Home » » TUME YA KATIBA YAHIMIZA WANAWAKE

TUME YA KATIBA YAHIMIZA WANAWAKE

na Stephano Mango, Songea
WANAWAKE mkoani Ruvuma wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya Tume ya Kukusanya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba ili watoe maoni yao kuhusu changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika jamii.
Wito huo umetolewa jana na Mwenyekiti wa kundi la tano la tume hiyo, Profesa Mwesiga Baregu, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Songea.
Profesa Baregu alisema kumekuwa na idadi isiyoridhisha ya wanawake wanaohudhuria katika mikutano ya tume kulinganisha na waliopo kwenye kata wanazofika, kwani takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watu 8,915 waliojitokeza katika Wilaya ya Namtumbo na Tunduru wanawake walikuwa 1,949 tu sawa na asilimia 21.9 ya mahudhurio.
“Hii ni idadi ndogo sana kwa akina mama, hivyo tume inatoa wito ili wajitokeze kwa wingi na kuchangia kutoa maoni yao kwa uwazi,” alisema Profesa Baregu.
Alieleza changamoto nyingine waliyokutana nayo ni idadi ndogo ya wananchi wanaotoa maoni kwa njia ya kuongea au kwa maandishi kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika wananchi 8,915 waliohudhuria mikutano mbalimbali, waliochangia ni 2,074 sawa na asilimia 23.3 ya waliohudhuria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Walioba, alisema kuwa wananchi wengi wanaojitokeza kwenye mikutano yao wamekuwa wakilalamika kwamba hawaielewi katiba iliyopo, hivyo ni vigumu kuchangia, ingawa alisema wanaeleza mambo ya msingi yanayohusiana na katiba.
Katika Mkoa wa Ruvuma tume itafanya mikutano 72 katika kata 72 zilizopo kwenye wilaya tano za Nyasa, Namtumbo, Mbinga, Tunduru na Songea.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa