UHABA WA DAWA WAITESA SONGEA

na Stephano Mango
BAADHI ya wagonjwa wanaopata matibabu katika kituo cha afya cha Mjimwema kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mkoa wa Ruvuma, wamelalamikia uhaba mkubwa wa dawa kituoni hapo na kusema waganga wanawashauri kununua dawa katika maduka binafsi ambako zinauzwa kwa bei kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wagonjwa hao walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifika kituoni hapo kwa lengo la kutaka kupata matibabu, lakini badala yake wamekuwa wakipewa ushauri wa waganga na kuandikiwa dawa ambazo kwenye kituo hicho hazipo.
Mmoja wa wagonjwa hao, alisema kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na kidonda, lakini kila alipokwenda kwenye kituo hicho kwa ajili ya kusafisha alikuwa akishauriwa akanunue dawa kwenye maduka ya watu binafsi, kwani kituo hicho kina uhaba wa dawa kwa muda mrefu.
Mgonjwa mwingine, alisema alipofika katika kituo hicho akiwa anasumbuliwa na malaria, aliambiwa hakuna dawa na badala yake akaelekezwa akanunue kwenye maduka binafsi.
“Jambo la kushangaza hata Panadol nazo wanadai hawana. Tunaiomba serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuona umuhimu wa kuihimiza Bohari ya Dawa (MSD) kuhakikisha inasambaza dawa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa wakati muafaka, ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi,” alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Dk. Daniel Mtamakaya, alipohojiwa kuhusiana na malalamiko ya wagonjwa hao, alikiri kwa muda mrefu kituo chake hakijapokea dawa kutoka MSD, jambo ambalo amedai limekuwa likileta usumbufu mkubwa kwa wagonjwa.
Dk. Mtamakaya alisema wamekuwa wakilazimika kuwapa ushauri wa kitaalamu wagonjwa, lakini dawa ni lazima waende wakanunue kwenye maduka ya watu binafsi, kwani tangu Juni mwaka huu hawajapata dawa.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea, Nachoa Zacharia, alisema kuna tatizo kubwa la uhaba wa dawa kwenye zahanati zote za manispaa hiyo kikiwamo kituo cha afya cha Mjimwema.
Chanzo: Taaanzania Daima

Wanajeshi Nao Watoa Maoni Katiba Mpya


Baadhi ya wapiganaji wa JWTZ Brigedi ya Kusini wakifuatilia kwa makini Mkutano wao na Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo(jana) katika kikosi cha JWTZ 411 KJ Songea.

Picha na Mjengwa blog

DC MSTAAFU ADAI KUTELEKEZWA

na Julius Konala, Songea
SERIKALI imedaiwa kumtelekeza bila matibabu mpigania uhuru ambaye amewahi kuwa mkuu wa wilaya kadhaa nchini, Josephat Mhagama (75), maarufu kama (Lilikuliku) aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, mkewe, Eva Komba, alisema kuwa Mhagama alilazwa zaidi ya mwaka mmoja bila msaada wowote toka serikalini na kwamba hakuna kiongozi yeyote aliyewahi kumtembelea.
Eva ambaye alisoma darasa moja na Spika wa Bunge, Anne Makinda, katika Shule ya Kati Peramiho, alisema mumewe anasumbuliwa na maradhi mbalimbali yakiwemo matatizo ya kibofu cha mkojo, kwikwi na uti wa mgongo hali inayomfanya alale muda mrefu.
Alifafanua kuwa Mhagama alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji cha Njoomlole, wilayani Namtumbo, na kusoma shule ya kati Peramiho kisha Sekondari ya Kigonsera ambapo alikutana na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alimtangulia darasa moja mbele.
Alisema kuwa baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa kama bwana shamba wa wilaya ya Songea na kuamua kuacha kazi baada ya kutofautiana na serikali ya kikoloni wakati huo kwa vile alitaka usawa kati ya Wazungu na Waafrika ambapo alirudi kijijini Njoomlole na kuwa Katibu wa TANU wa tawi.
“Mwaka 1963 hadi mwaka 1970 mume wangu alikuwa Katibu Mtendaji wa TANU wa Wilaya ya Songea na mwaka 1965 akagombea ubunge katika jimbo la Songea Kaskazini akichuana na Otien Kambona na kumshinda,” alisema Eva.
Aliongeza kuwa mumewe huyo mwaka 1970 aliteuliwa kuwa Katibu wa TANU wa Mkoa wa Dodoma na mwaka 1971 alipelekwa Singida ambako alifanya kazi na hayati Moses Nnauye ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa mkoa huo na baadaye alifanya kazi na Kingunge Ngombale Mwiru.
“Baadaye walihamishiwa Tanga wakati yeye akiwa Katibu wa TANU, Kingunge alikuwa Mkuu wa Mkoa na Oktoba 1975 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, mwaka 1976 akahamishiwa wilayani Biharamulo hadi mwaka 1980 alipohamia Muheza,” alisema.
Eva aliongeza kuwa mwaka 1981 mumewe alihamishiwa wilayani Manyoni hadi mwaka 1983 aliporejeshwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Songea na mwishoni mwaka huo akastaafu na kurudi kijijini kwake Njoomlole.
Chanzo: Tanania Daima

DC AOMBWA KUINGILIA MZOZO WA ARDHI

na Julius Konala, Mbinga
UONGOZI wa Shule ya Sekondari Agustino iliyoko katika wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, umemuomba mkuu wa wilaya (DC) hiyo, Senyi Ngaga, kuingilia kati kutatua mgogoro wa ardhi baina yao na wananchi wenye mashamba yanayozunguka eneo la shule hiyo.
Ombi hilo lilitolewa jana na mkuu wa shule, Moses Mapunda kwa mkuu wa wilaya hiyo wakati akitoa taarifa ya shule yake katika mahafali ya kwanza ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo.
Mapunda alisema mpango wa shule hiyo ni kuendeleza upanuzi na kujenga chuo cha ualimu kwa ngazi ya cheti na stashahada, lakini juhudi hizo zinapingwa na wananchi wenye mashamba yanayozunguka eneo hilo kwa kutaka fidia kubwa ya sh milioni sita kwa shamba la nusu hekari lisilo na zao lolote.
Alisema kuwa serikali imeshayatenga maeneo hayo kisheria kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa taasisi za elimu pamoja na viwanja vya michezo na sio kwa matumizi ya kilimo au makazi, jambo ambalo amemuomba DC Ngaga kushirikisha wahusika wa Idara ya Ardhi pamoja na mthaminishaji wa ardhi wa serikali ili aweze kufanya tathmini ya mashamba hayo kwani mkurugenzi wa shule hiyo yuko tayari kulipa fidia halali.
Mbali na suala hilo, aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuzisaidia vifaa vya maabara, vitabu na fedha shule za watu binafsi pindi inapopata msaada toka nje badala ya kuelekeza nguvu kwenye shule za serikali pekee kwani zote zinatoa mchango mkubwa wa elimu kwa Watanzania.
Akizungumzia kwa upande wa taaluma alisema shule yake imeweza kufanya vizuri ambapo mwaka 2009 shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza kati ya shule zote zilizofanya mitihani ya wilaya kwa kidato cha kwanza ambapo kati ya wanafunzi kumi bora walitoa wanafunzi saba.
Alisema mwaka 2010 shule ilishika nafasi ya kwanza katika mitihani ya kidato cha pili kwa mkoa ambapo ilishika nafasi ya 46 kati ya shule 387 za Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo wanafunzi wote 70 waliofanya mitihani hiyo walifaulu.
Aliongeza kuwa katika matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwaka 2011, walishika nafasi ya pili kati ya shule sita kimkoa na ya 32 kati ya 129 kitaifa kwa shule zenye watahiniwa chini ya 30 na kwamba wanafunzi 11 walifaulu na kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Alizitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa vitabu vya kiada na ziada, vifaa vya maabara na udogo wa eneo la shule na ukosefu wa viwanja kwa ajili ya kufanyia michezo ya wanafunzi, huku akipongeza jitihada zinazofanywa na serikali katika kusogeza huduma ya nishati ya umeme jambo ambalo litawezesha wanafunzi kujifunza masomo ya kompyuta na kujisomea usiku.
Kwa upande wake DC Ngaga alisema kuwa serikali kwa muda mrefu imekuwa ikithamini michango inayotolewa na sekta binafsi katika suala la elimu na kwamba itaendelea kutoa ushirikiano katika hilo kwa kuweka mazingira mazuri.
Chanzo: Tanzania Daima

TTCL YALALAMIKIA WIZI WA NYAYA ZA SIMU

Na Amon Mtega, Songea
MENEJA wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) mkoani Ruvuma, Dadiely Chanachayo, amelalamikia vitendo vya wizi wa nyaya za simu. Malalamiko hayo alitoa mjini hapa jana kutokana na wizi uliojitokeza kwa baadhi ya wananchi kuiba nyaya za simu na kusababishia baadhi ya wananchi kukosa huduma ya mawasiliano.

Alisema wizi huo umesababisha baadhi ya taasisi kushindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi wake ikiwamo Benki ya NMB.

Alisema watu hao wanaiba nyaya hizo kwa ajili ya kutafuta waya wa ndani uitwayo kopa kwa lengo la kutengenezea bidhaa mbalimbali ikiwamo mapambo ya kuvaa mikononi ikiwamo bangili.

Aidha, alisema katika kukabiliana na tatizo hilo wamejiwekea utaratibu wa kutoa zawadi kwa wale watakaotoa taarifa ya watu wanaofanya vitendo hivyo.

Aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuharibu miundombinu ya mawasiliano kwa kuwa kufanya hivyo ni kuisababishia Serikali hasara ambazo hazikustahili.
Chanzo: Mtanzania

MADAKTARI WATAKIWA KUPUNGUZA SAFARI NA SEMINA

Mwandishi wetu, Ruvuma Yetu
 
Madaktari Mkoani Ruvuma wametakiwa kutojilimbikizia Madaraka kwa kujipangia kila Semina na mikutano kuhudhulia wao huku wenzao wakiganga njaa, huo sio Utawala bora.
                    
Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma ameyasema hayo wakati akifungua Semina ya siku 2 ya kutathmini mafanikio na Changamoto zinazoikabili Sekta ya Afya Mkoani Ruvuma.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Hasani Bendeyeko amesema shughuli nyingi ambazo zinatakiwa kufanywa na Madaktari mara zote hukwama kutokana na Madaktari kuwa safarini kuhudhuria semina.

Alisema wakati mwingine daktari mmoja anweza kuhudhuria semina zaidi ya Saba mfululizo na kuacha shughuli za utendaji zikidorora katika hospitali.

Katibu tawala mkoa wa Ruvuma amesema kubadilishana safari nako kunaleta uzoefu kwa anayeenda semina.
 
Blogzamikoa

TANZANIA DAY..FROM SEATTLE WASHINGTON TO RUVUMA ,TANZANIA

Tanzania day ..mwangaza ,Jitegemee
Pictures of two Seattle based organizations ,Mwangaza Jitegemee Foundation (MJF)  and Volunteer group from Woodniville Alliance Church .Trip to Songea Tanzania, highlighting their work  at Songea Women  and Children Care organization (SWACCO), how to help Vulnerable children who in need in the community and hope to continue the efforts of making different

 Swahili food was only serving on that day ..without forgeting , Mandazi, kachumbari, etc .

 Our beautifull Tanzania fabric Khanga, Kitenge, and batiki was the most  shinning  dress on that day, look at the beautifull  models.....

MBUNGE WA PERAMIHO ATOA MSAADA WA PIKIPIKI

Na Amon Mtega, Songea
MBUNGE wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama, ameto msaada wa pikipiki saba zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 10 kwa makatibu kata wa chama hicho wa Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Msaada huo aliutoa jana katika Kijiji cha Lipokela kilichopo Kata ya Mbingamhalule kwa nia ya kuwarahisishia utendaji kazi wao ndani ya chama kwa ajili ya kuendana na mfumo wa siasa za sasa.

Kata zilizonufaika na msaada huo wa pikipiki ni Kikunja, Mtyangimbole, Muungano, Mpandangindo, Mkongotema na Mbingamhalule.

Akikabidhi msaada huo, aliwataka makatibu kata hao kutambua kwamba pikipiki hizo walizokabidhiwa si mali yao binafsi bali zitatumika kwa ajili ya shughuli zote za chama na Serikali, ikiwamo kusaidia kubebea wagonjwa katika maeneo yao.

Aidha, alitoa msaada wa trekta dogo za kulimia lenye thamani ya Sh milioni tisa kwa wananchi wa Kijiji cha Lipokela kama ahadi yake aliyoitoa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoifanya mapema mwaka huu mkoani Ruvuma.

Naye, Diwani wa Kata ya Mbingamhalule, Nasri Nyoni, alimshukuru na kumpongeza mbunge huyo kwa michango yake anayoitoa kwa wananchi, kwa ajili ya kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya jimbo hilo.
Chanzo: Mtanzania

Bi.Fatuma Saidi Ally Azungumza Na Wananchi Wa Kata Ya Kilolo,Mbinga


Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bi. Fatma Said Ally akizungumza na wananchi wa kata ya Kikolo wilayani Mbinga katika mkutano wa Tume hiyo na wananchi leo.
Mjengwa Blog

WANAWAKE WATAKIWA KUACHA UTEGEMEZI

Na Amon Mtega, Songea
BAADHI ya wanawake wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kuacha utegemezi kutoka kwa waume zao na badala yake wajitume kufanya kazi.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Margareth Chacha, wakati akizungumza katika mkutano uliojadili namna ya uanzishwaji wa tawi la benki hiyo.

Alisema kama akina mama wanataka kuheshimiwa zaidi na waume zao, ni lazima waonyeshe jitihada ya kuchangia kipato ndani ya nyumba kwa kufanya kazi na kuachana na tabia ya kuwa tegemezi kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya wanawake.

“Wanawake wenzangu nawaambieni ukiwa unachapa kazi na kusaidia kutoa mchango wa kipato ndani ya nyumba, hakika migogoro ndani ya ndoa zenu huisha, kwa kuwa mwanaume ataona umuhimu ulionao ndani ya familia,” alisema Chacha.

Alisema kwa utafiti uliyofanywa na baadhi ya wataalamu, wamegundua wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi ya kubuni miradi mbalimbali inayoweza kusaidia kuinua maisha ndani ya familia.

Aidha, alisema kuna changamoto wanayokutana nayo ya wanawake wengi nchini kujirudisha nyuma kuwa hawana uwezo wa kufanya kazi ya kuingiza kipato ndani ya familia, kwa kudai hawana pa kupatia mtaji.

Alisema benki hiyo itawahusisha na wanaume kwa lengo la kutojenga ubaguzi ndani ya familia zao, ingawa nembo yake inaonyesha ni ya wanawake.

Alisema ili tawi hilo liweze kufunguliwa, unahitajika mtaji wa Sh milioni 500.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi mkoani Ruvuma, Vestina Ngurusi, alisema kwa sasa wanatoa elimu kwa wanawake hao juu ya uanzishwaji wa benki hiyo na kushughulikia upatikanaji wa jengo na baada ya hapo wataanza kufanya kazi hiyo.
Chanzo: Mtanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe Atembelea Wilaya Mpya Ya Nyasa, Aangalia Mpaka Kati Ya Tanzania Na Malawi






 Mkuu wa Brigedi ya kusini Songea Kanali John Chacha akisamiliana na Waziri wa Mambo ya nje  na ushirikiano wa kimataifa Mhe. Bernad Membe mjini Songea
  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernad Membe   akisalimiana na mjumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Ruvuma Daud Masiko .
 Mzee aliyefahamika kwa jina moja la Ngatunga akizungumza jana wakati wa ujumbe wa wataalamu kutoka Serikalini ulipotembelea ziwa nyasa wilayani nyasa Ruvuma ili kupata ushahidi wa mmiliki halali wa ziwa nyasa ambalo limeziingiza katika mgogoro Malawi na Tanzania.
Mzee Gidion Ndembeka kulia akimuonesha Waziri wa mambo ya nchi za nje Bernad Membe kitabu chenye mipaka halali kati ya Malawi na Tanzania iliyopo ndani ya Ziwa Nyasa. Picha na Muhidin Amri

HOSPITALI YA MKOA WA RUVUMA YA KOSA X-RAY

Mwandishi wetu, Songea
 
Hospitali ya Songea ambayo nitegemeo kwa wakaazi wa Mkoa wa Ruvuma inakabiliwa na Changamoto ya Kukosa mashine ya kupiga picha x-ray kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa.
 
Hayo yamebainika baada ya watu 17 kupata ajali na kushindwa kupata huduma ya upimaji katika hospitali ya hiyo kutokana na mashine ya x-ray kuwa mbovu na kusababisha majeruhi kupelekwa hospitali ya Peramiho songea vijijini kilometa 24 kutoka songea mjini ili kwenda kupata huduma hiyo.
 
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Songea Mathew Chanangula amesema katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Mlima Mkwaya songea vijijini  kati ya watu 17 walio pata ajali hiyo mtoto  mwenye umri wa miaka 2  Daima Rashidi alifariki dunia baada ya kupoteza damu nyingi
 
 
Chanangula alisema wagonjwa waliokimbizwa katika Hospitali ya Peramiho na sabababu zilizomfanya kuidhinisha kwenda kutibiwa huko kuwa ni kutokana wengi kuvunjika mikono miguu na  Majeraha makubwa ambayo yalihitaji vipimo vya x-ray ambavyo havipatikani hospitalini hapo.
 
Majeruhi hao ni wale walionusurika katika ajali iliyotokea barabara ya Mkenda-Songea  Maeneo ya Mlima Mkwaya iliyosababishwa na mwendo wa Kasi na Gari aina ya Center iliyopinduka baada ya kukatika breki na kugonga Land Rover iliyo kuwa mbele yake.
 
Blogzamikoa

TUME YA KATIBA YAHIMIZA WANAWAKE

na Stephano Mango, Songea
WANAWAKE mkoani Ruvuma wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya Tume ya Kukusanya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba ili watoe maoni yao kuhusu changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika jamii.
Wito huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa kundi la tano la tume hiyo, Profesa Mwesiga Baregu, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Songea.
Profesa Baregu alisema kumekuwa na idadi isiyoridhisha ya wanawake wanaohudhuria katika mikutano ya tume kulinganisha na waliopo kwenye kata wanazofika, kwani takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watu 8,915 waliojitokeza katika Wilaya ya Namtumbo na Tunduru wanawake walikuwa 1,949 tu sawa na asilimia 21.9 ya mahudhurio.
“Hii ni idadi ndogo sana kwa akina mama, hivyo tume inatoa wito ili wajitokeze kwa wingi na kuchangia kutoa maoni yao kwa uwazi,” alisema Profesa Baregu.
Alieleza changamoto nyingine waliyokutana nayo ni idadi ndogo ya wananchi wanaotoa maoni kwa njia ya kuongea au kwa maandishi kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika wananchi 8,915 waliohudhuria mikutano mbalimbali, waliochangia ni 2,074 sawa na asilimia 23.3 ya waliohudhuria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Walioba, alisema kuwa wananchi wengi wanaojitokeza kwenye mikutano yao wamekuwa wakilalamika kwamba hawaielewi katiba iliyopo, hivyo ni vigumu kuchangia, ingawa alisema wanaeleza mambo ya msingi yanayohusiana na katiba.
Katika Mkoa wa Ruvuma tume itafanya mikutano 72 katika kata 72 zilizopo kwenye wilaya tano za Nyasa, Namtumbo, Mbinga, Tunduru na Songea.
Chanzo: Tanzania Daima
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa