na Julius Konala, Mbinga
UONGOZI wa
Shule ya Sekondari Agustino iliyoko katika wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma,
umemuomba mkuu wa wilaya (DC) hiyo, Senyi Ngaga, kuingilia kati kutatua mgogoro
wa ardhi baina yao na wananchi wenye mashamba yanayozunguka eneo la shule hiyo.
Ombi hilo
lilitolewa jana na mkuu wa shule, Moses Mapunda kwa mkuu wa wilaya hiyo wakati
akitoa taarifa ya shule yake katika mahafali ya kwanza ya kidato cha nne
yaliyofanyika shuleni hapo.
Mapunda alisema
mpango wa shule hiyo ni kuendeleza upanuzi na kujenga chuo cha ualimu kwa ngazi
ya cheti na stashahada, lakini juhudi hizo zinapingwa na wananchi wenye
mashamba yanayozunguka eneo hilo kwa kutaka fidia kubwa ya sh milioni sita kwa
shamba la nusu hekari lisilo na zao lolote.
Alisema kuwa
serikali imeshayatenga maeneo hayo kisheria kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa
taasisi za elimu pamoja na viwanja vya michezo na sio kwa matumizi ya kilimo au
makazi, jambo ambalo amemuomba DC Ngaga kushirikisha wahusika wa Idara ya Ardhi
pamoja na mthaminishaji wa ardhi wa serikali ili aweze kufanya tathmini ya
mashamba hayo kwani mkurugenzi wa shule hiyo yuko tayari kulipa fidia halali.
Mbali na suala
hilo, aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuzisaidia vifaa vya maabara,
vitabu na fedha shule za watu binafsi pindi inapopata msaada toka nje badala ya
kuelekeza nguvu kwenye shule za serikali pekee kwani zote zinatoa mchango
mkubwa wa elimu kwa Watanzania.
Akizungumzia
kwa upande wa taaluma alisema shule yake imeweza kufanya vizuri ambapo mwaka
2009 shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza kati ya shule zote zilizofanya
mitihani ya wilaya kwa kidato cha kwanza ambapo kati ya wanafunzi kumi bora
walitoa wanafunzi saba.
Alisema mwaka
2010 shule ilishika nafasi ya kwanza katika mitihani ya kidato cha pili kwa
mkoa ambapo ilishika nafasi ya 46 kati ya shule 387 za Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini ambapo wanafunzi wote 70 waliofanya mitihani hiyo walifaulu.
Aliongeza kuwa
katika matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwaka 2011, walishika
nafasi ya pili kati ya shule sita kimkoa na ya 32 kati ya 129 kitaifa kwa shule
zenye watahiniwa chini ya 30 na kwamba wanafunzi 11 walifaulu na kuendelea na
masomo ya elimu ya juu.
Alizitaja
changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa vitabu vya
kiada na ziada, vifaa vya maabara na udogo wa eneo la shule na ukosefu wa
viwanja kwa ajili ya kufanyia michezo ya wanafunzi, huku akipongeza jitihada
zinazofanywa na serikali katika kusogeza huduma ya nishati ya umeme jambo
ambalo litawezesha wanafunzi kujifunza masomo ya kompyuta na kujisomea usiku.
Kwa upande wake
DC Ngaga alisema kuwa serikali kwa muda mrefu imekuwa ikithamini michango
inayotolewa na sekta binafsi katika suala la elimu na kwamba itaendelea kutoa
ushirikiano katika hilo kwa kuweka mazingira mazuri.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment