Home » » MFADHILI ATUMIA BIL. 1/- MIRADI YA MAENDELEO

MFADHILI ATUMIA BIL. 1/- MIRADI YA MAENDELEO

na Julius Konala, Songea
ZAIDI ya sh bilioni moja zimetumika kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo katika Tarafa ya Ruvuma, Wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma iliyofadhiliwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Misheni, Peramiho.
Hayo yalisemwa na mratibu wa Mpango wa Huduma za Afya ya Msingi (HAM) Tarafa ya Ruvuma, Abel Mapunda, wakati wa Jubilei ya miaka 25 ya Dk. Ansgar Stufe OSB, iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Likuyufusi.
Mapunda alisema katika kipindi cha miaka 25 ya utumishi wa Dk. Ansgar alichangia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwamo uboreshaji wa visima vya jadi ili kupata maji safi na salama kwa vijiji vyote vya tarafa hiyo, kuchimba visima vya maji ya pampu na ujenzi wa vyoo bora.
Aliendelea kuitaja miradi mingine iliyofadhiliwa na Dk. Ansgar kuwa ni udhibiti wa malaria kwa kutumia vyandarua vyenye dawa, upimaji wa wanafunzi shuleni kwa kutumia vifaa vya maabara ili kugundua iwapo wana minyoo, kichocho na kiwango cha  damu ambapo watakaokutwa na maradhi hayo hutibiwa bure.
Kwa upande wake Dk. Ansgar aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kuchangia miradi ya maendeleo, nguvu ya mfadhili itumike pale wanaposhindwa kuimalizia huku akibainisha kwamba anao mpango wa kusaidia zaidi maji ya mtiririko katika vijiji vingine.
Alisema licha ya serikali kuipandisha hadhi Hospitali ya Peramiho kuwa ya rufaa tangu mwaka jana hadi sasa haijachangia lolote hali inayosababisha uongozi wa hospitali hiyo kushindwa kujiendesha.
Aliiomba serikali kununua dawa na kulipa mishahara ya watumishi wa hospitali hiyo huku akiweka wazi kwamba bajeti ya hospitali hiyo ni sh bilioni tatu kwa mwaka.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa