Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa amefarijika kuona wazee wanapata huduma za matibabu bure na kwa utaratibu mzuri katika hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa hospitali hiyo wiki hii, alivyokuwa kwenye ziara mkoani humo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema utaratibu wa kutenga chumba maalum chenye madaktari wawili mahsusi kwa ajili ya kuwahudumia wazee unaotekelezwa hospitalini hapo umeondoa adha kubwa kwa wazee kusubiri matibabu kwa muda mrefu jambo ambalo ni kero kwao.
Amesema kuwa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma imethibitisha kwamba agizo la Serikali la kutaka hospitali zote za Serikali nchini ziwe na dirisha maalum kwa ajili ya wazee na watibiwe bure linatekelezeka na kuzitaka hospitali zote nchini kuiga mfano huo.
“Hospitali zote nchini ziige mfano wa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuwaheshimu wazee wanaokwenda kutibiwa katika hospitali hizo kwa kuanzisha dirisha maalum kwa ajili yao kama agizo la serikali linavyosema na wasitozwe malipo ya aina yoyote” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa hata wanapokwenda kuchukuwa dawa uwekwe utaratibu wa kuwapa kipaumbele kwa kuwahudumia kwanza ili wasisubiri kwa muda mrefu. Na kusisitiza kuwa kibali maalum kinachowapa fursa wazee kutibiwa bure hospitalini hapo kindelee kutolewa na kiheshimiwe.
Awali, alitembelea chumba maalum cha wazee ambapo Waziri Mkuu alipata fursa ya kuzungumza na Bibi Antonia Moyo ambaye alisema hajawahi kutozwa fedha wala kukaripiwa wakati wote alipofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu kupitia dirisha la wazee.
Waziri Mkuu Majaliwa, pia ametembelea wodi mbalimbali, chumba cha upasuaji pamoja na duka la dawa kwa wagonjwa wanaotumia huduma za Bima ya Afya.
0 comments:
Post a Comment