Home » » MWALIMU AKUTWA AMEJINYONGA CHUMBANI

MWALIMU AKUTWA AMEJINYONGA CHUMBANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Peramiho, Songea mkoani Ruvuma, Baraka Mwakajila (29), amekutwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia shati ndani ya nyumba alimokuwa akiishi.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea juzi saa sita mchana katika mji mdogo wa Peramiho, nje kidogo ya Manispaa ya Songea.
 
Malimi alisema inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, Mwalimu Mkuu Msaidizi, Rashid Pilly, aligundua kujinyonga kwa mwalimu huyo, baada ya kupita eneo la nyumba aliyokuwa anaishi na kuona nzi wengi wametapakaa kwenye eneo la dirisha la chumba alichokuwa analala.
 
Alifafanua zaidi kuwa Mwalimu Pilly baada ya kuona hali hiyo, alisogea hadi mlangoni na kukutwa mlango ukiwa umefungwa huku eneo hilo likiwa na harufu kali iliyoashiria kuna kitu ambacho kimeoza.
 
Alisema baadaye Mwalimu Pilly alilazimika kwenda kutoa taarifa kwenye kituo kidogo cha Polisi cha Peramiho na baadaye askari polisi wakiwa wameongozana na mganga, walifika eneo la tukio.
 
Baada ya kufika, alisema walivunja mlango na kuingia ndani ya nyumba hiyo ambako walimkuta Mwalimu Mwakajila akiwa tayari ameshakufa muda mrefu baada ya kujinyonga.
 
Alisema Mwakajila alijinyonga ndani ya nyumba ambayo ni mali ya shule na askari walikuta barua chini ya sehemu aliyojinyongea iliyokuwa imeandikwa Januari 4 mwaka huu na mwanamke (jina linahifadhiwa), anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake, ambaye alimtaka aachane naye na aendelee na maisha yake.
 
Malimi alisema polisi baada ya kuiona na kuisoma, waliendelea kuufanyia upekuzi mwili wa marehemu na kukuta pia karatasi kwenye mfuko wa suruali yake, ambayo Mwakajila aliandika Januari 2, mwaka huu, akimtuhumu mpenzi wake huyo kuwa amekuwa malaya na mlevi
 
Kamanda Malimi alisema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo na mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajiki ya taratibu za mazishi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa