na Julius Konala, Songea
SERIKALI
imedaiwa kumtelekeza bila matibabu mpigania uhuru ambaye amewahi kuwa mkuu wa
wilaya kadhaa nchini, Josephat Mhagama (75), maarufu kama (Lilikuliku)
aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma sasa.
Akizungumza na
waandishi wa habari hospitalini hapo, mkewe, Eva Komba, alisema kuwa Mhagama
alilazwa zaidi ya mwaka mmoja bila msaada wowote toka serikalini na kwamba
hakuna kiongozi yeyote aliyewahi kumtembelea.
Eva ambaye
alisoma darasa moja na Spika wa Bunge, Anne Makinda, katika Shule ya Kati
Peramiho, alisema mumewe anasumbuliwa na maradhi mbalimbali yakiwemo matatizo
ya kibofu cha mkojo, kwikwi na uti wa mgongo hali inayomfanya alale muda mrefu.
Alifafanua kuwa
Mhagama alizaliwa mwaka 1937 katika kijiji cha Njoomlole, wilayani Namtumbo, na
kusoma shule ya kati Peramiho kisha Sekondari ya Kigonsera ambapo alikutana na
Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alimtangulia darasa moja
mbele.
Alisema kuwa
baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa kama bwana shamba wa wilaya ya Songea
na kuamua kuacha kazi baada ya kutofautiana na serikali ya kikoloni wakati huo
kwa vile alitaka usawa kati ya Wazungu na Waafrika ambapo alirudi kijijini
Njoomlole na kuwa Katibu wa TANU wa tawi.
“Mwaka 1963
hadi mwaka 1970 mume wangu alikuwa Katibu Mtendaji wa TANU wa Wilaya ya Songea
na mwaka 1965 akagombea ubunge katika jimbo la Songea Kaskazini akichuana na
Otien Kambona na kumshinda,” alisema Eva.
Aliongeza kuwa
mumewe huyo mwaka 1970 aliteuliwa kuwa Katibu wa TANU wa Mkoa wa Dodoma na
mwaka 1971 alipelekwa Singida ambako alifanya kazi na hayati Moses Nnauye
ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa mkoa huo na baadaye alifanya kazi na Kingunge
Ngombale Mwiru.
“Baadaye
walihamishiwa Tanga wakati yeye akiwa Katibu wa TANU, Kingunge alikuwa Mkuu wa
Mkoa na Oktoba 1975 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera,
mwaka 1976 akahamishiwa wilayani Biharamulo hadi mwaka 1980 alipohamia Muheza,”
alisema.
Eva aliongeza
kuwa mwaka 1981 mumewe alihamishiwa wilayani Manyoni hadi mwaka 1983
aliporejeshwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Songea na mwishoni mwaka huo akastaafu na
kurudi kijijini kwake Njoomlole.
Chanzo: Tanania Daima
0 comments:
Post a Comment