Rais Dk. John Magufuli.
Wakati utekelezaji wa mpango wa elimu bure ya Rais
Dk. John Magufuli, ukianza jana, baadhi ya wazazi wamekumbwa na
sintofahamu baada ya wanafunzi kurudishwa nyumbani wakidaiwa michango na
maeneo mengine utitiri wa wanafunzi ukiwa kikwazo, huku kwingine mwamko
wa uandikishaji ukiwa chini.
Mwishoni mwa mwaka jana, serikali ilitoa mwongozi wa elimu ya
msingi (shule ya msingi mpaka kidato cha nne) kuwa wazazi watatakiwa
kununua sare za shule na michezo, madaftari, kalamu, chakula kwa
wanafunzi wa kutwa na kugharamia matibabu ya watoto wao.
Ilisema, watatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa
wanafunzi wa kutwa na wa bweni wakati wa likizo, kununua magodoro,
shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na
wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali.
Hali shuleni, ruvuma
Mkoani Ruvuma, baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya
Sekondari ya Kutwa ya Nandembo iliyopo wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma,
walifukuzwa kwa madai ya kushindwa kuwasilisha michango.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi hao wanaoishi
hosteli iliyojengwa eneo la shuleni hapo kutokana na kuishi mbali na
shule, walisema walifukuzwa kutokana na wazazi wao kushindwa kuchangia
michango ya chakula, kusagia nafaka na michango ya kulipa mpishi.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao, kila mtoto ambaye amechaguliwa kusoma
katika shule hiyo akiwa anatokea vijiji jirani, anatakiwa kuchangia debe
nne za mahindi, moja la mpunga, kilo 30 za maharage, kilo mbili za
chumvi, lita mbili za mafuta, Sh.10,000 kwa ajili ya kusagia mahindi na
Sh. 5,000 za kumlipa mpishi wa shule hiyo.
Wanafunzi Waziri Seifu, Kadiri Ally na Fadhili Rajabu kutoka katika
Kijiji cha Muhuwesi wanaosoma kidato cha pili katika shule hiyo
walisema kuwa wanarudi nyumbani wakiwa hawana matumaini ya kurejea tena
shuleni kuendelea na masomo yao kwa kuwa wazazi wao hawatawapatia
michango hiyo hasa kwa kipindi hiki ambacho makwao wanakabiliwa na
upungufu wa chakula.
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa shule hiyo, Mary Ndunguru, alikiri
kuwarudisha baadhi ya wanafunzi hao ili wakachukue chakula majumbani
kwao kwa madai kuwa hali hiyo imetokana na shule yake kutokuwa na uwezo
wa kuwahudumia watoto hao kwa kuwapatia chakula siku za masomo yao.
Afisa Elimu wa Shule za Sekondari Wilayani Tunduru, Ally Mtamila,
alisema ofisi yake kwa kushirikiana na ya mkurugenzi mtendaji wa
halamshauri ya wilaya hiyo, walikwishapeleka taarifa za maelekezo kwa
madiwani, waratibu elimu kata, yaliyowataka kufanya mikutano ya
kufafanua maelekezo ya serikali juu ya utoaji wa elimu bure.
Mtamila aliendelea kufafanua kuwa kwa mujibu wa maelekezo hayo
kutoka Tamisemi, fedha walizopokea kwa ajili ya utekelezaji wa elimu
bure, katika maelekezo ya fedha hizo za Rais Magufuli, hakuna maelekezo
yanayowataka kuwahudumia wanafunzi wa kutwa chakula.
322 MBOZI WAKOSA MADARASA
Jumla ya wanafunzi 322 wa shule nne za sekondari waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika Wilaya ya Mbozi mkoani
Mbeya, hawataanza masomo na wenzao kufuatia shule zao kukosa vyumba vya
madarasa.
Ofisa Elimu Sekondari Wilaya yai Mbozi, Honsana Nshullo, alisema
majina ya wanafunzi hao yamefichwa, mpaka pale wananchi watakapomaliza
ujenzi wa vyumba vya madarasa ndipo yatakapotolewa, ili waanze masomo na
kuwataka madiwani katika maeneo husika kuharakisha ukamilishaji wa
vyumba hivyo mapema ili wanafunzi hao waanze masomo haraka baada ya
kufanya usaili wa pili.
Alizitaja shule hizo na idadi ya wanafunzi kuwa ni pamoja na
Kilimampimbi wanafunzi 40 (chumba kimoja cha darasa kinahitajika),
Nalyelye wanafunzi 88 (vyumba viwili vya madarasa), Mlowo wanafunzi 64
(vyumba viwili vya madarasa) na Insani wanafunzi 88 (vyumba viwili) na
kwamba katika shule hii hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyechukuliwa.
Aidha, Nshullo alisema pamoja na kwamba serikali imefuta ada na
michango mingine kwa wanafunzi lakini wazazi watakuwa na wajibu wa
kuhakikisha watoto wanapata chakula cha mchana na mahitaji mengine kama
vile sare, daftari na kalamu.
Manispaa ya Dodoma
Uongozi wa Shule ya Sekondari Mbabala iliyopo Manispaa ya Dodoma,
umedaiwa kutoza Sh. 500,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi anayelala
shuleni (boarding).
Akizungumza na Nipashe, Mkuu wa shule hiyo, Gaitan Mwatenga,
alikiri shule kutoza fedha hizo na kudai shule hiyo si ya bweni bali ina
hosteli kwa wazazi wanaotaka watoto wakae shuleni hulipa fedha hizo.
Alisema kiasi cha Sh. 250,000 hutozwa kwa kila mwanafunzi anayekaa
hosteli kwa muhula na kwa mwaka mzazi anatakiwa kulipa Sh. 500,000.
“Mimi sina bweni hapa, nina hosteli na shule zenye hosteli kwa hapa
Manispaa ya Dodoma ni Mbabala, Mpunguzi na Hombolo yaani huwa kuna
nafasi kidogo za hosteli kwa yule anayetaka kuja kukaa anakuja lakini
anatakiwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya gharama ya chakula, wapishi,
matroni, kuni na vitu vingine,”alisema mkuu huyo na kufafanua kuwa bodi
ya shule ndiyo iliyopanga kiwango hicho ambacho ni sawa na mwanafunzi
kutumia Sh.1,500 kwa siku.
Akifafanua suala hilo, Afisa Elimu mkoani hapa, Juma Kaponda,
alikiri shule hiyo kutoza fedha hizo na kudai kuwa ni kwa ajili ya
hosteli sio bweni.
Alisema kinachozungumzwa kwenye elimu bure ni kwa maana ya gharama za uendeshaji na si bure kwa maana ya gharama za mtoto.
Mwamko hafifu simiyu
Katika Shule ya Sekondari Simiyu, iliyoko Kata ya Malambo,
Halmashauri ya Mji wa Bariadi, hadi juzi hakukuwapo mwanafunzi yeyote
ambaye alifika kwa ajili ya kujiandikisha kuanza kidato cha kwanza.
Mmmoja wa walimu wa shule hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake
kwa madai kuwa si msemaji wa shule, alisema hakukuwa na mwanafunzi
yeyote ambaye amerejesha fomu zilizochukuliwa kwa ajili ya kujiunga na
masomo shuleni hapo.
“Shule hii inatakiwa kupokea wanafunzi 220 na ambao wamechukua fomu
mpaka sasa ni zaidi ya 100, lakini hadi leo (juzi) hakuna hata mmoja
ambaye amerejesha fomu kwani mimi ndiye napokea fomu hizo,” alisema.
Pia katika Shule ya Sekondari Kidinda, kata ya Bariadi, Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo, Shija Mayunga, alisema wamepokea wanafunzi watatu tu
ambao alisema walifika na fomu pamoja na mahitaji muhimu kwa ajili ya
kuanza masomo.
“Mwitikio bado mdogo sana mpaka sasa tumepokea wanafunzi watatu tu
na hapa hatuoni dalili za kupokea wanafunzi wengine lakini tuna
matumaini hadi kufika mwishoni mwa wiki hii wanafunzi wanaweza
kuongezeka,” alisema.
Mayunga alisema shule hiyo inatakiwa kupokea wanafunzi 253 na
kuonyesha kushangazwa na wazazi kushindwa kuwapeleka wanafunzi shule
wakati serikali imetangaza elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha
nne.
Katika Shule ya Sekondari Biashara, kata ya Sima, Mwalimu Mkuu wa
shule hiyo, Mathias Joseph, alisema hadi juzi saa 6:40 mchana walikuwa
wamepokea wanafunzi 29 kati ya 337 wanaotakiwa kuripoti shuleni hapo
kuanza kidato cha kwanza.
Alisema mwitikio wa wazazi kupeleka wanafunzi shule ni mdogo
ikilinganishwa na matarajio yao baada ya serikali kuondoa michango
ikiwamo ada.
Mwongozo wa elimu Bure
Mwongozo wa elimu bure uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi, elimu msingi bila malipo, serikali ilikuwa
igharamikie utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa, uthibiti
ubora wa shule, ruzuku ya uendeshaji wa shule ikiwamo ulinzi, umeme,
maji na ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na vifaa vingine vya
kufundishia na kujifunzia.
Serikali pia itagharamikia kununua vitabu, kemikali na vifaa vya
maabara, samani yakiwamo madawati, vifaa vya michezo, matengenezo ya
mashine na mitambo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya shule.
Majukumu ya wazazi
Kwa mujibu wa mwongozo huo, wazazi wanatakiwa kununua sare za
shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwamo madaftari na kalamu,
chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharamia matibabu kwa watoto wao.
Imeandaliwa na Anceth Nyahore, Simiyu, Bosco Nyambege, Mbozi, Stevie Chindiye, Tunduru na Augusta Njoji, Dodoma
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment