu wake na kuwa kwenye kampeni ya uchaguzi mkuu wa 2010 yeye alikuwa ni mmoja wa wanakamati wa kumsaidia Kikwete kuhakikisha  anashinda na kufanikiwa.

Alisema alidai ndiye aliyekuwa akiandika ratiba za kampeni na hotuba za mikutano ya kampeni aliyokuwa akifanya Kikwete katika majimbo mbalimbali nchini,  hivyo anazo sifa za kutosha kugombea nafasi urais kwa mwaka 2015.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya CCM Songea Mjini, Gerald Mhenga, alipohojiwa na NIPASHE kwa njia ya simu kuhusu ujio wa January, alisema hana taarifa kwa sababu hakupitia ofisini kwake.

Mhenga alisema kama kweli January ana nia ya kugombea urais kupitia CCM hasingeweza kukwepa kufika ofisi za Chama hicho labda atagombea kupita vyama vingine.
Naye Katibu wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma, Velena Shumbusho, alipohojiwa na NIPASHE kwa njia ya simu,  alisema hana taarifa za ujio huo wala za kikao chake na wafanyabiashara hao.
Hata hivyo, Shumbusho alikataa kuzungumzia kwa undani kwa madai kuwa yupo katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM wa Taifa, Abdallahiman Kinana.
Kwa upande wake, January alipohojiwa na NIPASHE kwa simu alithibitisha kufika mjini Songea na kukutana na wafanyabiashara hao.
Alifafanua kuwa alifanya hivyo baada ya wafanyabiashara hao kumuita kwa lengo la kuwasilisha malalamiko yao na kufanya nao mazungumzo kwa muda mrefu kujadili ajenda nne walizompelekea.

Alitaja malalamiko hayo kuwa ni kuhangaishwa kwa kubebeshwa mahindi kutoka vijijini hadi kwenye  Hifadhi ya Taifa ya Chakula (SGR) mjini Songea na yakifikishwa hapo wanatafutwa wafanyabiashara wakubwa kuyapeleka mikoa mingine ikiwamo Dar es Salaam na Dodoma.

Alisema wafanyabiashara hao walimlalamikia kuwa kitendo hicho kinaashiria kuwapo kwa mianya ya rushwa zinazotolewa na wafanyabiashara wakubwa kwa baadhi ya viongozi wa kitengo hicho na serikali.

Kuhusu kugombea urais, January alisema aliombwa na wafanyabiashara hao kujitosa katika kinyang'anyiro hicho mwaka 2015, lakini aliwajibu  wakati ukifika ataangalia kama ataamua au.

Alisema aliwataka wafanyabiashara hao kuvuta subira kwa madai kuwa kwa sasa bado ni mapema mno kuzungumzia kama ana dhamira hiyo au la.

"Ndugu mwandishi mimi niliitwa na wafanyabiashara wenyewe na waliniomba niwape ukweli kama ninahitaji kugombea urais 2015, lakini mimi sikuja kutafuta watu wa kunisaidia kugombea," alisisitiza.

NIPASHE ilizungumza na Kigwenembe kwa njia ya simu juu ya kuratibu mkutano wa January, alithibitisha Naibu Waziri huyo kufika Songea na kukutana na baadhi ya wafanyabiashara na kukataa kuzungumzia zaidi akidai hakuwapo kwenye kikao hicho.

Ujio wa January mji hapa na kikao hicho na wafanyabiashara hao, umeacha maswali kwa baadhi ya wananchi na wanasiasa wakihoji kuwa wizara yake haina dhamana ya kufanya hivyo.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti walisema wanajiuliza maswali mengi kwa sababu hana dhamana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Biashara na Viwanda na Wizara ya Uchukuzi ambazo kwa namna moja au nyingine zingeweza kupelekewa malalamiko hayo na kuyapatia ufumbuzi.
CHANZO: NIPASHE

KINANA AFANYA MKUTANO WA HADHARA NA WANANCHI WA NAKAPANYA WILAYANI TUNDURU MKOANI RUVUMA,AWAHIDI KUMALIZA TATIZO LA BEI YA KOROSHO.

 Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Abdulrahman Kinana akitolea ufafanuzi wa kina kwa Wakazi wa kijiji cha Nakapanya Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma mapema leo jioni,kuhusiana na tatizo sugu la bei ya zao la Korosho kwa wakulima,ambao wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu,Kinana aliwahakikishia Wanachi hao kuwa tatizo hilo watalifanyia kazi ipasavyo na kufikia hatua ya kulimaliza kabisa. 

Aidha tatizo hilo ni kubwa kwa upande wa mikoa ya Kusini,ikiwemo Mtwara,Lindi na Ruvuma.Kinana alibainisha kuwa CCM kitahakikisha suala la hilo linashughulikiwa kwa umakini  mkubwa ikishirikiana na Serikali sambamba na sambamba na taasisi zinazohusika na zao hilo,ili kukomboa uchumi wa Wananchi wa eneo hilo hasa kwa kuhakikisha viwanda vya kubangua korosho vinajengwa na vile ambavyo vimebinafsishwa na havifanyi kazi kunaandaliwa utaratibu ambao utawafanya wawekezaji wengine kupewa ili vifanye kazi na kutatua tatizo la bei ndogo ya zao hilo inayolipwa na wanunuzi. 

Katika ziara hiyo hiyo Kinana ameongozana na Katibu wa NEC siasa,Itikadi na uenezi Ndugu Nape Nnauye na Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Dkt.AshaRose Migiro. 
 Baadhi ya Wakazi wa kijiji cha Nakapanya Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakishangilia jambo mara baada ya Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Abdulrahman Kinana,kuzungumzia na kufafanua vyema kuhusiana na tatizo kubwa lililopo kwenye zao la Korosho,ambako kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ikiwemo suala la bei ya ununuzi wa Korosho kuwa ndogo,malipo kutokulipwa kwa wakati kwa wakulima na mengineyo.
Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini ,Mh.Ramo Matalla Makani akielezea baadhi ya matatizo yanayoisumbua Wilaya hiyo kwa Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Kinana  (pichani kulia) mapema leo,katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Nakapanya,Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.Kinana na ujumbe wake wataanza ziara yao rasmi leoo Wilayani humo mkoani Ruvuma kwa madhumuni ya kuimarisha chama na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa Ilani ya CCM,katika Mikoa ya Ruvuma na Mbeya.
Baadhi ya Wakazi wa kijiji cha Nakapanya Wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakiwa wamekusanyika mapema jana wakimsikiliza Katibu Mkuu wa CCM,Ndugu Abdulrahman Kinana,alipokuwa akizungumza nao kuhusiana na ufumbuzi wa matatizo yao mbalimbali ikiwemo suala la huduma za afya,Barabara,Maji sambamba na tatizo sugu la zao la Korosho wilayani humo.
Michuzi blog

Wanafunzi wamtaka mkuu wa chuo cha ualimu aachie ngazi



WAKUFUNZI na wafanyakazi wa Chuo cha Ualimu Songea, wameilalamikia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kitendo cha kushindwa kushughulikia mgogoro uliopo chuoni hapo na kusababisha shughuli mbalimbali za kiutendaji kudorora.
Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao wameelezea hofu ya kutofanikisha mpango mkakati wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa na kuitaka serikali kumuondoa madarakani Mkuu wa Chuo hicho, Ubaya Suleiman, ili kukinusuru chuo hicho.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa wanafunzi hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, walisema kuwa katika chuo hicho kuna mgogoro ambao umeshindwa kuchukuliwa hatua na kusababisha amani na utulivu kukosekana chuoni hapo kwa zaidi ya miezi saba sasa.
Walisema kuwa mgogoro huo umetokana na uongozi mbovu usiozingatia misingi ya uongozi na demokrasia katika vyuo vya ualimu nchini kwani mkuu wa chuo hicho, amekuwa mbabe, lugha chafu na mtu wa vitisho kwa wafanyakazi na wanachuo.
“Pamoja na hayo, mkuu huyo wa chuo amediriki kuwapeleka baadhi ya wafanyakazi wake kwenye vyombo vya dola (polisi), akiwatuhumu kuwa wanataka kumuua.
“Baada ya mgogoro huo kutopata suluhu kupitia vikao vya ndani, jitihada zifuatazo zilifanyika na wafanyakazi wa chuo hicho ili kuleta hali ya amani na utulivu.”
Walifafanua kuwa Aprili 27 mwaka huu, walifanya kikao na mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, Mei 15 na Juni mosi mwaka huu, walifanya kikao na bodi ya ushauri ya chuo, hata hivyo suluhu ya mgogoro huo haikupatikana.
Walisema kuwa kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome aliunda tume ya watu watano ikiongozwa na mkaguzi mkuu wa shule na vyuo wa nyanda za juu kusini ambaye alifahamika kwa jina moja la Lyapambile, kuja kufanya utafiti wa chanzo cha mgogoro, lakini mpaka sasa tume hiyo haijatoa majibu ya uchunguzi wa jambo hilo.
“Hata hivyo wakufunzi hawakuishia hapo Agosti 13, 2013 walifanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu, ambaye baada ya kusikiliza mgogoro huo aliahidi kuleta suluhisho la kudumu mapema iwezekanavyo ili kuleta amani na utulivu chuoni hapo. Lakini cha kushangaza hadi sasa yapata miezi mitatu hakuna kilichofanyika hali ambayo imeendelea kuwavunja moyo wafanyakazi wa chuo hicho,” walisema.
Mkuu wa chuo hicho, Ubaya Suleiman, alipoulizwa kuhusu mgogoro huo, alisema hana jambo la kuzungumza kwani mgogoro huo uko kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hivyo hawezi kusema chochote.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo ambaye amejitambulisha kwa jina la H. Lugome ameonyesha masikitiko makubwa sana juu ya utendaji wa mkuu wa chuo hicho na kuahidi kukutana na wafanyakazi hao ili kuweza kufanya kikao cha mwisho cha majadiliano.
Naye Naibu Waziri wa Elimu Philipo Mulugo alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani, alisema swala hilo bado halijafika mezani kwake na endapo likifika basi atachukua hatua stahiki 

Chanzo;Tanzania Daima

WANAOTUMIA KADI ZA BIMA YA AFYA ZA WALIOKUFA KUCHUKULIWA HATUA


Mfuko wa Bima ya Afya Mkoani Ruvuma umefanikiwa kukusanya  kiasi cha Shilingi 182,573,809.36 sawa asilima 79 lengo likiwa kukusanya shilingi 228,668.000 kwa mwaka 2012 -2013

Meneja wa Bima ya Afya Mkoa wa Ruvuma  Siliveri Mgonja amesema hayo katika Mkutano wa wadau wa mfuko wa Afya ulio jumuisha wilaya tano za mkoa wa Ruvuma .

Akiwakilisha tarifa ya mafanikio na changamoto zinzo ikabili bima ya afya amesema moja ya changamoto ni pale wanapo fariki na vitambulisho vyao kutumika na familia iliyo baki.

Amesma hatua za kisheria zita chukuliwa kwa wale wote watakao bainika wa kitumia kadi za marehemu pia ameiomba serekari kutotoa fedha za mirathi mpaka kadi za Marehemu zirudishwe.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Saidi Thabiti Mwambungu amewataka watumishi wa serekari kuwa mfano bora kwa kuongoza kupima afya zao ili wananchi waige mfano wao wakujua afya zao.

Mganga Mkuu wa Hosipitali ya Mkoa wa Ruvuma Benedick  Ngaiza amesema Mfuko wa Bima ya Afya  unatakiwa kwenda na wakati kiwango kinacho tumilka cha malipo hakilingani na huduma zinazo tolewa akitoa mfano amesma huduma ya mama mja mzito bima hulipa shilingi 10.000/= lakini huduma hiyo kwa uhalisia ni shilingi 80,000

Mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi amesema Bima ya Afya ni mkombozi kwa wanyonge gharama wanazo lipa kwa familia moja ni kiasi kidogo sana amehimiza wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya

Hata hivyo wadau wa bima ya Afya walilalamikia upatikanaji wa dawa katika vituo vya Afya Vijijini na Mjini ,Halimashauri za miji na vjijini vime kuwa vikilipa fedha ndogo kwa waheshimiwa madiwani badala ya kulipa asilimia 6 hulipa asilimia 3 tu na kuacha mzigo mkubwa kwa mfuko wa bima ya afya.

HALI TETE CHUO CHA UALIMU SONGEA, WIZARA YA ELIMU YAMBEBA MKUU WA CHUO.


Ni takribani miezi nane sasa tangu nianze kufuatilia uendeshaji wa chuo cha Ualimu Songea kama kinaweza kuendana na kauli mbiu ya sasa ya Serikali ya Big Result Now (Matokeo Makubwa Sasa)
Nimelazimika kukifuatilia Chuo hicho kutokana na mgogoro mkubwa uliopo kati ya wafanyakazi (wakufunzi) na mkuu wao wa chuo Ubaya Suleiman.
Mgogoro huo umetokana na uongozi mbovu usiozingatia misingi ya uongozi na Demokrasia katika vyuo vya ualimu Tanzania kwani Mkuu huyo wa chuo amekuwa na lugha za matusi,vitisho kwa wafanyakazi na wanachuo, kutopokea ushauri kwa washauri wake, mbinafsi, kutowaamini watendaji wake kwa nafasi alizowateua, kufanya kazi kwa kutumia vyanzo visivyo rasmi, Matumizi mabaya ya fedha za Serikali na vyombo vya usafiri.(P.T)

Pamoja na hayo mkuu huyo wa chuo amediriki kuwapeleka baadhi ya wafanyakazi wake kwenye vyombo vya dola (polisi) (kuwatishia) akiwatuhumu kuwa wanataka kumuua. Baada ya mgogoro huo kutopata suluhu kupitia vikao vya ndani, Jitihada zifuatazo zilifanyika na wafanyakazi wa chuo hicho ili kuleta hali ya amani na utulivu wa chuo;
Tarehe 27/04/2013 walifanya kikao na mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, tarehe 15/05/2013 na tarehe 01/06/2013 walifanya kikao na Bodi ya ushauri ya Chuo, hata hivyo suluhu ya mgogoro huo haikupatikana.
Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome aliunda tume ya watu watano ikiongozwa na Mkaguzi Mkuu wa shule na vyuo wa nyanda za juu kusini ambaye alifahamika kwa jina moja la Lyapambile, kuja kufanya utafiti wa chanzo cha mgogoro, lakini mpaka sasa tume hiyo haijatoa majibu ya uchunguzi wa jambo hilo
Tume hiyo haikuishia hapo tarehe 13/08/2013 wafanyakazi walifanya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, ambaye baada ya kusikiliza mgogoro huo aliahidi kuleta suluhisho la kudumu mapema iwezekanavyo ili kuleta amani na utulivu(peace and Tranquility) chuoni hapo.
Lakini cha kushangaza hadi sasa yapata miezi mitatu hakuna kilichofanyika hali ambayo imeendelea kuwavunja moyo wafanyakazi wa chuo hicho.
Licha ya jitihada zilizofanywa, Mkuu huyo wa Chuo Ubaya Suleiman anaendelea kuwanyanyasa wafanyakazi wake na kusema pigeni kelele lakini wakuning'oa mimi hapa hayupo na lugha zingine ambazo sio za ustaarabu anazitoa, na kuwafanya wafanyakazi wenzake wahoji nguvu aliyonayo katika utendaji, mfano wa lugha zake mbovu ni "kwani mizizi yangu ni mirefu". Kitendo hicho kinawafanya wafanyakazi wa chuo na wadau wengine watilie mashaka juu ya sifa za uteuzi wake kushika nafasi kubwa kama hiyo.
Tunamuomba Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Shukuru Kawambwa na Naibu wake Philipo Mulugo kumuondoa mkuu huyo wa chuo madarakani na kumtafutia shughuli nyingine ya kufanya kwa ustawi wa chuo cha ualimu songea, taaluma ya ualimu Tanzania na ili kuleta ufanisi wa kauli mbiu ya serikali ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now)
Sababu zinazopelekea hilo ni nyingi ila kwa sasa nitazitaja chache ili kuweka kumbukumbu sawa, ya kwanza Novemba 1, 2013 Mkuu huyo wa chuo bila kuwasiliana na Mtaaluma wake wa Chuo Maiko Luoga, alidiriki kuwaandikia Barua Wakufunzi kuwataka watunge Mtihani wa Moko wa Ualimu viwango vya Baraza la Taifa la Mitihani(NECTA) kwa lugha ya kejeri hali ambayo imesababisha maudhi na utulivu wa akili miongoni mwa wafanyakazi katika kufanikisha utungaji wa mitihani hiyo
Kitendo hicho licha ya kuwa ni kinyume na utawala bora , lakini pia kimekiuka maagizo ya Bodi ya Chuo ambayo yalitolewa tarehe 28/8/2013 (....... mambo yote yanayohusu fedha yaendeshwe kwa uwazi na ushirikishwaji mkubwa miongoni mwa wanaidara / taasisi kwani inaonekana mambo yanaenda kwa usiri mno).
Sababu ya pili amekuwa na vitisho vingi katika utendaji wake na maneno ya kuudhi dhidi ya viongozi wenzake , mfano wa maneno yake ambayo anayatamka huku akigonga meza kuashiria ubabe na kiburi cha madaraka ni kama vile,(.... Ukiingia ndani ya kumi na nane zangu nakumaliza, Angalieni msije mkaumia wengine tunambavu za chuma, Nipo tayari kuua inzi kwenye kioo cha TV hata kama itavunjika potelea mbalimbali raha yangu ni kuhakikisha inzi amekufa, Mkitoboa mtumbwi nitahakikisha kabla sijazama mimi nawazamisha ninyi kwanza, Angalia wengine watakaanga mbuyu na kuwaachia wenye meno watafune, Amekuwa akitishia kung'oa mtu kwa kumwendea (kumpandia)wizarani ndani ya siku mbili na kumchukulia barua ya uhamisho kwenda vyuo vya pembezoni mwa Tanzania, Mimi nafanya haya hata niking'olewa kwa muda mfupi potelea pote nitakuwa nimejenga historia)
Sababu ya tatu ni kutokuwa na uwazi, ukweli na ushirikishwaji kwa njia ya kidemokrasia miongoni mwa idara zake katika chuo hicho na hasa katika fedha ambazo zinakuja kwa ajiri ya manunuzi ya vitu mbalimbali, fedha ya kuendeshea mafunzo ya ualimu kwa vitendo(BTP)
Fedha hiyo licha ya kuchelewesha kuitoa kutokana na ufisadi wake lakini pia hakuitoa yote na wala hakueleza kwa uwazi na ukweli, hali ambayo haikuwezesha wakufunzi kwenda kufanya kazi stahiki kwenye maeneo kusudiwa ya kuwatahini wanachuo ambao walikwenda kwenye shule mbalimbali kwa ajili ya mazoezi ya kufundisha kwa vitendo.
Sababu ya nne ni uwezo wake wa kiuongozi kwani kumekuwepo na mashaka mengi katika Wasifu wake wa kielimu na kiutendaji, hali inayopelekea kuendesha Chuo katika misingi binafsi bila kuzingatia Kanuni, Sheria na Taratibu za Wizara.
Kutokana na hayo yote Chuo hicho kimejikuta kikiingia kwenye mgogoro wa muda mrefu na mkubwa na kupelekea shughuli zote za kiutendaji chuoni hapo kutofanyika katika viwango vyenye ubora na kwa wakati na hasa pale anaposafiri mambo huwa yanasimama, kwani mara nyingi utendaji wote anaufanya yeye mwenyewe na wakati mwingine huwa anajiita Chief Accountant na kumuona Makamu wake kuwa hana uwezo wala mamlaka ya kutoa maamuzi kwa mustakabali wa chuo
Ni mengi ambayo nimeyabaini na ushaidi upo wazi kuwa Mkuu huyo wa Chuo hafai kuendelea kuongoza Chuo hicho kwani Wakufunzi, Wafanyakazi na Wanachuo hawana imani nae, na wanafanya mambo mengi bila morari ya utendaji kutokana na mazingira mabovu ya utendaji kazi katika chuo hicho
Nimefanya jitihada za kukutana na baadhi ya Wakuu wa Idara Chuoni hapo na kupata majibu ambayo yanaonyesha ukataji wa tamaa kutokana na mazingira mabovu ya kiutawala ambayo yanaonyeshwa na Mkuu wa Chuo hicho katika kufanikisha mpango mkakati wa matokeo makubwa sasa,
Pia nimebahatika kuwauliza viongozi wa Bodi akiwemu Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo ambaye amejitambulisha kwa jina la H,Lugome naye pia ameonyesha masikitiko makubwa sana juu ya utendaji wa Mkuu wa Chuo hicho
Lakini pia Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti ambaye pia ameshiriki kusuluhisha mgogoro huo katika kikao chake cha April 27, 2013 lakini ameshindwa na kukata rufaa kwa kulipeleka swala hilo kwa Mkuu wa Mkoa ili aweze kuliingilia kati
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu Philipo Mulugo alipo tafutwa kupitia simu yake ye kiganjani yenye namba hii 0754315922 alijibu kuwa swala hilo bado halijafika mezani kwake na endapo likifika basi atachukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria dhidi ya Mkuu yoyote wa Chuo ambaye atakwamisha malengo na ufanisi wa kazi nchini
Kutokana na hayo na mengine mengi ni dhahiri kuwa utendaji wa kazi katika chuo cha Ualimu Songea kilichopo eneo la Matogoro Mkoani Ruvuma wilayani Songea ni mgumu miongoni mwa Wafanyakazi na kusababisha hali ya sintofahamu katika Saikolojia zao na mustakabali wa Elimu ya wanachuo
Ni vema sasa mamlaka zinazohusika zikachukua hatua stahiki za kumaliza mgogoro huo ikiwemo na kumuondoa Mkuu huyo wa Chuo ili kurudisha Amani na Utulivu chuoni hapo miongoni mwa wanajumuia wanaokizunguka chuo hicho ili kuweza kufanikisha mikakati mbalimbali iliyopo nchini ya kuhakikisha kuwa elimu bora inafikiwa nchini hapa.

Na, Stephano Mango, Songea

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa