Home » » HALMASHAURI SONGEA KUPANDA MITI 200,000

HALMASHAURI SONGEA KUPANDA MITI 200,000

Na Amon Mtega, Songea
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea inatarajia kupanda miti rafiki wa maji zaidi ya 200,000 katika vyanzo mbalimbali vya maji na kandokando ya mito kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la ukame.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Ofisa Misitu na Nyuki wa Manispaa hiyo, Robart Mgowole, alipozungumza na MTANZANIA.

Alisema miti hiyo itapandwa katika vyanzo 18 vya maji.

Alisema sababu kubwa iliyosababisha kutokea kwa ukame wa maji katika manispaa hiyo ni kutokana na baadhi ya wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji, ikiwamo kilimo cha bustani za mbogamboga, uchomaji moto katika vyanzo vya Mlima wa Matogoro na mvua chache zilizonyesha mwaka huu ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Alisema sababu nyingine ni uchimbaji ovyo wa mabwawa ya kufugia samaki na wanapojitahidi kuwaelekeza wananchi kuhusiana na athari itakayotokea wanasiasa wamekuwa wakiwaingilia kwa kuwatetea wananchi hao.

“Tumekuwa tukijitahidi kutoa elimu inayohusiana na utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na mazingira yake, lakini tunakwamishwa na baadhi ya viongozi ambao ni wanasiasa huingilia kazi hiyo ya kuwatetea wapiga kura wao huku wakijua wanavunja sheria iliyowekwa,” alisema Mgowole.

Aidha, alisema baada ya kulitambua hilo wamejiwekea mikakati ikiwamo kuwazuia wananchi kufanya shughuli za kilimo ndani ya mita 60 toka katika vyanzo vya maji, kuweka mashindano ya upandaji miti kandokando ya mito na vyanzo vya maji na kuweka ushindani wa uoto wa asili katika vyanzo hivyo.

Aliwataka wananchi waondokane na tabia ya uharibifu wa mazingira, hasa katika vyanzo vya maji badala yake waandae njia bora ya uandaaji wa mashamba yao bila kuathiri mazingira.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa